Thursday 7 May 2015

Hii Ndiyo Njia Pekee ya Kutatua Matatizo Yako Yote



Habari za siku ya leo mpenzi msomaji wa blogu hii. Ni matumaini yangu unaendelea vizuri na shughuli zako mbalimbali za kila siku. Siku ya leo napenda kukuletea mada inayohusiana na afya. Tukihusiha binadamu na mada hii , inatusadia kuigawa katika maeneo makuu matatu yaani mwili, akili na roho. Akili na roho vipo ndani ya mwili. Akili na roho ni sehemu ya binadamu ambayo haionekani yaani hauwezi kugusa wakati mwili ni sehemu ya binadamu ambayo inaonekana na unaweza kuigusa mfano vidole katika mkono unaviona na pia unaweza kuvigusa.



Katika makala hii napenda kujikita zaidi katika eneo la afya ya akili kwa kuwa ndilo lenye umuhimu katika kuhakikisha tunaishi maisha yale ambayo tuna shauku ya kuyaishi. Katika akili ya mwanadamu hapo ndipo kuna kiwanda cha kuzalisha mawazo ambayo unaona yamebadilisha namna maisha yetu ya kila siku yanavyokwenda. Uwezo uliopo katika akili ya binadamu ni wa ajabu mno hasa ukiakisi katika kufanya mambo mbalimbali makubwa na ya kushangaza.
Mtoto anapozaliwa kimsingi akili yake inakuwa haijalishwa yaani haijaendelezwa vya kutosha kumuwezesha kufanya mambo mbalimbali. Akili ya mtoto hulishwa kupitia milango ya fahamu ya macho na masikio kwa kufundishwa mambo mbalimbali na mzazi. Katika kipindi hichi cha utoto mambo mengi yanayolishwa katika akili yapo chini ya usimamizi wa mzazi kuamua nini ujifunze na nini usijifunze. Ndiyo kusema hata kwa sehemu wazazi hutusaidia kufikiri pia kwa niaba yetu katika kipindi hiki. Ujumbe mkubwa uliopo katika hatua hii ya kwanza kutoka kwa wazazi ni kuwa wanataka tuwe na mwelekeo mzuri kadiri tunavyokua lakini pia lililo zito zaidi ni kutujengea mtazamo wa kupenda na kuendelea kujifunza katika kipindi chote cha maisha yetu.
 



Pamoja na huo msingi ambao tunakuwa tumewekewa  na ambao unakuwa unatuongoza mpaka hapo tunapofika hatua ya kuweza kujisimamia wenyewe si wengi hupenda kuundeleza huo utaratibu wa kupenda na kuendelea kujifunza kwa kasi na kiwango sawasawa na kile ambacho wazazi wametuwekea ili kuweza kutusaidia kuwa bora siku hadi siku. Wengi huona kama ndiyo wameshafanya mahafali ya kujifunza vitu vyote ambavyo wanatakiwa au wanaweza kujifunza katika muda wao wote wa kuishi hapa ulimwenguni. Na hii kadiri hii  tabia ya kutojifunza inavyoendelea kukua hupelekea kutokuwa na afya ya akili, kutokana na kushindwa kupatia akili chakula ambacho kingeweza kuzalisha mawazo bora ambayo yangesaidia kupata masuluhisho ya changamoto mbalimbali ambzo ulimwengu unazipata kwa sasa.
Kipindi ambacho tabia hii ya kutokujifunza huwa inaanza mara nyingi kwa wale ambao wameajiriwa kwa mara ya kwanza, yaani wamepata ajira baada tu ya kumaliza masomo yao. Asilimia kubwa ya watu baada ya kupata ajira ya kwanza huwa na mgando au mapumziko ambayo hupelekea kabisa kuunda na kuiendeleza hii tabia ya kutopenda kujiendeleza.




Asilimia kubwa ya changamoto ambazo unaona unashindwa kuzitatua leo haziwezi kutatuliwa bila kuwa umeilisha akili yako kwa kiwango cha kutosha ili kuweza kukupatia au kukuzalishia mawazo yanayoweza kuwa suluhisho kwa hizo changamoto. Ni muhimu sana kuwa na usimamizi mzuri wa kuamua mambo gani utakuwa unalisha akili yako kupitia vile unavyoviona na vile unavyovisikia. Chambua video unazoitazama , maandishi ambayo unayasoma , na hata yale mazungumzo unayoyasikiliza kupitia sauti zilizorekodiwa au kusikiliza moja kwa moja, je zina manufaa yoyote au kuna kitu kinarutubisha afya ya akili yako? Au unavifanya kwa sababu ndio utaratibu wa kundi la hao ambao unahusiana nao moja kwa moja wanafanya basi na wewe unafanya. 

Miaka mitano ijayo utakuwa kama ulivyo leo isipokuwa uamue kwa makusudi na kudhamiria kabisa kubadili mambo makuu mawili ; mambo unayoyasoma na watu ambao unakutana nao. Uzuri wa maendeleo ya teknolojia yamerahisisha namna ya upataji wa maarifa mbalimbali mfano blogu hii inakupatia makala mbalimbali ambazo zinalisha akili yako kila siku. Na kuhusu watu unaokutana nao haina maana wale unaokutana nao ana kwa ana hata ila dhana nzima imebebwa katika kusikiliza yale unayoambiwa kwa hivo uwe na uchaguzi mambo gani unayaruhusu yailishe akili yako.