Saturday, 8 October 2016

Uchambuzi wa Kitabu cha " THE 21 IRREFUTABLE LAWS OF LEADERSHIP"

Habari rafiki,
John C. Maxwell ni mmoja wa waandishi maarufu ambao amedumu akitushirikisha mambo mbalimbali ambayo amejifunza katika maisha yake. John ni mwanafalsafa mzuri sana katika eneo la Uongozi. Wiki hii nimepata nafasi ya kusoma kitabu chake kinachoitwa " THE 21 IRREFUTABLE LAWS OF LEADERSHIP". Hapa chini ninakushirikisha maarifa machache kwa muhtasari ambayo nimejifunza kutoka katika kitabu hiki.


1. Mafanikio yoyote ambayo mtu anayapata yanaamuliwa na uwezo wake wa uongozi, ili kuweza kufanikiwa zaidi ni lazima uingie gharama ya kuweka jitihada kujiimarisha katika eneo la uongozi , na hii huwezekana kwa kupitia kujifunza. Uwezo wako wa uongozi unapoongezeka husababisha ufanisi pia kuongezeka.
2. Mambo makuu mawili ambayo yanahitajika kufanyika ikiwa kampuni haifanyi vizuri kibiashara:
(a) Kuwafundisha wafanyakazi wake kuboresha uwezo wao wa kutoa huduma bora ya viwango vya pekee kwa wateja.
(b) Kumfukuza kiongozi ambaye yupo sasa kwa sababu ameshindwa kufanya kazi yake ya uongozi kusaidia kampuni kuweza kufanya vizuri katika biashara.
3. Hakuna mafanikio yoyote ambayo yanaweza kutokea katika kipindi kifupi mfano ndani ya siku moja. Mafanikio yanahitaji nidhamu ya kujifunza kwa uendelevu kidogo kidogo. Muendelezo huu wa kujifunza usio na ukomo au nafasi kwa kuruka kati ya siku moja na nyingine ni sawa na uwekezaji ambao ukiupima kwa kutazama muda tangu umeanza kufanya uwekezaji kwa kujifunza ni gharama uliyolipia ili kuwa sawasawa na uliyojifunza.
4. Kabla hujaanza kufanya mradi au project yoyote ni vizuri kuhakikisha umefanya tathmini kwa upande chanya na upande hasi pia kutokana na uzoefu ulionao ili kama kuna mazuri ambayo uliyafanya kupitia miradi iliyopita uyachukue yakusaidie kupata urahisi wa kufanya mradi wa sasa na kama kuna mabaya ambayo yalikukwamisha yakusaidie kuyaepuka usiyarudie. Washirikishe wataalamu mbalimbali ambao wanaweza kukusaidia kufanya homework kujua vitu vinavyohusiana na mradi unaofanya ili wakusaidie taarifa muhimu zinazohitajika kufanikisha mradi.
5. Kiongozi yoyote hutunza mahusiano na wale anaowaongoza kwa kuhakikisha thamani inapewa kipaumbele. Thamani katika mahusiano ya kiongozi na anawaongoza inaweza kuwa kwa njia zifuatazo:
(a) Kuwathamini unaowaongoza kupitia njia ya kuwajali kwa kufanya mambo madogo kama kuwasalimu, kuwajulia hali na kadhalika.
(b) Kuongeza thamani kupitia yale mambo ambayo umejifunza au unayafahamu lakini wao hawayafahamu. Hapa unawasaidia kwa kuwapa maarifa na hivyo wanakuwa wamepata thamani kupitia kuwa na wewe.
(c) Kuheshimu vile vitu ambavyo wao wanavithamini, kwa kufanya hivi kunajenga mahusiano mazuri na kuona unawaheshimu.
6. Kiongozi anatakiwa kujenga uaminifu kwa watu anaowaongoza, uaminifu hujengwa kupitia matendo ya kiongozi na sio maneno anayoyazungumza kwa watu anaowaongoza. Kiwango cha watu kumwamini kiongozi hudhihirika kupitia heshima wanayompa kiongozi, kiongozi atapata heshima kutoka kwa watu wake ikiwa:
(a) Atafanya maamuzi ambayo yanaleta tija au manufaa kwa ajili ya wale anaowaongoza.
(b) Atakubali kukosolewa pale anapoenda tofauti au kukubali makosa ambayo ameyafanya aidha yawe katika maamuzi ama katika utekelezaji au utendaji.
(c) Atayapa kipaumbele maslahi ya wale anaowaongoza na kuyaweka pembeni na kuuacha maslahi yake binafsi.
7. Kiongozi mzuri ni yule ambaye anaweza kusoma hali au kuelewa nyakati husika wale anaowaongoza wanapitia. Kabla hajatatua tatizo lolote ni vizuri kujitahidi kukusanya taarifa za kutosha ili ziweze kusaidia katika kutumia uwezo wako wa kuongoza kutatua tatizo linalowakabili wale unaowaongoza. Ni muhimu kiongozi kuwa na kitu cha ziada ambacho wale anaowaongoza hawana ili waweze kumheshimu , kumsikiliza na hata kutekeleza maagizo anayoyatoa kwa kuwa wale anaowaongoza wanaamini katika uwezo wake mkubwa alionao wa uongozi katika kuwavusha kutoka hatua waliopo kwenda hatua iliyobora zaidi.
8. Ubora au sifa au uwezo alionao kiongozi unaweza kufahamika kutegemeana na watu wake wa karibu. Kikawaida watu wanavutiwa na kiongozi mwenye sifa zinazolingana na wao au uwezo au ubora kama walionao . Mara baada ya kujitathmini ukiona watu walio karibu na wewe sio wenye vile viwango vinavyofanana na wewe unaweza kuamua kuanza kuwekeza katika kujifunza ili ukuze uwezo wako au ubora wako na hivyo itapelekea kuwavutia na kuwaleta karibu watu ambao mnaendana uwezo au ubora.
Endelea kutembelea blogu hii kujifunza zaidi.

Friday, 7 October 2016

Unawezaje Kutofautisha TABLET na iPAD?

Habari rafiki,
Kutokana na maendeleo makubwa yanayotokea katika teknologia kumekuwa na vifaa vya aina mbalimbali vinatengenezwa ili kusaidia kwanza  kuendana na kasi ya ukuaji katika teknologia lakini pili kurahisha utaratibu wa kawaida wa utendaji kazi kwa kutumia vifaa hivi.
Ni hakika katika jamii yetu utakuwa umekutana na aina za simu ambazo zinakuwa na kioo kikubwa chenye saizi kuanzia inchi saba, nane au zaidi.Aidha kutegemeana na namna mtu husika anavyofahamu ama urahisi wa kutamka kutoka kwa mhusika inachangia sana katika kifaa husika kitakavyoitwa. Aina hizi za simu kitaalamu zinaitwa "Tablet".


Kuna makampuni ya aina mbalimbali ambayo wanatengeneza hizi "tablet". Kwa kuyaorodhesha ni Apple, Nokia,HP, Dell, Lenovo, Toshiba, Asus, Samsung, Google Nexus na kadhalika.
Katika hizi "tablet" kuna programu maalum ambayo inawekwa na mtengenezaji ili kumsaidia mtumiaji kutumia kifaa hiki. Programu hii
inatambulika kwa lugha ya kiingereza "Operating System". Kuna aina tatu maarufu za "Operating System" ambazo zinatumika katika "tablet";
1. Apple iOS
Hii ni "Operating System" ambayo imetengenezwa na kampuni ya Apple. Mara nyingi huwekwa katika bidhaa za kampuni hii tuu.
2. Google Android OS
Hii ni "Operating System" ambayo imetengenezwa na kampuni ya Google. Hizi hutumiwa na kampuni zingine pia sio Google peke yake lakini hazitumiwi na kampuni ya Apple.
3. Microsoft Windows Phone OS
Hii ni "Operating System" ambayo imetengenezwa na kampuni ya Microsoft. Hizi hutumiwa mara nyingi na bidhaa za kampuni ya Nokia.
"Tablet" ambazo zimetengenezwa na kampuni ya Apple zinatumia "operating system" ya iOS. Hizi zinafahamika kwa jina maarufu la "iPad". Ni jina ambalo kampuni ya Apple wanatumia kuzitambulisha "tablet" zao kwa wateja.
"Tablet" zingine ambazo zimetengenezwa na kampuni nyingine kama nilivyoorodhesha hapo juu hutumia "operating system" aidha ya Android au Windows. Hizi ndiyo ambazo hutumia jina la "tablet".
Kwa mfano kama unatumia "tablet" iliyotengenezwa na kampuni ya Samsung si sahihi kuiita iPad bali unapaswa kuiita "tablet" au "Samsung Tablet".
N.B:
Aina nyingine za "operating system" zinazotumika katika simu ni Symbian OS, web OS, Blackberry OS na kadhalika.
Endelea kutembelea blogu hii kujifunza zaidi.

Thursday, 6 October 2016

Tafsiri Sahihi ya Tarehe Zinazoandikwa Katika Bidhaa

Habari rafiki,
Mwili wa binadamu hutumia bidhaa mbalimbali za afya. Kutegemeana na namna ambayo inatumika katika mwili wa binadamu tunaweza kuzigawa hizi bidhaa katika makundi mawili.


1. Kundi la kwanza linahusisha bidhaa ambazo huingia ndani ya mwili wa binadamu. Njia iliyozoeleka au inayotumiwa mara kwa mara kupeleka bidhaa hizi ndani ya mwili ni mdomo. Mfano wa bidhaa hizi ni dawa za kumeza au vyakula vilivyohifadhiwa katika mikebe maalum ya vyakula "food containers".
2. Kundi la pili linahusisha bidhaa ambazo hutumiwa nje ya mwili wa binadamu. Sehemu iliyozoeleka au inayotumiwa mara kwa mara kwa bidhaa hizi kuhudumia mwili ni ngozi. Mfano wa bidhaa hizi ni vipodozi vinavyotumika kwa ajili ya ngozi kama vile "lotion".
Bidhaa hizi zote bila kutegemea zipo katika kundi la kwanza au kundi la pilihuwa zina ukomo wa muda ambao zinaweza kutumika bila kuleta madhara kwa mtumiaji.Hii ina maana bidhaa hizi zikitumika nje ya kipindi ambacho kimeainishwa katika mikebe yake ya kuhifadhia hugeuka kuwa sumu pale zinapotumiwa.
Tafsiri za Alama na Tarehe
1. Mfg au MFG
Hiki ni kifupi cha neno la kiingereza "Manufacturing". Baada ya hili neno hufuata tarehe. Kwa mfano ukikuta bidhaa imeandikwa MFG 22/09/2016 ina maana bidhaa husika imetengenezwa tarehe tajwa mbele ya neno MFG. Hii husaidia kujua muda au umri wa bidhaa kutoka ilipotengenezwa hadi sasa ambapo umeipata.
2. EXP au EXPIRE au USE BY
EXP ni kifupi cha neno la kiingereza "Expire". Baada ya hili neno hufuata tarehe pia. Kwa mfano ukikuta bidhaa imeandikwa EXP 12/12/2016 au EXPIRE 12/12/2016 au USE BY 12/12/2016 ina maana bidhaa husika ikitumika kuanzia tarehe 13/12/2016 italeta madhara kwa mtumiaji. Yaani mtumiaji anatakiwa kuhakikisha hatumii bidhaa husika zaidi
3. BB
BB ni kifupi cha neno la kiingereza "Best Before". Baada ya hili neno hufuata tarehe. Kwa mfano ukikuta bidhaa imeandikwa BB 10/11/2016 ina maana bidhaa husika itapoteza ubora wake kuanzia tarehe 11/11/2016. Mfano wa ubora utakaopotezwa na bidhaa unaweza kuwa rangi au ladha kuonekana tofauti na asili ya bidhaa wakati imetengenezwa.
4. PKG
PKG ni kifupi cha neno la kiingereza "Packaging". Baada ya hili neno hufuata tarehe. Kwa mfano ukikuta bidhaa imeandikwa PKG 07/10/2016 ina maana bidhaa husika imehifadhiwa katika mkebe wake tarehe tajwa.
NB
1. Bidhaa hizi huwa na masharti au maelekezo ya namna salama na sahihi ya kuhifadhi ili ziweze kudumu katika ubora na usalama. Ikiwa masharti yaliyoelekezwa hayatazingatiwa itasababisha bidhaa hizi kuleta madhara pindi zinapotumika
2. Tarehe inaweza kuandikwa katika muundo huu pia 09/2016 au 09/16, hii ina maana sawa mwezi wa tisa mwaka elfu mbili na kumi na sita
Endelea kutembelea blogu hii kujifunza zaidi

Wednesday, 5 October 2016

Je, Unafahamu Kifaa Kinachoitwa Mouse?

Habari rafiki,
Kompyuta huundwa na vifaa vilivyogawanyika katika makundi makuu matatu. Makundi haya yamewekwa kutegemeana na kazi zinazotekelezwa na vifaa vinavyoundwa kundi husika.


1. Kundi la kwanza linajumuisha vifaa vyote vinavyobeba jukumu la kuingiza taarifa katika kompyuta. Katika lugha ya kiingereza vinafahamika kwa jina la "input devices".
2. Kundi la pili linajumuisha vifaa vyote vinavyobeba jukumu la kupokea na kuwasilisha au kuonesha taarifa zinazozalishwa na kompyuta. Katika lugha ya kiingereza vinafahamika kwa jina la "output devices".
3. Kundi la tatu linajumuisha kifaa ambacho kimebeba jukumu la kupokea taarifa ilizozipokea kutoka vifaa vinavyounda kundi la kwanza, kuzichakata kutegemeana na mahitaji yaliyoanishwa na kisha kuwasilisha matokeo kwa vifaa vinavyounda kundi la pili. Katika lugha ya kiingereza kifaa hiki hufahamika kwa jina la "Central Processing Unit" au "Processor".
"Mouse" ni mojawapo ya kifaa ambacho kinaunda kundi la kwanza.
Kutegemeana na teknologia iliyotumika kutengeneza sehemu ambayo waya wa "mouse" unaunganishwa na kompyuta kuna makundi mawili ya kifaa hichi;
1. Kundi la kwanza linatumia teknologia ya PS/2. PS/2 ni kifupi cha neno la kiingereza "Personal System/2 Series". Sehemu hii ya kuunga katika kompyuta huwa katika muundo wa duara. "Mouse" zinazotumia teknologia hii zinaitwa "PS2 Mouse"
2. Kundi la pili linatumia teknologia ya USB. USB ni kifupi cha neno la kiingereza "Universal Serial Bus". Sehemu hii ya kuunga katika kompyuta huwa katika muundo wa pembe nne (mstatili). "Mouse" zinazotumia teknologia hii zinaitwa "USB Mouse"
Kuna kundi lingine la "mouse" ambalo halitumii waya kabisa. Hapa zipo ambazo zinatumia teknologia ya "Bluetooth" na zile ambazo zinatumia teknologia ya "USB"  isipokuwa hamna waya kati ya "mouse" na kompyuta, pia betri huwekwa katika "mouse".
Taarifa inatumwa kutoka katika "mouse" kwenda katika kompyuta kwa njia kuu tatu:
1. Kitufe cha kushoto
(a) Unapobofya kitufe hichi mara moja husaidia kuchagua kitu husika katika kompyuta. Zoezi hili linaitwa kwa lugha ya kiingereza "click".
(b) Unapobofya kitufe hiki mara mbili kwa haraka ndani ya muda mfupi husaidia kufungua kitu husika katika kompyuta. Zoezi hili linaitwa kwa lugha ya kiingereza "double click".
(c) Unapobofya kitufe hiki bila kukiachia zoezi hili linaitwa kwa lugha ya kiingereza "drag"
2. Kitufe cha kulia
Hichi husaidia kitufe cha kushoto. Mara baada ya kuchagua kitu kwa kitufe cha kwanza unaweza kutumia kitufe cha kulia kukupatia uchaguzi zaidi wa vitu unavyotaka kuvifanya.
3. Kitufe cha tatu kipo kati ya kitufe cha kulia na kushoto (Gurudumu)
Ikiwa umeshafungua faili lenye kurasa nyingi kitufe hiki husaidia kutoka ukurasa mmoja kwenda mwingine kwa haraka.
Endelea kutembelea blogu hii kupata maarifa zaidi.

Tuesday, 4 October 2016

Utaratibu Sahihi wa Uandishi wa Saa

Habari rafiki!
Kumekuwa na changamoto katika kujua namna sahihi ya uandishi wa muda kutoka katika saa.Saa ni kifaa ambacho kinatumika kusoma muda ambao huwa katika mpangilio wa kuanza na saa, kisha kufuata dakika na kuishia na sekunde. Sehemu inayopaswa kuandikwa saa huwekwa alama ya HH au hh, wakati sehemu inayopaswa kuandikwa dakika huwekwa alama ya MM au mm, na sehemu inayopaswa kuandikwa sekunde huwekwa alama ya SS au ss.



Mfumo wa Uandishi wa Muda
Kuna njia kuu mbili ambazo zinafahamika kuandika muda unasomwa kutoka katika saa:
1. Mfumo wa Masaa 24
2. Mfumo wa Masaa 12
1. Mfumo wa Masaa 24
Katika mfumo huu saa huanza kuandikwa kwa tarakimu mbili na kisha kufuata dakika ambazo pia huandikwa kwa tarakimu mbili. Kwa kutumia alama utakuta imeandikwa katika namna hii HHMM.
Tarakimu zinazokubalika kuandika sehemu ya HH zipo kati ya 00 hadi 23. Wakati tarakimu zinazokubalika katika sehemu ya MM zipo kati ya 00 hadi 59.
2. Mfumo wa Masaa 12
Katika mfumo huu saa huanza kuandikwa kwa tarakimu mbili, kisha kufuata alama ya nukta mbili ":" , na kuishia na dakika ambazo huandikwa kwa tarakimu mbili. Kwa kutumia alama utakuta imeandikwa katika namna hii HH:MM
Tarakimu zinazokubalika kuandika sehemu ya HH zipo kati ya 00 hadi 12. Wakati tarakimu zinazokubalika katika sehemu ya MM zipo kati ya 00 hadi 59.
Mfumo huu umegawanywa katika vipindi viwili:
(a) A.M
(b) P.M
(a) A.M
A.M ni kifupi cha neno la kilatini Ante Meridiem. Kipindi hichi ni kati ya saa sita usiku (00:00) hadi saa sita mchana (12:00). Ikiwa muda unaouandika upo ndani ya kipindi hiki utapaswa kuandika A.M mara baada ya kumaliza kuandika dakika.
(b) P.M
P.M ni kifupi cha neno la kilatini Post Meridiem. Kipindi hichi ni kati ya saa sita mchana (12:00) hadi saa sita usiku (00:00). Ikiwa muda unaouandika upo ndani ya kipindi hiki utapaswa kuandika P.M mara baada ya kumaliza kuandika dakika.
Mifano
(a) Saa sita usiku itaandikwa 0000 au 12:00A.M
(b) Saa kumi na mbili asubuhi itaandikwa 0600 au 06:00A.M
(c) Saa nne na dakika nane asubuhi itaandikwa 1008 au 10:08A.M
(d) Saa saba mchana itaandikwa 1300 au 01:00P.M
(e) Saa kumi na moja jioni itaandikwa 1700 au 05:00P.M
(f) Saa mbili usiku itaandikwa 2000 au 08:00P.M
(g) Saa nne na dakika arobaini usiku itaandikwa 2240 au 10:40P.M
Endelea kutembelea blogu hii kujifunza zaidi.

Monday, 3 October 2016

Jinsi ya Kutumia Kompyuta Yako Kuwa Chanzo cha Intaneti

Habari rafiki!
Katika makala ya leo ninapenda kukushirikisha namna ya "kushare" intaneti kutoka kwenye kompyuta na kwenda kwenye vifaa vingine vyenye uwezo wa kupokea intaneti.
Kompyuta yoyote ambayo ina kifaa kinachoitwa "Wireless Network Card" inayo uwezo wa "kushare" intaneti ambayo inaipokea kwenda katika vifaa vingine ambavyo pia vinauwezo wa kupokea intaneti bila kutumia waya kati ya vifaa hivyo.
Vifaa vyote vyenye uwezo wa kupokea intaneti bila ya kutumia waya kati yake na chanzo cha intaneti huwa katika maelezo au sifa za kifaa husika utakuta wameandika neno "Wifi" kwa matamshi neno hili linatamkwa "waifai".
Kompyuta ambayo itatumika kama chanzo cha intaneti inatakiwa iwe imewekwa programu ya "Microsoft Windows 7 Operating System"



Hatua za Kufanya:
1. Hakikisha kompyuta yako imewaka na imeshapokea intaneti kwa kutumia waya
2. Nenda upande wa kushoto chini katika "screen" ya kompyuta kisha kwa kutumia kitufe cha kushoto cha "mouse" bofya katika sehemu iliyoandikwa "start" yenye alama kama ya dirisha  yenye rangi nne (bluu,kijani,nyekundu na njano)
3. Tumia "keyboard" kuandika neno "cmd"  katika kiboksi kilichoandikwa maneno yaliyofifia yaliyolala kuelekea kulia yanayosemeka "Search programs and files"
4. Bonyeza kitufe cha kulia cha "mouse" katika sehemu yenye alama nyeusi inayofuatiwa na maneno "cmd" kisha chagua maneno yaliyoandikwa "Run as administrator" kwa kutumia kitufe cha kushoto cha "mouse"
5. (a) Ikiwa mara baada ya hatua ya 4 utaulizwa neno siri basi itabidi     uliandike katika kwa usahihi ili uweze kuendelea. Hii ina maana akaunti unayotumia siyo "Administrator"
    (b) Ikiwa mara baada ya hatua ya 4 itatokea maelezo yenye kichwa "User Account Control" ikikuhitaji uchague kati ya "Yes" na "No", chagua "Yes" ili uweze kuendelea. Hii ina maana akaunti unayotumia ni "Administrator"
6. Katika kiboksi cheusi kilichojitokeza andika neno lifuatalo kisha bofya kitufe cha "Enter" katika keyboard;
netsh wlan set hostednetwork mode="allow" ssid="Intaneti" key="tehama" keyUsage=persistent
7. Ikiwa baada ya hatua ya 6 utapata maneno yaliyoandikwa "The hosted network started" basi andika tena neno lifuatalo kisha bofya kitufe cha "Enter" katika keyboard;
netsh wlan start hostednetwork
8. Rudia hatua ya 2
9. Bofya kwa kutumia kitufe cha kushoto cha "mouse" katika maneno yaliyoandikwa "Control Panel", kisha bofya sehemu iliyoandikwa "View network status and tasks" , kisha bofya tena sehemu iliyoandikwa "Change adapter settings"
10. Bofya kwa kutumia kitufe cha kulia cha "mouse" sehemu iliyoandikwa "Local Area Connection" kisha uchague kwa kubofya kitufe cha kushoto cha "mouse" sehemu iliyoandikwa "Properties"
11. Bofya kwa kutumia kitufe cha kushoto cha "mouse" sehemu iliyoandikwa "Sharing" , kisha bofya kwa kutumia kitufe cha kushoto cha "mouse" ndani ya kiboksi kidogo chenye maneno yaliyoandikwa "Allow other network users to connect..."
12. Bofya kwa kutumia kitufe cha kushoto cha "mouse" sehemu iliyoandikwa "Home networking connection" kisha chagua kwa kitufe cha kushoto cha "mouse" sehemu yenye maneno "Wireless Network Connection 2"
13. Bofya kwa kutumia kitufe cha kushoto cha "mouse" ndani ya kiboksi kidogo chenye maneno yaliyoandikwa "Allow other network users to control..." ili kuondoa alama ya vema ndani ya kiboksi, kisha bofya sehemu iliyoandikwa "OK"
Sasa unaweza kutumia intaneti hiyo hiyo inayoingia katika kompyuta yako kwenda katika vifaa vingine. Jina la intaneti ni lile lililoandikwa katika ssid hapa tumetumia Intaneti na neno la siri litatumika tehama
NB:
1. ssid hili hutumika kutambulisha netiweki yako katika makala hii tumetumia Intaneti
2. key hili ni neno siri utakalotumia kuweka ulinzi na kuamua watu ambao wanaweza kutumia netiweki yako
3. ssid na key unaweza kuandika maneno yoyote unayopendelea
Ili kuendelea kupata makala mpya kadiri zinavyowekwa au kutumiwa vitabu katika mfumo wa nakala tete, unaweza kuandika barua Pepe yako sehemu ya juu kulia iliyoandikwa Jiunge

Sunday, 2 October 2016

Uchambuzi Kitabu cha " DIFFICULT CONVERSATIONS - HOW TO DISCUSS WHAT MATTERS MOST"


Kuna wakati mada ambayo unahitaji kuzungumza na hadhira kuwa na ugumu katika uwasilishaji. Na hii hupelekea kuleta hata hofu kuona kama mahusiano yako na hadhira kuweza kubadilika. Changamoto hii huonekana hasa katika mada ambazo labda hazijazoeleka katika tamaduni za jamii husika au kuona zinagusa hisia moja kwa moja ya hadhira au kuona kama utaonekana ni mtu asiyejali. Majadiliano yenye ugumu namna hii huenda yakatokea katika mazungumzo yanayohusu binafsi, biashara , dini, siasa n.k.
Waandishi wa kitabu hiki wameweka mbinu ambazo zitasaidia kuweza kuwasilisha ujumbe hata kama unaonekana mgumu lakini pia kuendelea kulinda na kuyaboresha mahusiano ya pande zote mbili na kuacha pande zote zikiwa na furaha.



Mambo ya kujifunza na kuyafanyia kazi:
1. Kunapokuwa kuna mazungumzo ambayo yana ugumu ndani yake mara nyingi kunakuwa na mambo ambayo yanafikiriwa na mambo ambayo hayasemwi pia, na hofu ya kusema inatokea kutokana na kuona kuwa utaharibu mazungumzo zaidi, kunakuwa hakuna kuridhika na maamuzi yanayotokana na mazungumzo ya namna hii, maamuzi mengi yanayotokana na mazungumzo haya hufanywa kwa kuwa kiongozi tuu amesema
2. Kuna aina tatu za mazungumzo yenye ugumu:
a) Kitendo: mazungumzo ya namna huleta fikra ya kujiuliza ni nini kimetokea, jambo gani halikufanywa ipasavyo
b) Hisia: mazungumzo haya huhusisha namna mtu atakavyojisikia mfano kudharauliwa, kuumizwa na kadhalika
c) Utambulisho: mazungumzo haya huhusisha haiba ya mtu, yaani mtu amekuonaje kwa nafasi yako
3. Mara nyingi kunakuwa na kulaumu kwa nini upande wa pili umefanya vile umefanya katika shughuli mliyokubaliana na kupelekea kulaumu badala ya kutaka kuelewa kuwa kila mmoja ana mtazamo wake, matatizo yake na hivyo mnahitaji kuheshimu kila wazo la mmoja linapowekwa mezani na linatakiwa lipewe nafasi
4. Kunahitajika kuelewa (dhamira) dhumuni lililonyuma ya kile kilichotekelzwa na sio kuyatazama mambo kibinafsi na kuona kama umedharauliwa na kutoheshimika kwa mawazo au maelekezo yako umeyatoa
5. Ni vizuri pia kuheshimu hisia kutokana na yale yalikubalika kufanyiwa kazi, usifanye kitu kikamuumiza mtu na kuona amegandamizwa badala ya kuona amepewa nafasi ya kutenda ka uhuru na kufanya afurahie yale anayoyafanya
6. Kunapokuwa kuna mazungumzo ambayo ni magumu ni muhimu kuelewa mtazamo wa kila pande na kuona inaleta maana ipi katika lile suala mnalojadili ili kuweza kufikia muafaka , kwa hiyo ni muhimu kila mmoja apewe hiyo nafasi na sio kujibizana tuu maana hii ndo hatua muhimu ya kwanza kuelekea mabadiliko au kukubali mtazamo wa pande ya upinzani
7. Kila mtu anakuwa ana uchaguzi wa taarifa anazozingiza katika akili yake kutegemeana na mvuto alionao na hizo taarifa, kuna uwezekano wote mnaongea mada inayofanana ila kwa jinsi kila mmoja anavovutiwa na kipengele husika utakuta atatoa mchango wa mawazo kutegemeana na maslahi aliyonayo katika eneo hilo
8. Wakati mnapokuwa na mazungumzo magumu ni vizuri kama ukiwa unakataa mawazo ya mtu ukayakataa kwa uwazi, na pia lengo si kuonesha nani ameshinda bali ni kuonesha namna gani kila pande imeeeleweka na mawazo ya kila pande yamrjumuishwa pamoja
9. Kunapokuwa na mada unahitaji kuwasilisha kwa muhusika na ukiwa unafahamu kuwa wewe ndio upo sahihi na yeye hayuko sahihi, njia nzuri ni kwanza kuelewa namna anavyolielewa au kuamini kuhusu lile jambo na pia kufahamu wajibu wako wa kumsaidia ni nini katika hilo suala
10. Kosa kubwa linalofanyika katika mazungumzo huwa ni kufikiri tumepewa nia ya mtu bila kujua kuwa tunakuwa tunaelewa nia ya mtu kupitia hisia tulizonazo kutegemeana na kwamba tunaathirika kwa kiwango gani, inatakiwa hisia hizi ziwekwe pembeni
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako.