Thursday, 25 June 2015

Kanuni Sita(6) Muhimu Za Kushinda Tatizo Lolote Unalokutana Nalo.

Matatizo mengi kamwe hayatatuliwi au hayadhibiti kwa ufanisi kutokana na kutoyapa uzito wa kutosheleza. Hakuna tatizo ambalo halina umuhimu kiasi kuwa hatuhitaji kujali kuhusu hilo tatizo. Mfano kwa mwanafunzi inawezekena hapati A au B lakini anafaulu. Kwa mwanafunzi anaweza akalipuuzia kwa kigezo kuwa hajafeli.

Kamwe usilipuuze tatizo wala usipuuze uwezo wako wa kukabiliana na tatizo. Tambua kuwa tatizo unalokutana nalo kuna mamilioni ya watu duniani wameshapitia tatizo kama hilo. Ukiwa na mtazamo chanya kuhusu tatizo utabadili tatizo na litakupatia uzoefu. Na unapokosa mtazamo sahihi kuhusu tatizo unalokumbana nalo itasababisha tatizo husika kuwa kubwa zaidi.

Siri kubwa ambayo imewafanya watu waliofanikiwa kuendelea vizuri ni mtazamo juu ya matatizo wanayokutana nayo. Hapa nakuletea kanuni sita kuhusu matatizo na ambazo ukizifanyia kazi ipasavyo wewe pia utakuwa mshindi kwa kuwa kila unapokutana na tatizo utakuwa sehemu ya utatauzi wa tatizo husika.

1. Kila mtu anayo matatizo
Usifikiri ukishafanikiwa utakuwa ndio umeyaaga matatizo, kadiri unavyofanikiwa ndivyo matatizo unayatengeneza mapya. Mafanikio huwa hayaondoi matatizo bali hutengeneza matatizo mapya. Kwa mfano inawezekana unafikiri ukipata kazi fulani ndo utakuwa umefanikiwa Sana, lakini kumbe unaweza kupata hiyo kazi lakini bosi wako akawa ni mkorofi. Sawa suluhisho unaweza kufikiri ni kujiajiri hapo pia utakutana na matatizo ya kushughulika na wafanyakazi wako ili wazalishe zaidi. Kubaliana na uhalisia kuwa Hakuna mtu ambaye yuko huru hana matatizo bali kutegemeana na shughuli unayojishughulisha nayo basi utakutana na matatizo yanayoendana na shughuli husika


2. Kila tatizo lina ukomo wake
Hakuna tatizo ambalo ni la kudumu yaani litakuwepo milele. Muda wa uhai wa tatizo ukiisha litakufa kwa kuisha/kutokuwepo kabisa na litapita. Kila tatizo huwa lina muda wake ambao kiuhalisia ni mdogo kwa hivyo hakuna haja ya kukwepa au kukimbia tatizo kwa kuwa ukikwepa tatizo sio kuwa unatatua tatizo bali unatengeneza matatizo mapya.

3. Kila tatizo lina fursa
Tatizo linaweza kuwa tatizo kwa mtu mmoja ila kwa mtu mwingine linaweza kuwa fursa. Mfano hospitali zipo kwa sababu watu wanaumwa au wanasheria wapo kwa sababu kuna matatizo ya kisheria. Kwa hiyo kwa mgonjwa ana tatizo la kuumwa lakini mtu mwingine amabaye anafikiria kuhusu kutatua matatizo ya magonjwa mbalimbali atafungua hospitali kutibu magonjwa yanayosumbua jamii na hivyo kumpatia fursa kwa kuwa atalipwa anapotoa huduma hiyo.

4. Kila tatizo litakubadilisha
Hakuna tatizo ambalo litakuja katika maisha yetu na kutuacha kama lilivyotukuta. Tatizo litakufanya uamke au uchangamke na usonge mbele. Na hii ni kwa sababu ya wewe kuwa na uwezo wa kuchagua tatizo husika likkufanyie nini katika ujuzi wako, uzoefu wako, au likufundishe nini ili uweze kuwa na uwezo stahihi wa kutatua tatizo husika

5. Unao uwezo wa kuchagua tatizo likuathiri vipi/kwa kiwango gani
Namna ambavyo unavyolikabili tatizo linavyokutokea inaamua pia athari ya tatizo husika kwako.Inawezekana usiwe na uwezo wa kuchagua tatizo linalokutokea lakini unao uwezo wa kuchagua namna unavyolikabili tatizo.


6. Kuna namna chanya na hasi jinsi ya kukabili kila tatizo
Mara zote chagua namna chanya ya kutatua tatizo kuliko namna hasi ya utatuzi wa tatizo. Jambo la msingi ni kuwa kama huwezi kutatua tatizo basi unahitaji kulisimamia kwa ubunifu. Unapotatua tatizo leo unakuwa ni sehemu ya suluhisho la tatizo na hivyo itakupelekea kufaidika na faida zinazoambayana na kutatua tatizo husika.

Kumbuka utatuzi wa matatizo hufanywa rahisi kama matatizo yatachukuliwa au kutazamwa kama changamoto.