Kabla ya kitu chochote
hakijaweza kuwa katika hali yake ya uhalisia huanza katika wazo. Nyumba haiwezi
kujengwa kabla ya kuanza kuwa na mchoro unaongoza ujenzi wa hiyo nyumba. Katika
maana nyingine rahisi unaweza kusema tunafikiri kwanza alafu tunafuata
utekelezaji au kuweka katika matendo kile tunachokifikiri.
Jaribio rahisi ambalo
linaweza kukufanya ujue kama mtu ataishia kuwa tajiri au tayari ni tajiri ni
kwa kutazama yale mambo anayoyafanya kwa kuwa yale anayoyafanya yanaweza
kutabiri matokeo yanayotarajiwa.Mambo anayoyafanya mtu huyafnaya kutokana na
mwongozo anaopata kutoka katika kiwanda chake cha kuzalisha mawazo.
Jaribio lenyewe ni kutazama
mawazo ambayo anayatengeneza kupitia jinsi anavyoilisha akili yake. Chunguza ni
mambo gani au vitabu vya aina gani au majarida ya aina gani au makala za aina
gani huyo mtu anasoma. Katika hivo vitabu au majarida mwangalie vipengele gani
ambavyo anavyovisoma na pia uangalie vipengele gani katika majarida au vitabu
hivyo hivyo huwa havipi mkazo kuvisoma. Katika vile vipengele anavyovisoma
chunguza anavisoma katika mpangilio gani au mfuatano upi?
Jaribio hili unaweza
kulifanya hata kwako binafsi kama kweli una kiu ya kubadili hali yako ya sasa
kuwa tajiri au kama tayari ni tajiri basi kuufanya utajiri wako ukue zaidi.
Watu ambao ni matajiri walio kaa chini kutafakari na kuamua kwa kusudia kuwa
wanataka kuwa matajiri tofauti na wale ambao labda wameshinda bahati nasibu au
wamerithishwa mali huchagua vitabu au majarida ambayo yanaongeza thamani katika
utajiri wao, huchagua vipengele katika majarida au vitabu ambavyo kweli
vinaongeza thamani katika maisha yao, havipi mkazo vipengele vile ambavyo
haviongezi thamani na katika haya majarida au vitabu utagundua huwa wanasoma
viengele vinavyohusiana na fedha au biashara kwanza kabla ya kusoma vipengele
vingine.
Ukitaka kuwa daktari ni
muhimu sana usomee udaktari, au ukitaka kuwa msanifu majengo ni muhimu sana
usome kuhusu masuala ya usanifu majengo ili uwe na uwezo wa kufanya kazi yako
kwa ufanisi na usiwe mbabaishaji katika eneo husika ulilolichagua. Matajiri
wote ambao wamechagua kwa makusudi kuwa matajiri wamejifunza kwa njia
mbalimbali kuhusu utajiri. Mmoja wa wanamafanikio maarufu duniani Jim Rohn
hupenda kusema ukihitaji furaha nenda ujifunze furaha, ukihitaji uhuru wa
kifedha nenda ujifunze kuhusu uhuru wa kifedha, ukihitaji afya bora nenda
ujifunze kuhusu afya bora, orodha hii inaweza kuendelea zaidi lakini Jim
alihitimisha kwa kusema kila kitu unachokihitaji ni kujifunza, ndiyo maana nikasema
kama unataka utajiri jifunze utajiri. Kujifunza huku sio kwa kukaa darasani kwa
sababu mifumo yetu ya elimu haina mitaala inayowaelekeza watu namna ya kuwa
matajiri bali ina mitaala ambayo inawaandaa watu kuwa waajiriwa. Matajiri wengi
waliamua kujiendeleza binafsi kwa kusoma
makala, vitabu na majarida ambayo yanawapatia maarifa ambayo hayajawekwa katika
mitaala ya mifumo wa elimu tulio nao.
Mafunzo makubwa ambayo
wamejifunza ni namna ambavyo matajiri wengine kabla yao jinsi wanavyowaza kwa
kudhibiti malighafi inayotumika katika kiwanda cha mawazo kupitia ulishaji wa
akili zao kwa yale wanayoyasoma, wamejifunza namna matajiri waliotangulia wanavyofanya
kazi, wanavyokula, wanavyoishi , wanavyoweka akiba, wanavyowekeza katika vitega
uchumi mbalimbali.Wamejifunza kwa kujaribu kuongea na watu matajiri ili kuwapa
mbinu za kufanikiwa kwa upande mmoja na kwa upande mwingine kuwaelekeza mambo
ambayo wanatakiwa kuchukua tahadhari ili kuepuka kutetereka. Wamejifunza kwa
kuuliza maswali sahihi, maswali sahihi ni yale maswali ambayo ukiuliza yanaenda
kugusa na kubadili maeneo maisha yako moja kwa moja. Wamesoma mahojiano
mbalimbali ambayo hawa matajiri waliotangulia wameyafanya, wamesoma kuhusu
wasifu wa hawa matajiri waliotangulia. Hayo ndio masomo ambayo wanajifunza
katika chuo cha utajiri.
Kama kweli umeamua kwa
makusudi kabisa unahitaji kuwa tajiri ni lazima ujiendeleze kwa kuwa na uelewa
pamoja na maarifa ya kujitosheleza kuhusu utajiri.