Thursday 2 July 2015

Sifa Unazotakiwa Kuzitambua Kwa Kiongozi Anayeweza Kuleta Mabadiliko

Habari na karibu ndugu mpenzi msomaji wa blogu hii. Ni matumaini yetu umekuwa na wiki ya mafanikio sana.
Leo tutaangalia sifa unazotakiwa kuzitambua kwa mtu unayetaka awe kiongozi au unamtegemea awaongoze.

  1. Tabia
Mtu mwenye tabia nzuri au njema anakuwa na uaminifu, utiifu, nidhamu, kutegemewa, uvumilivu, kujitambua na pia anakuwa na bidii katika kazi.Wakati kwa upande mwingine mtu asiye na tabia njema au nzuri anakuwa hana uwezo wa kuwajibika kwa matendo yake, hawezi kukamilisha kazi kwa wakati, na pia hatimizi ahadi au majukumu yake.

  1. Kuhamasisha
Mtu ambaye anajua wapi anaelekea anakuwa na uwezo wa kuhamsisha wengine wafuatane nae kutokana na ahadi au mambo mazuri yanayopatikana kule anakoelekea. Kwa hiyo unahitaji kuangalia mtu Yule ambaye anafuatawa na watu wazuri na sio wale walio wa kawaida kabisa pia angalia huyu mtu anamtazama nani kama mtu anayemhamasisha bila shaka kwa Yule anayefaaa kuwa kiongozi utamkuta anamfatilia mtu ambae pia ni kiongozi na ana sifa njema

  1. Mtazamo chanya
Tafuta mtu Yule ambaye hana vizuizi katika akili yake kwa kuona jambo Fulani haliwezekani bali awe ni Yule mwenye nia ya kujaribu pamoja na kuwaza chanya kuwa atafanikiwa katika lile atendalo na anakuwa hazuiwi na vikwazo binafsi.

  1. Ufanisi mzuri katika kuwasiliana
Viongozi wazuri ni wale ambao wanaweza kuwasiliana vema, wanakuwa wanajihusisha vema na wale wanaoongea nao kwa kuweza kumtazama ana kwa ana pamoja na kuwa na tabasamu kwa Yule anayeongea naye. Kiongozi mzuri si Yule anayeweza kuwasilisha ujumbe wake lakini pia anakuwa na uwezo mzuri wa kusikiliza pia wale anaowaongoza.

  1. Kujiamini
Bila kujali hali gani katika wakati husika kiongozi pamoja na kundi wanapitia , kiongozi mzuri ni Yule anayekuwa anayejiamini na kuwa na ujasiri kuwa yeye pamoja na timu anayoiongoza wanaweza kusogea hatua kutoka walipofika

  1. Nidhamu
Kiongozi ni Yule mwenye nidhamu anayeweza kutawala hisia zake na pia ana uwezo wa kusimamia au kutawala muda wake jinsi ya kuutumia ili kumsaidia kupata mafanikio kwa ajili yake na timu anayoiongoza

  1. Rekodi nzuri ya mafanikio

Ni vizuri ukacheki historia yake ya nyuma ya utendaji wa mtu. Na kiongozi mzuri utakuta ana rekodi nzuri ya utendaji 

Jinsi ya Kujua Kama Unachofanya Ni Sahihi Katika Maisha Yako

Kila mtu anapokuja hapa ulimwenguni anakuwa amebeba maagizo maalum ambayo anatakiwa ayatekeleze kwa ajili ya kufanya ulimwengu kuwa sehemu bora ya kuishi. Njia nzuri ya kuweza kujua kile unachofanya kama ni sahihi ni kwa kuyafahamu maagizo uliyobeba ambayo hakuna mwingine zaidi yakeo anaweza kuatekeleza. Na maagizo hayo unaweza kuyafahamu kwa kuanza kujitathimini kwa njia ya maswali kama je umeshatambua maagizo uliyoyabeba? Au je una kipaji, uwezo, shauku gani ambayo ni ya kipekee kwako na hakuna mtu mwingine wa aina yoyote anayo isipokuwa wewe tu? Au ya mwisho ambayo ni nzuri zaidi ni kwa kuangalia kile unachokifanya na kujiuliza je unachokifanya ndicho ulichokusudiwa au sababu ya wewe kuwepo hapa ulimwenguni?
Hapa ninakuletea viashiria ambavyo vitakusaidia kujitathmini kama kwanza upo katika kada au eneo sahihi lakini la muhimu zaidi ni lile unalofanya katika hilo eneo ndilo lile unalopaswa au sababu yaw ewe kuwepo hapa ulimwenguni.
  1. Unakuwa unapenda kile unachokifanya kwa kuwa kinakuvutia , kinakupa shauku na mvuto wa kipekee kukifanya
  2. Unakuwa unataka kuwa bora sana katika kile unachokifanya. Na miongoni mwa asilimia kumi ya watu walio bora katika eneo au kada yako unataka na wewe uwepo
  3. Unawapenda wale wote ambao wako katika eneo au kada uliyopo na pia unapenda kufikia mafanikio ambayo wao pia wameyafikia
  4. Unapenda kujifunza kuhusiana na hilo eneo au kada yako kwa kusoma mambo yanayohusu kada yako, kuhudhuria semina au mihadhara ambayo inazungumzia mambo yanayohusu eneo au kada yako, kusikiliza program za sauti zilizorekodiwa kuhusiana na kada yako. Na zaidi hata iweje unakuwa huchoki kujifunza katika hilo eneo lako.
  5. Kada au eneo sahihi kwako ni lile ambalo kwako ni rahisi kujifunza na pia ni rahisi kuweka katika matendo yale uliyojifunza. Ila kwa wengine inaonekana ni vigumu na kwako inakuwa kawaida sana kufanya.
  6. Kutokana na kufurahia kile unachofanya unakuta muda unakuwa kama umesimama kwako na inaweza ikawa imekukolea sana hadi unasahau kula, kunywa hata kwend mapumziko
  7. Mafanikio unayoyapata katika eneo ndiyo inayokupa hamasa ya kipeekee na furaha adimu. Na pia unakuwa huwezi kuacha kusubiri au kukaa muda mrefu bila kufanya kitu kikusogeze hatua moja mbele upate mafanikio mengine
  8. Unapenda kufikiri kuhusu hilo eneo au kada yako na pia wakati haufanyi kitu unapenda kuzungumza kuhusu eneo au kada yako. Masiha yako yote yanakuwa yamezngukwa na mambo yanayohusu eneo au kada yako
  9. Unapenda kuwa na mahusiano na kuwa karibu na watu zaidi ambao wapo katika eneo lako.
  10. Na mwisho ni kuwa unapenda kufanya hayo unayofanya kwa maisha yako yote, hutaki kustaafu kuyafanya kwa kuwa unafarahia jinsi unavyoyafanya

Kwa kuweza kutambua eneo au kada yako sahihi ambayo unatakiwa uwe itakusaidia kupata mafanikio nah ii itakusaidia kuwelekeza moyo wako kufanya vizuri na vizuri zaidi. 

Hatua Saba (07) Muhimu Za Kukamilisha Malengo Yako Makubwa

Watu wengi hufikiri kuwa na lengo lilio fasaha pamoja na kuwa na mtazamo chanya kuhusiana na ukamilishaji wa lengo ndio msingi mkuu wanaohitaji ili kuweza kuwa na furaha pamoja na kufanikiwa. Lakini kumbe hata kabla hujaanza safari yako ya kukamilisha lengo lako ni muhimu kuwa na mipango hatua kwa hatua inayokuhakikishia uwezekano mkubwa wa kukamilisha lengo lako.



Haa ninakuletea hatua saba zitakazokuwezesha kukamilisha lengo lolote ambalo unajiwekea

  1. Amua ni nini hasa unakihitaji katika kila eneo la maisha yako. Unahitaji kufafanua lengo lako katika lugha rahisi kiasi kwamba motto mdogo aweze kuelewa. Mfano unaweza kusema lengo lako ni kuwa na fedha nyingi, lakini uwingi wa fedha unazotaka haujaweka ni fedha nyingi kiasi gani. Sasa kutokuwa fasaha katika lengo kunakupelekea kutokuwa na hamasa na kufanya maamuzi ya kukamilisha lengo.
  2. Andika lengo lako na lifanye liwe linaweza kupimika. Lengo ambalo halijaandikwa linakuwa ni lengo ambalo halihuishwa au halijapewa nguvu ya kuwa hai.Ukilifanya lipimike maanake unakuwa umetengeneza tageti unayotaka kuifikia.
  3. Weka ukomo wa kukamilisha. Unahitaji kuwa fasaha ni lini unahitaji kukamilisha lengo husika. Sehemu ya ubongo inayoitwa “subconscious”  inapenda kuwa na ukomo nah ii inakusaidia kuwa na nguvu na kukupa hamasa ya kuelekea kufanikisha lengo husika
  4. Ainisha vikwazo ambavyo unahitaji kuvivuka ili kukamilisha lengo. Fahamu kitu gani kinaweza kwenda tofauti. Fahamu ni kitu gani kipo kati yako na lengo. Fahamu kwa nini bado haupo katika lengo lako.
  5. Tambua maarifa na ujuzi wa ziada ambao utahitaji ili kuweza kufikia lengo lako. Ili kuweza kufanikiwa kukamilisha malengo ambayo hujawahi kuyakamilisha hapo kabla unahitaji kujifunza na kuwafanya vitu vya tofauti ambavyo hujwahi kufanya kabla.
  6. Watambue watu ambao utwahitaji wakusaidie au waungane nawe ili uweze kufikia malengo yako. Kufikia malengo makubwa unahitaji kuwa natimu ya watu wengi wa kukusaidia. Kwa hiyo unahitaji kuwa na ufasaha ni watu wa aina gani hasa unaowahitaji ili uweze kuwa na timu ambayo itakupa msada unaouhitaji.
  7. Tengeneza orodha ya maelezo kwa kila kipengele ambavyo nimeanisha hapo juu na uweke mpangilio katika mfuatano yaani kipi kinaanza na kipi kinafuata na pia ni muhimu kuwa na kipaumbele. Ni muhimu kujua kipi unahitaji kwanza, kipi ni muhimu.

Baada ya kukamilisha hatua hizo saba ni muhimu kufanya kila siku japo kwa udogo sehemu ya kufikia lengo lako.

Aina Tano (05) za Uwekezaji Zinazoweza Kubadili Maisha Yako

Ili kuweza kuwa na utajiri endelevu katika maisha yako na unaojitosheleza ni muhimu ukawa mwekezaji. Uwekezaji upo wa aina nyingi. Hapa ninakuletea aina za uwekezaji unazoweza kuzifanya ili kukuwezesha wewe na wale watu wako wa karibu kuishi maisha ya utajiri wa kujitosheleza:




  1. Uwekezaji binafsi
Watu ambao wanatengeza utajiri wanafanya uwekezaji binafsi . hawa wanakuwa wasomaji kwa kujifunza. Daima huweka jitihada ya kujiboresha wao wenyewe siku hadi siku na kuongeza mipaka ya maeneo ambayo wanona wakijaribu watafanikiwa. Wanaongeza maarifa na uwezo wa kushawishi siku hadi siku. Na kiwango cha jitihada wanachoweka katika kujiboresha huwa kipo katika hali ya kukua siku hadi siku.

  1. Kuwekeza kwa wengine
Mwanamafanikio maarufu duniani Zig Ziglar alisema ukitaka kupata kitu chochote katika maisha ni vizuri uwasaidie wengine wapate vile wanavyovihitaji katika maisha yao. Watu wenye utajiri utagundua wamewekeza kuwasaidia wengine wafikie malengo yao na hivyo kusababisha na wao kufanikiwa kwa kuwafanikisha wenzao

  1. Wekeza katika taasisi
Katika taasisi unayofanya wekeza katika kuijenga taasisi hiyo ili iweze kuwa bora na taasisi inapoweza kuwa bora inawezesha kuongeza upataji wa mapato. Kuongezeka kwa mapato kwa taasisi kwa ujumla kunasaidia pia wale waliosababisha kuongezeka kwa mapato kuneemeka na hiyo faida. Kwa hivyo hili likifanyika katika kipindi chako cha kutumikia taasisi yako maanake utaongeza kujenga utajiri siku hadi siku.

  1. Wekeza katika mali zinazoongezeka thamani
Ubadilishaji wa fedha kwenda katika mali ambazo zinaongezeka thamani na zinafanya kazi badala yako siku hadi siku huongeza utajiri kwako. Mfano wa hili ni nyumba ambayo imejengwa kwa lengo la kupangasha au kukodisha. Sasa ile fedha uliyowekeza katika hiyo nyumba utaipata kwa kuendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka bila yaw ewe kufanya kazi.

  1. Wekeza katika mawazo

Vitu vingi tunavyoviona leo havikuanza moja kwa moja bila kupitia hatua Fulani, vingi vilianza kama wazo na kuendelezwa. Mawazo amabyo ni mazuri yakichanganywa na uchukuaji hatua wa kuyaweka katika matendo huleta matokeo mazuri ambayo yanaleta utajiri 

Hatua 6 za Kuwalea Viongozi Watarajiwa (Chipukizi)

Habari na karibu ndugu mpenzi msomaji wa blogu hii. Ni matumaini yetu umekuwa na wiki ya mafanikio sana. Ni dhahiri umekuwa ukipata mlo kamili wa akili siku hadi siku kupitia blogu hii. Ninachopenda kukuhamasisha jitahidi katika kila makala inayowekwa hapa tafuta vitu vichache ambavyo vitafanya tofauti kubwa inayoweza kuonekana waziwazi au inayoweza kupimika katika maisha yako na vitu hivo viwe ni rahisi kuanza na kuendelea navyo kadiri unavyosafiri katika safari yako ya kuelekea mafanikio.

Leo nitazungumzia namna ya kuwalea watu wenye sifa za uongozi ambao umewatambua upo nao katika timu yako katika taasisi, ambapo nitakuwa pamoja nawe kukupitisha katika hatua sita za muhimu.


Kwanza, ili kuwa na viongozi wazuri unahitaji kuwapa muda; ukiwa kama kiongozi ambaye unaandaa viongozi watarajiwa unahitaji kuwaamini wale unaowaandaa kwa kuwatamkia wazi wazi na kuwatia moyo namna ambavyo unaamini katika uwezo wao wa kutenda mambo wanayoyafanya na hii itaanza kuwahamasisha na kuwafanya pia wajiamini binafsi. Unahitaji kujitolea ukiwa unamaanisha na kuwepo kwa muda watakaohitaji uwashauri.

Pili, kuwa na msimamo thabiti, bila kujali hali inayojitokeza unahitajika kuwaonyesha msimamo wako  ambao hauyumbishwi na unakuwa katika kiwango kile kile kila mara katika utoaji ushauri, kujitolea muda wako na kuwahamisha. Hii itawasaidia kujenga uaminifu au kukuamini wewe.

Tatu, tambua kufanikisha kwao, waonyeshe kile wanachofanya kina umuhimu na thamani kwako wewe kama kiongozi wao na pia kwa taasisi.Namna rahisi ambayo unaweza kuongeza umuhimu katika kazi wanayofanya hawa unaowaandaa kuwa viongozi ni kuwahusisha kuwa sehemu ya kitu cha thamani kwa kuwapa picha kubwa ambayo taasisi husika imekusudia kuifikia na namna gani wao ni sehemu muhimu ya kufanikisha hilo kufanikiwa.

Nne, wapatie usalama, watu wakifahamu kuwa wapo sehemu salama ni rahisi kuwa na utayari wa kukua, kujiendeleza kwa kujifunza, na hata kuchukua hatari kwa ajili ya kujiboresha wao wenyewe.

Tano, toa tuzo kwa ufanikishaji wa jambo lolote, unahitaji kuwafanya wajue nini matarajio yako na ni tuzo gani watapata au zinawasubiri kwa wao kufanikiwa kufikia au kuzidi matarajiao yako hii itawafanya wajitume kufikia hayo matarajio uliyoyaweka. Na ni vizuri kuhakikisha wanapewa tuzo stahiki ambazo zifanyike kwa njia ya wazi kutegemeana na taratibu mlizoziweka na si lazima ziwe ni za kifedha tuu bali zinaweza kuwa za kutambua mchango wa watu husika katika kufanikisha jambo katika taasisi. Kwa kuwapatia tuzo kwa kazi nzuri iliyofanywa itawasadia kujisukuma kufanya vizuri zaidi.


Sita, wapatie msaada au waunge mkono, hakuna kitu ambacho kinaumiza kama kuwapa watu kazi waifanye na huwapatii msaada wanaostahili na rasilimali wanazozihitaji ili kufanikisha kazi uliyowapa. Tengeneza mfumo mzuri wa wao kupata msaada kutoka kwako na msaada unaweza kuwa ni wa kuwahamasisha, kuwajali, kifedha, kiujuzi, mafunzo au hata kifaa sahihi cha kuwarahishia kazi au mtu wa kuwaongezea nguvu. 

Jinsi ya Kuwaandaa Kuongoza Viongozi Watarajiwa (Chipukizi)

Habari na karibu ndugu mpenzi msomaji wa blogu hii ya. Ni matumaini yetu umekuwa na wiki ya mafanikio sana.


Leo nitazungumzia namna ya kuwaandaa watu wenye sifa za uongozi ambao umewatambua upo nao katika timu yako katika taasisi. Kuwaandaa viongozi hawa watarajiwa kunahusisha wewe ambaye tayari ni kiongozi pamoja na hao viongozi watarajiwa , nah ii inaweza kulinganishwa kwa kiasi Fulani kama unawawapatia mafunzo.

  1. Tengeneza Mahusiano na Viongozi Chipukizi Unaowaandaa
Viongozi chipukizi ambao umeshawatambua unahitaji kuwafahamu, kuwasikiliza historia za maisha yao ili uweze kuwajua zaidi ya vile unavowajua tu kiofisi. Huhitaji kujua kuhusu uwezo au ubora wao tu bali unahitaji pia kujua kuhusu madhaifu yao pia ili uweze kujua namna ya kuwafanya wakamilifu kwa hayo mapungufu uliyoyatambua. Na ukiweza kujenga mahusiano mazuri maanake utafanya wakupende na pia kuongeza nia na kiu kwao kujifunza kutoka kwako

  1. Washirikishe ndoto yako
Wakati unaendelea kuwafahamu usiwaache wao peke yao tu wakuambie ya kwao, na wewe pia unahitaji kuwashirikisha pi historia ya maisha yako na unahitaji kwenda hatua ya ziada kwa kuwashirikisha ndoto yako kuhusiana na taasisi ambayo unaiongoza. Na hii itawasaidia kujua ni wapi unataka kwenda na hivo kujiunga kujitoa kufuatana nawe mpaka mwisho wa safari yako

  1. Waombe utayari wao kujitoa kiuongozi
Moja ya kiungo muhimu ambacho kinaweza kumfanya kiongozi chipukizi kuwa kiongozi mwenye mafanikio, ni utayari wa kujitolea kiuongozi. Ni muhimu sana kwa hawa viongozi chipukizi unaowaandaa wawe wamejitoa kwa ajili ya uongozi pamoja na taasisi. Na unahitaji kuwaeleza gharama ambayo itawachukua kwa wao kuwa viongozi, na jambo la muhimu ni uwe mkweli kuhusu mambo ambayo watahitaji kuzingatia au kuyajua hata kabla ya hatua yenyewe ya kufanya maamuzi ya kukubali kuweza kujitoa kiuongozi.

  1. Weka malengo kwa ajili ya ukuaji
Viongozi hawa chipukizi wanahitaji kujua malengo yaliyo fasaha ambayo wanatakiwa kuyapigania au kuyafanikisha, nah ii itawasaidia kujua ni nini wnatakiwa kufanya na pia ni vitu gani vinatarajiwa kutoka kwao. Jambo muhimu zaid la kuzingatia ni unapoweka malengo zingatia malengo yawe yako wazi, fasaha na yanayoeleweka. Malengo yawe ni sahihi kwao lakini pia yawe yanaweza kupimika. Baada ya kuyafahamu hayo malengo ni vizuri yawekwe katika maadnishi ili kila mmoja aweze kujitoa kikamilifu katika malengo hayo

  1. Weka mambo ya msingi sawa
Ni muhimu sana kuweka misingi kwa kuwaelewesha majukumu yao na wayafahamu kwa undani. Weka kwa ufasaha mategemeo yako kwao lakini pia na wao wajue vipaumbele ni vipi katika majukumu yao. Na uhakikishe wanaweza kujua tofauti kati ya kazi iliyo ya umuhimu sana na ile kazi yenye umuhimu kiasi.

  1. Mfumo wa ufundishaji unaofaa
Kuna hatua tano muhimu zinazoweza kukupatia matokeo mazuri hasa inapohusisha kuwaandaa kiuongozi viongozi chipukizi
                                i.            Kuwa mfano kwanza kwa kila unachotaka waweze kukifanya
                              ii.            Wafundishi au waelekeze
                            iii.            Simamia maendeleo ya kile unachowaelekeza
                            iv.            Wahamasishe
                              v.            Wape fursa pia ya kutengeneza viongozi kati yao viongozi chipukizi

  1. Simamia maendeleo yao bila kuacha
Ni muhimu ukawa na mikutano iliyo rasmi na isiyo rasmi pia ili kuweza kujua mahitaji, matatizo ambayo wanakumbana nayo pia. Na hii itakusaidia kuwapatia vifaa sahihi zaidi na kuendelea kuwapa ujasiri na kuwahamasisha.

Thursday 25 June 2015

Kanuni Sita(6) Muhimu Za Kushinda Tatizo Lolote Unalokutana Nalo.

Matatizo mengi kamwe hayatatuliwi au hayadhibiti kwa ufanisi kutokana na kutoyapa uzito wa kutosheleza. Hakuna tatizo ambalo halina umuhimu kiasi kuwa hatuhitaji kujali kuhusu hilo tatizo. Mfano kwa mwanafunzi inawezekena hapati A au B lakini anafaulu. Kwa mwanafunzi anaweza akalipuuzia kwa kigezo kuwa hajafeli.

Kamwe usilipuuze tatizo wala usipuuze uwezo wako wa kukabiliana na tatizo. Tambua kuwa tatizo unalokutana nalo kuna mamilioni ya watu duniani wameshapitia tatizo kama hilo. Ukiwa na mtazamo chanya kuhusu tatizo utabadili tatizo na litakupatia uzoefu. Na unapokosa mtazamo sahihi kuhusu tatizo unalokumbana nalo itasababisha tatizo husika kuwa kubwa zaidi.

Siri kubwa ambayo imewafanya watu waliofanikiwa kuendelea vizuri ni mtazamo juu ya matatizo wanayokutana nayo. Hapa nakuletea kanuni sita kuhusu matatizo na ambazo ukizifanyia kazi ipasavyo wewe pia utakuwa mshindi kwa kuwa kila unapokutana na tatizo utakuwa sehemu ya utatauzi wa tatizo husika.

1. Kila mtu anayo matatizo
Usifikiri ukishafanikiwa utakuwa ndio umeyaaga matatizo, kadiri unavyofanikiwa ndivyo matatizo unayatengeneza mapya. Mafanikio huwa hayaondoi matatizo bali hutengeneza matatizo mapya. Kwa mfano inawezekana unafikiri ukipata kazi fulani ndo utakuwa umefanikiwa Sana, lakini kumbe unaweza kupata hiyo kazi lakini bosi wako akawa ni mkorofi. Sawa suluhisho unaweza kufikiri ni kujiajiri hapo pia utakutana na matatizo ya kushughulika na wafanyakazi wako ili wazalishe zaidi. Kubaliana na uhalisia kuwa Hakuna mtu ambaye yuko huru hana matatizo bali kutegemeana na shughuli unayojishughulisha nayo basi utakutana na matatizo yanayoendana na shughuli husika


2. Kila tatizo lina ukomo wake
Hakuna tatizo ambalo ni la kudumu yaani litakuwepo milele. Muda wa uhai wa tatizo ukiisha litakufa kwa kuisha/kutokuwepo kabisa na litapita. Kila tatizo huwa lina muda wake ambao kiuhalisia ni mdogo kwa hivyo hakuna haja ya kukwepa au kukimbia tatizo kwa kuwa ukikwepa tatizo sio kuwa unatatua tatizo bali unatengeneza matatizo mapya.

3. Kila tatizo lina fursa
Tatizo linaweza kuwa tatizo kwa mtu mmoja ila kwa mtu mwingine linaweza kuwa fursa. Mfano hospitali zipo kwa sababu watu wanaumwa au wanasheria wapo kwa sababu kuna matatizo ya kisheria. Kwa hiyo kwa mgonjwa ana tatizo la kuumwa lakini mtu mwingine amabaye anafikiria kuhusu kutatua matatizo ya magonjwa mbalimbali atafungua hospitali kutibu magonjwa yanayosumbua jamii na hivyo kumpatia fursa kwa kuwa atalipwa anapotoa huduma hiyo.

4. Kila tatizo litakubadilisha
Hakuna tatizo ambalo litakuja katika maisha yetu na kutuacha kama lilivyotukuta. Tatizo litakufanya uamke au uchangamke na usonge mbele. Na hii ni kwa sababu ya wewe kuwa na uwezo wa kuchagua tatizo husika likkufanyie nini katika ujuzi wako, uzoefu wako, au likufundishe nini ili uweze kuwa na uwezo stahihi wa kutatua tatizo husika

5. Unao uwezo wa kuchagua tatizo likuathiri vipi/kwa kiwango gani
Namna ambavyo unavyolikabili tatizo linavyokutokea inaamua pia athari ya tatizo husika kwako.Inawezekana usiwe na uwezo wa kuchagua tatizo linalokutokea lakini unao uwezo wa kuchagua namna unavyolikabili tatizo.


6. Kuna namna chanya na hasi jinsi ya kukabili kila tatizo
Mara zote chagua namna chanya ya kutatua tatizo kuliko namna hasi ya utatuzi wa tatizo. Jambo la msingi ni kuwa kama huwezi kutatua tatizo basi unahitaji kulisimamia kwa ubunifu. Unapotatua tatizo leo unakuwa ni sehemu ya suluhisho la tatizo na hivyo itakupelekea kufaidika na faida zinazoambayana na kutatua tatizo husika.

Kumbuka utatuzi wa matatizo hufanywa rahisi kama matatizo yatachukuliwa au kutazamwa kama changamoto.

Thursday 7 May 2015

Hii Ndiyo Njia Pekee ya Kutatua Matatizo Yako Yote



Habari za siku ya leo mpenzi msomaji wa blogu hii. Ni matumaini yangu unaendelea vizuri na shughuli zako mbalimbali za kila siku. Siku ya leo napenda kukuletea mada inayohusiana na afya. Tukihusiha binadamu na mada hii , inatusadia kuigawa katika maeneo makuu matatu yaani mwili, akili na roho. Akili na roho vipo ndani ya mwili. Akili na roho ni sehemu ya binadamu ambayo haionekani yaani hauwezi kugusa wakati mwili ni sehemu ya binadamu ambayo inaonekana na unaweza kuigusa mfano vidole katika mkono unaviona na pia unaweza kuvigusa.



Katika makala hii napenda kujikita zaidi katika eneo la afya ya akili kwa kuwa ndilo lenye umuhimu katika kuhakikisha tunaishi maisha yale ambayo tuna shauku ya kuyaishi. Katika akili ya mwanadamu hapo ndipo kuna kiwanda cha kuzalisha mawazo ambayo unaona yamebadilisha namna maisha yetu ya kila siku yanavyokwenda. Uwezo uliopo katika akili ya binadamu ni wa ajabu mno hasa ukiakisi katika kufanya mambo mbalimbali makubwa na ya kushangaza.
Mtoto anapozaliwa kimsingi akili yake inakuwa haijalishwa yaani haijaendelezwa vya kutosha kumuwezesha kufanya mambo mbalimbali. Akili ya mtoto hulishwa kupitia milango ya fahamu ya macho na masikio kwa kufundishwa mambo mbalimbali na mzazi. Katika kipindi hichi cha utoto mambo mengi yanayolishwa katika akili yapo chini ya usimamizi wa mzazi kuamua nini ujifunze na nini usijifunze. Ndiyo kusema hata kwa sehemu wazazi hutusaidia kufikiri pia kwa niaba yetu katika kipindi hiki. Ujumbe mkubwa uliopo katika hatua hii ya kwanza kutoka kwa wazazi ni kuwa wanataka tuwe na mwelekeo mzuri kadiri tunavyokua lakini pia lililo zito zaidi ni kutujengea mtazamo wa kupenda na kuendelea kujifunza katika kipindi chote cha maisha yetu.
 



Pamoja na huo msingi ambao tunakuwa tumewekewa  na ambao unakuwa unatuongoza mpaka hapo tunapofika hatua ya kuweza kujisimamia wenyewe si wengi hupenda kuundeleza huo utaratibu wa kupenda na kuendelea kujifunza kwa kasi na kiwango sawasawa na kile ambacho wazazi wametuwekea ili kuweza kutusaidia kuwa bora siku hadi siku. Wengi huona kama ndiyo wameshafanya mahafali ya kujifunza vitu vyote ambavyo wanatakiwa au wanaweza kujifunza katika muda wao wote wa kuishi hapa ulimwenguni. Na hii kadiri hii  tabia ya kutojifunza inavyoendelea kukua hupelekea kutokuwa na afya ya akili, kutokana na kushindwa kupatia akili chakula ambacho kingeweza kuzalisha mawazo bora ambayo yangesaidia kupata masuluhisho ya changamoto mbalimbali ambzo ulimwengu unazipata kwa sasa.
Kipindi ambacho tabia hii ya kutokujifunza huwa inaanza mara nyingi kwa wale ambao wameajiriwa kwa mara ya kwanza, yaani wamepata ajira baada tu ya kumaliza masomo yao. Asilimia kubwa ya watu baada ya kupata ajira ya kwanza huwa na mgando au mapumziko ambayo hupelekea kabisa kuunda na kuiendeleza hii tabia ya kutopenda kujiendeleza.




Asilimia kubwa ya changamoto ambazo unaona unashindwa kuzitatua leo haziwezi kutatuliwa bila kuwa umeilisha akili yako kwa kiwango cha kutosha ili kuweza kukupatia au kukuzalishia mawazo yanayoweza kuwa suluhisho kwa hizo changamoto. Ni muhimu sana kuwa na usimamizi mzuri wa kuamua mambo gani utakuwa unalisha akili yako kupitia vile unavyoviona na vile unavyovisikia. Chambua video unazoitazama , maandishi ambayo unayasoma , na hata yale mazungumzo unayoyasikiliza kupitia sauti zilizorekodiwa au kusikiliza moja kwa moja, je zina manufaa yoyote au kuna kitu kinarutubisha afya ya akili yako? Au unavifanya kwa sababu ndio utaratibu wa kundi la hao ambao unahusiana nao moja kwa moja wanafanya basi na wewe unafanya. 

Miaka mitano ijayo utakuwa kama ulivyo leo isipokuwa uamue kwa makusudi na kudhamiria kabisa kubadili mambo makuu mawili ; mambo unayoyasoma na watu ambao unakutana nao. Uzuri wa maendeleo ya teknolojia yamerahisisha namna ya upataji wa maarifa mbalimbali mfano blogu hii inakupatia makala mbalimbali ambazo zinalisha akili yako kila siku. Na kuhusu watu unaokutana nao haina maana wale unaokutana nao ana kwa ana hata ila dhana nzima imebebwa katika kusikiliza yale unayoambiwa kwa hivo uwe na uchaguzi mambo gani unayaruhusu yailishe akili yako.