Tuesday, 4 October 2016

Utaratibu Sahihi wa Uandishi wa Saa

Habari rafiki!
Kumekuwa na changamoto katika kujua namna sahihi ya uandishi wa muda kutoka katika saa.Saa ni kifaa ambacho kinatumika kusoma muda ambao huwa katika mpangilio wa kuanza na saa, kisha kufuata dakika na kuishia na sekunde. Sehemu inayopaswa kuandikwa saa huwekwa alama ya HH au hh, wakati sehemu inayopaswa kuandikwa dakika huwekwa alama ya MM au mm, na sehemu inayopaswa kuandikwa sekunde huwekwa alama ya SS au ss.



Mfumo wa Uandishi wa Muda
Kuna njia kuu mbili ambazo zinafahamika kuandika muda unasomwa kutoka katika saa:
1. Mfumo wa Masaa 24
2. Mfumo wa Masaa 12
1. Mfumo wa Masaa 24
Katika mfumo huu saa huanza kuandikwa kwa tarakimu mbili na kisha kufuata dakika ambazo pia huandikwa kwa tarakimu mbili. Kwa kutumia alama utakuta imeandikwa katika namna hii HHMM.
Tarakimu zinazokubalika kuandika sehemu ya HH zipo kati ya 00 hadi 23. Wakati tarakimu zinazokubalika katika sehemu ya MM zipo kati ya 00 hadi 59.
2. Mfumo wa Masaa 12
Katika mfumo huu saa huanza kuandikwa kwa tarakimu mbili, kisha kufuata alama ya nukta mbili ":" , na kuishia na dakika ambazo huandikwa kwa tarakimu mbili. Kwa kutumia alama utakuta imeandikwa katika namna hii HH:MM
Tarakimu zinazokubalika kuandika sehemu ya HH zipo kati ya 00 hadi 12. Wakati tarakimu zinazokubalika katika sehemu ya MM zipo kati ya 00 hadi 59.
Mfumo huu umegawanywa katika vipindi viwili:
(a) A.M
(b) P.M
(a) A.M
A.M ni kifupi cha neno la kilatini Ante Meridiem. Kipindi hichi ni kati ya saa sita usiku (00:00) hadi saa sita mchana (12:00). Ikiwa muda unaouandika upo ndani ya kipindi hiki utapaswa kuandika A.M mara baada ya kumaliza kuandika dakika.
(b) P.M
P.M ni kifupi cha neno la kilatini Post Meridiem. Kipindi hichi ni kati ya saa sita mchana (12:00) hadi saa sita usiku (00:00). Ikiwa muda unaouandika upo ndani ya kipindi hiki utapaswa kuandika P.M mara baada ya kumaliza kuandika dakika.
Mifano
(a) Saa sita usiku itaandikwa 0000 au 12:00A.M
(b) Saa kumi na mbili asubuhi itaandikwa 0600 au 06:00A.M
(c) Saa nne na dakika nane asubuhi itaandikwa 1008 au 10:08A.M
(d) Saa saba mchana itaandikwa 1300 au 01:00P.M
(e) Saa kumi na moja jioni itaandikwa 1700 au 05:00P.M
(f) Saa mbili usiku itaandikwa 2000 au 08:00P.M
(g) Saa nne na dakika arobaini usiku itaandikwa 2240 au 10:40P.M
Endelea kutembelea blogu hii kujifunza zaidi.

1 comment:

  1. Nimejifunza kitu.lakini umechanganya maelezo niya kiswahili lakini mfumo wa saa ni wa kiingereza. Elezea kwa saa za kiswahili. Mfano saa moja kamili asubuhi kwa kiswahili na mfumo wa masaa 12 ni 1:00 asubuhi. Je, ktk mfumo wa masaa 24 itaandikwaje?

    ReplyDelete