Tuesday, 3 January 2017

Uchambuzi wa Kitabu cha " SOMETIME YOU WIN SOMETIME YOU LEARN"

Mafunzo tunayoyapata kutoka shuleni yanatusaidia kutupa maarifa na msingi wa kutusaidia kutuongoza katika kuelekea maisha yetu nje ya shule au maisha yetu ya kila siku. Ukuaji wa mtu unachangiwa sana na fursa anazojipa katika kujifunza mambo mapya, kujifunza huku kunagunduliwa kutokana na maswali ambayo tunakuwa tunawauliza makocha wetu ili kujua sehemu gani ya kuboresha zaidi. Maisha ni kujifunza.

1. Baadhi ya makosa ambayo tunayafanya yanachangiwa sana na usahaulifu ambao unasababishwa na kutokufanya mambo kwa wakati pale tunapokumbuka kuwa hatujaweka jambo fulani sawa na badala yake tunapuuza na kuahirisha na kuamini tutafanya wakati ujao. Hii huleta gharama kubwa aidha kifedha au muda.

2. Ni vizuri kufikiria kuwa na mlinganyo katika mafunzo tusichague mafunzo ya kufanikiwa tuu , mafunzo yanayotokana na kushindwa ni muhimu pia katika kutujenga kuwa na uwezo wa kuhimili kushindwa bila kuwa na majuto kutokana na kushindwa au kuwa na hofu ya kushindwa kwa mambo yaliyo mbele yetu ya baadaye.

3. Kuna pengo kati ya matendo au kufanya na kujua kile unachopaswa kukifanya, unapoweza kuziba au kuondoa pengo husika ndipo utaweza kufanikiwa

4. Mara nyingi tunafanya ulinganisho kati ya udhaifu tulionao na ubora wa wengine na wakati mwingine hata kinyume chake pia. Ni muhimu kuwa makini na yale unayojisemea binafsi au unafikiri juu yako binafsi

5. Kushindwa au kupoteza kunatarajiwa kutufundisha mambo mengi sana kuliko kututawala na kutufanya tuwe tumezimia moyo au kukatishwa tamaa, kushindwa ni kipindi cha mpito tuu mara baada ya kipindi kupita hatutakiwi kuendelea kubaki hapo.

6. Asilimia kubwa ya watu wanapitia vipindi mbalimbali vigumu, ni katika vipindi hivi hivi wanatarajia kuona fursa iliyojificha katika hali wanazopitia, fursa ya kujifunza, kukua, kukusaidia kusogea viwango vingine, kamwe usikubali kuruhusu kukosa au kushindwa kutumia fursa ya kujifunza katika kipindi kigumu.

7. Majigambo huzuia kujenga roho ya kujifunza kutokana na kuridhika kuona kuwa uko bora kuliko wengine wakati kiuhalisia unakuwa bado unawahitaji wengine pia na kuendelea kujifunza. Majigambo yanakujengea hali ya kulaumu badala ya kukubali kuwajibika.

8. Ni rahisi kufanikiwa mara baada ya kushindwa kunakotokana na kujaribu kufanya jambo kuliko kuweza kufanikiwa kutokana na kutoa sababu za kushindwa kufanya jambo husika. Ni muhimu kufahamu hakuna jambo unalolipata kiurahisi bila kukubali kulipa gharama na kuweka jitihada ya kuweza kulipata jambo husika.

9. Hakuna mtu ambaye kwa namna moja au nyingine hapitii vipindi vigumu katika maisha , kukwepa kupitia vipindi hivi vigumu vya maisha hakutakusaidia kukua, zaidi unapoteza fursa ya kufanikiwa.

10. Ili kuweza kufanya maboresho katika maeneo mbalimbali ya maisha yako unahitaji kujiboresha kwanza wewe binafsi. Suala la kujiboresha binafsi ndiyo linaweka msingi kwa mambo yote mengine ambayo yanayofuata.

11. Hitaji la kiwango cha chini kinachohitajika ili uweze kujiboresha zaidi ni kuamua kutumia angalau kwa saa moja kila siku kwa miaka mitano mfululizo kujifunza katika eneo unalolipenda , basi baada ya hapo utakuwa mahiri katika eneo ambalo umelipenda. Na ni muhimu kujitoa kwa kukusudia na kikamilifu kuhakikisha inajengeka na kuwa tabia.

12. Unapopoteza kitu chochote katika maisha yako, huwa jambo hili haliambatani na furaha, lakini katika mambo ambayo hautakiwi kuyapa nafasi ya kupoteza mojawapo ni tumaini. Haijalishi unapitia hali gani lakini usikubali kutoa nafasi ya kupoteza tumaini katika jambo lolote.

Rafiki napenda kukuarifu kuwa ikiwa una maswali au mada ambayo ungependa niiandikie makala , unaweza tuma katika anuani yangu luckmoshi@gmail.com

Goodluck Moshi
Mwandishi
StadizaMafanikio

0 comments:

Post a Comment