Saturday, 8 October 2016

Uchambuzi wa Kitabu cha " THE 21 IRREFUTABLE LAWS OF LEADERSHIP"

Habari rafiki,
John C. Maxwell ni mmoja wa waandishi maarufu ambao amedumu akitushirikisha mambo mbalimbali ambayo amejifunza katika maisha yake. John ni mwanafalsafa mzuri sana katika eneo la Uongozi. Wiki hii nimepata nafasi ya kusoma kitabu chake kinachoitwa " THE 21 IRREFUTABLE LAWS OF LEADERSHIP". Hapa chini ninakushirikisha maarifa machache kwa muhtasari ambayo nimejifunza kutoka katika kitabu hiki.


1. Mafanikio yoyote ambayo mtu anayapata yanaamuliwa na uwezo wake wa uongozi, ili kuweza kufanikiwa zaidi ni lazima uingie gharama ya kuweka jitihada kujiimarisha katika eneo la uongozi , na hii huwezekana kwa kupitia kujifunza. Uwezo wako wa uongozi unapoongezeka husababisha ufanisi pia kuongezeka.
2. Mambo makuu mawili ambayo yanahitajika kufanyika ikiwa kampuni haifanyi vizuri kibiashara:
(a) Kuwafundisha wafanyakazi wake kuboresha uwezo wao wa kutoa huduma bora ya viwango vya pekee kwa wateja.
(b) Kumfukuza kiongozi ambaye yupo sasa kwa sababu ameshindwa kufanya kazi yake ya uongozi kusaidia kampuni kuweza kufanya vizuri katika biashara.
3. Hakuna mafanikio yoyote ambayo yanaweza kutokea katika kipindi kifupi mfano ndani ya siku moja. Mafanikio yanahitaji nidhamu ya kujifunza kwa uendelevu kidogo kidogo. Muendelezo huu wa kujifunza usio na ukomo au nafasi kwa kuruka kati ya siku moja na nyingine ni sawa na uwekezaji ambao ukiupima kwa kutazama muda tangu umeanza kufanya uwekezaji kwa kujifunza ni gharama uliyolipia ili kuwa sawasawa na uliyojifunza.
4. Kabla hujaanza kufanya mradi au project yoyote ni vizuri kuhakikisha umefanya tathmini kwa upande chanya na upande hasi pia kutokana na uzoefu ulionao ili kama kuna mazuri ambayo uliyafanya kupitia miradi iliyopita uyachukue yakusaidie kupata urahisi wa kufanya mradi wa sasa na kama kuna mabaya ambayo yalikukwamisha yakusaidie kuyaepuka usiyarudie. Washirikishe wataalamu mbalimbali ambao wanaweza kukusaidia kufanya homework kujua vitu vinavyohusiana na mradi unaofanya ili wakusaidie taarifa muhimu zinazohitajika kufanikisha mradi.
5. Kiongozi yoyote hutunza mahusiano na wale anaowaongoza kwa kuhakikisha thamani inapewa kipaumbele. Thamani katika mahusiano ya kiongozi na anawaongoza inaweza kuwa kwa njia zifuatazo:
(a) Kuwathamini unaowaongoza kupitia njia ya kuwajali kwa kufanya mambo madogo kama kuwasalimu, kuwajulia hali na kadhalika.
(b) Kuongeza thamani kupitia yale mambo ambayo umejifunza au unayafahamu lakini wao hawayafahamu. Hapa unawasaidia kwa kuwapa maarifa na hivyo wanakuwa wamepata thamani kupitia kuwa na wewe.
(c) Kuheshimu vile vitu ambavyo wao wanavithamini, kwa kufanya hivi kunajenga mahusiano mazuri na kuona unawaheshimu.
6. Kiongozi anatakiwa kujenga uaminifu kwa watu anaowaongoza, uaminifu hujengwa kupitia matendo ya kiongozi na sio maneno anayoyazungumza kwa watu anaowaongoza. Kiwango cha watu kumwamini kiongozi hudhihirika kupitia heshima wanayompa kiongozi, kiongozi atapata heshima kutoka kwa watu wake ikiwa:
(a) Atafanya maamuzi ambayo yanaleta tija au manufaa kwa ajili ya wale anaowaongoza.
(b) Atakubali kukosolewa pale anapoenda tofauti au kukubali makosa ambayo ameyafanya aidha yawe katika maamuzi ama katika utekelezaji au utendaji.
(c) Atayapa kipaumbele maslahi ya wale anaowaongoza na kuyaweka pembeni na kuuacha maslahi yake binafsi.
7. Kiongozi mzuri ni yule ambaye anaweza kusoma hali au kuelewa nyakati husika wale anaowaongoza wanapitia. Kabla hajatatua tatizo lolote ni vizuri kujitahidi kukusanya taarifa za kutosha ili ziweze kusaidia katika kutumia uwezo wako wa kuongoza kutatua tatizo linalowakabili wale unaowaongoza. Ni muhimu kiongozi kuwa na kitu cha ziada ambacho wale anaowaongoza hawana ili waweze kumheshimu , kumsikiliza na hata kutekeleza maagizo anayoyatoa kwa kuwa wale anaowaongoza wanaamini katika uwezo wake mkubwa alionao wa uongozi katika kuwavusha kutoka hatua waliopo kwenda hatua iliyobora zaidi.
8. Ubora au sifa au uwezo alionao kiongozi unaweza kufahamika kutegemeana na watu wake wa karibu. Kikawaida watu wanavutiwa na kiongozi mwenye sifa zinazolingana na wao au uwezo au ubora kama walionao . Mara baada ya kujitathmini ukiona watu walio karibu na wewe sio wenye vile viwango vinavyofanana na wewe unaweza kuamua kuanza kuwekeza katika kujifunza ili ukuze uwezo wako au ubora wako na hivyo itapelekea kuwavutia na kuwaleta karibu watu ambao mnaendana uwezo au ubora.
Endelea kutembelea blogu hii kujifunza zaidi.

0 comments:

Post a Comment