Habari za siku ya leo
mpenzi msomaji wa blogu hii. Ni matumaini yangu unaendelea vizuri na shughuli
zako mbalimbali za kila siku. Siku ya leo napenda kukuletea mada inayohusiana
na afya. Tukihusiha binadamu na mada hii , inatusadia kuigawa katika maeneo
makuu matatu yaani mwili, akili na roho. Akili na roho vipo ndani ya mwili.
Akili na roho ni sehemu ya binadamu ambayo haionekani yaani hauwezi kugusa
wakati mwili ni sehemu ya binadamu ambayo inaonekana na unaweza kuigusa mfano
vidole katika mkono unaviona na pia unaweza kuvigusa.
Katika makala hii
napenda kujikita zaidi katika eneo la afya ya akili kwa kuwa ndilo lenye
umuhimu katika kuhakikisha tunaishi maisha yale ambayo tuna shauku ya kuyaishi.
Katika akili ya mwanadamu hapo ndipo kuna kiwanda cha kuzalisha mawazo ambayo
unaona yamebadilisha namna maisha yetu ya kila siku yanavyokwenda. Uwezo uliopo
katika akili ya binadamu ni wa ajabu mno hasa ukiakisi katika kufanya mambo
mbalimbali makubwa na ya kushangaza.
Mtoto anapozaliwa
kimsingi akili yake inakuwa haijalishwa yaani haijaendelezwa vya kutosha
kumuwezesha kufanya mambo mbalimbali. Akili ya mtoto hulishwa kupitia milango
ya fahamu ya macho na masikio kwa kufundishwa mambo mbalimbali na mzazi. Katika
kipindi hichi cha utoto mambo mengi yanayolishwa katika akili yapo chini ya
usimamizi wa mzazi kuamua nini ujifunze na nini usijifunze. Ndiyo kusema hata
kwa sehemu wazazi hutusaidia kufikiri pia kwa niaba yetu katika kipindi hiki.
Ujumbe mkubwa uliopo katika hatua hii ya kwanza kutoka kwa wazazi ni kuwa
wanataka tuwe na mwelekeo mzuri kadiri tunavyokua lakini pia lililo zito zaidi
ni kutujengea mtazamo wa kupenda na kuendelea kujifunza katika kipindi chote
cha maisha yetu.
Pamoja na huo msingi
ambao tunakuwa tumewekewa na ambao
unakuwa unatuongoza mpaka hapo tunapofika hatua ya kuweza kujisimamia wenyewe
si wengi hupenda kuundeleza huo utaratibu wa kupenda na kuendelea kujifunza kwa
kasi na kiwango sawasawa na kile ambacho wazazi wametuwekea ili kuweza kutusaidia
kuwa bora siku hadi siku. Wengi huona kama ndiyo wameshafanya mahafali ya
kujifunza vitu vyote ambavyo wanatakiwa au wanaweza kujifunza katika muda wao
wote wa kuishi hapa ulimwenguni. Na hii kadiri hii tabia ya kutojifunza inavyoendelea kukua hupelekea
kutokuwa na afya ya akili, kutokana na kushindwa kupatia akili chakula ambacho
kingeweza kuzalisha mawazo bora ambayo yangesaidia kupata masuluhisho ya
changamoto mbalimbali ambzo ulimwengu unazipata kwa sasa.
Kipindi ambacho tabia
hii ya kutokujifunza huwa inaanza mara nyingi kwa wale ambao wameajiriwa kwa
mara ya kwanza, yaani wamepata ajira baada tu ya kumaliza masomo yao. Asilimia
kubwa ya watu baada ya kupata ajira ya kwanza huwa na mgando au mapumziko
ambayo hupelekea kabisa kuunda na kuiendeleza hii tabia ya kutopenda
kujiendeleza.
Asilimia
kubwa ya changamoto ambazo unaona unashindwa kuzitatua leo haziwezi kutatuliwa
bila kuwa umeilisha akili yako kwa kiwango cha kutosha ili kuweza kukupatia au
kukuzalishia mawazo yanayoweza kuwa suluhisho kwa hizo changamoto. Ni muhimu
sana kuwa na usimamizi mzuri wa kuamua mambo gani utakuwa unalisha akili yako
kupitia vile unavyoviona na vile unavyovisikia. Chambua video unazoitazama ,
maandishi ambayo unayasoma , na hata yale mazungumzo unayoyasikiliza kupitia
sauti zilizorekodiwa au kusikiliza moja kwa moja, je zina manufaa yoyote au
kuna kitu kinarutubisha afya ya akili yako? Au unavifanya kwa sababu ndio
utaratibu wa kundi la hao ambao unahusiana nao moja kwa moja wanafanya basi na
wewe unafanya.
Miaka mitano ijayo
utakuwa kama ulivyo leo isipokuwa uamue kwa makusudi na kudhamiria kabisa
kubadili mambo makuu mawili ; mambo unayoyasoma na watu ambao unakutana nao.
Uzuri wa maendeleo ya teknolojia yamerahisisha namna ya upataji wa maarifa
mbalimbali mfano blogu hii inakupatia makala mbalimbali ambazo zinalisha akili
yako kila siku. Na kuhusu watu unaokutana nao haina maana wale unaokutana nao
ana kwa ana hata ila dhana nzima imebebwa katika kusikiliza yale unayoambiwa
kwa hivo uwe na uchaguzi mambo gani unayaruhusu yailishe akili yako.