Saturday, 15 October 2016

Uchambuzi wa Kitabu cha " SECRETS OF SELF MADE MILLIONAIRE"

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!

Mwandishi na mjasiriamali Adam Khoo kupitia kitabu hiki cha Secrets of Self Made Millionare, anatushirikisha mbinu mbalimbali ambazo matajiri wengi wametumia kutengeneza vipato visivyo vya kawaida kutoka ngazi ya chini kabisa ya kiuchumi mpaka kufikia kiwango cha uhuru wa kifedha. Kitu ambacho cha kipekee kinachohamasisha ni kuwa walianza bila ya kuwa na fedha, walianza na wazo tuu.



Mambo ambayo nimejifunza katika kitabu hiki
1. Moja ya rasilimali ya pekee na thamani uliyonayo ni akili yako, kuwekeza muda na fedha kwa ajili ya elimu ya fedha ni uwekezaji wa pekee ambao malipo yake yamethibitishwa kuwa na faida zaidi.
2. Mzazi ni vizuri katika hatua ya malezi ya mtoto amjengee njaa ya mafanikio kwa kutompatia kila kitu anachoomba bali amwambie atafute mwenyewe. Lakini pia jukumu kubwa  la mzazi ni kumpatia mtoto upendo, chakula na support ya kielimu.
3. Mambo ambayo unaweza kujifunza ikiwa umeanza kutafuta mwenyewe:
(a) Jinsi ya kupambana na hali ya kuona aibu
(b) Jinsi ya kupambana na hali ya kukataliwa
(c) Jinsi ya kuongea na kutumbuiza hadhira
4. Muundo wa elimu hausadii kukujengea ujuzi wa namna ya kudhibiti fedha na stadi za maisha ambazo zinaweza kukusaidia kukufanya ufanikiwe, badala yake unaelekezwa namna ya kufanya vizuri katika masomo upate kazi nzuri.
5. Ili uweze kuwa na maisha ya mafanikio unahitaji kuwa na mtazamo wa ushindi. Watu wengi wanapenda kuwa na mtazamo wa kulaumu. Mtazamo huu umejikita zaidi katika kutoa sababu kuliko kutafuta utatuzi wa matatizo.
6. Hatua Saba Kuelekea Uhuru wa Kifedha
(a) Kuwa na Mtazamo wa Milionea
Mtazamo huu utakusaidia sana kuyaangalia mambo mbalimbali kwa jicho la tofauti sana. Sehemu ambapo watu wanalalamika kuhusu tatizo wewe utakuwa unaona fursa ya kutengeneza kipato kupitia kutatua tatizo husika. Na mabadiliko haya yatakwenda hadi katika ngazi ya tabia yako, kujifunza kwako, kufikiri kwako.
(b) Weka Kwa Ufasaha Malengo Yako ya Kifedha
Suala la kuwa tajiri halitokei kwa bahati mbaya , ni jambo ambalo linatokea kwa maksudi kabisa kutokana na uamuzi wako wa kuwa tajiri. Ufasaha wa malengo unaonekana katika kiwango sahihi unachokitaka kukipata, kiwango hiki ni lazima kiwe kinaweza kupimika. Malengo yanayowezekana kupimika yanasaidia sana katika upangaji wa mkakati, kuonesha kiwango cha jitihada kinachohitajika kuwekwa.
(c) Tengeneza mpango wa kifedha
Baada ya kukamilisha uwekaji wa malengo, ni muhimu kuwa na mpango wa kukuwezesha kufikia malengo yako. Mpango wako ni lazima uwe na ufasaha kwamba kiasi gani utakitunza, kiasi gani utawekeza, idadi ya mifereji ya kipato utakayoitengeneza, kiwango cha faida unachokitaka kutoka katika uwekezaji unaofanya. Ingawa kuna wataalamu ambao wanaweza kukusaidia kutengeneza mpango huu ila ni muhimu suala hili ukalifanya wewe mwenyewe binafsi.
(d) Ongeza kiasi chako cha kipato
Kikawaida baada ya kuwa na mpango utaona kama itakuchukua muda mrefu mpaka uweze kufikia uhuru wa kifedha. Ukweli ni kuwa unahitaji kuongeza kipato chako sio kwa kiwango cha asilimia bali ni kiwango cha maradufu, mara tatu au zaidi kadiri inavyowezekana. Na hili unaweza kulifanya bila kuacha ajira unayofanya au kuhatarisha kwa kuwekeza fedha zote unazopata kwenda katika biashara.
(e) Dhibiti mapato na matumizi yako
Ni muhimu kuangalia mlinganyo kati ya fedha unazoingiza na fedha unazozitoa. Kuingiza fedha nyingi na kuwa na matumizi ya fedha kidogo ndiyo siri kuu. Unapokuwa na matumizi kidogo inasaidia kubakia na kiasi cha fedha ambacho unaweza kuwekeza na kuhifadhi. Tofauti katika maisha ya tajiri na maskini imejengwa hapa  unafanya nini ni hiki kiasi kinachobaki.
(f) Kuza fedha ziweze kukurudia katika kiwango cha milioni
Baada ya kudhibiti matumizi yako ni vizuri kiasi kile ambacho unabakiza ukiwekeze katika maeneo ambayo faida yake utaipata katika kiwango cha milioni au zaidi. Na siyo unawekeza tuu bila kuzingatia kiwango cha faida unayopata. Hii ni muhimu sababu itafika wakati huwezi kutumia nguvu zako kutengeneza fedha bali fedha uliyonayo iwe inafanya kazi ya kukutengenezea fedha.
(g) Weka ulinzi katika utajiri wako
Utengenezaji utajiri ni suala ambalo utatumia muda na jitihada. Ni muhimu kuhakikisha haupati hasara katika uwekezaji ambao umefanya. Ulinzi unautengeneza kwa kuweka bima , kumpata mtaalamu wa kisheria ambaye anaweza kukushauri mambo ya kisheria kuhusu uwekezaji unaoufanya, na hata wataalamu wa mahesabu ya fedha ili wakuongoze katika eneo hilo bila ya kupata hasara.
7. Tabia za Watu wenye mtazamo wa kuwa milionea
Utajiri wowote huanza kwenye akili kwanza kabla ya kutokea katika uhalisia. Utajiri unapokuwa katika akili unakusaidia kuyatazama mambo mbalimbali katika hali ya fursa ya kuwa milionea zaidi. Na pia inakusaidia hata makosa yakitokea hautakufa kifedha kabisa bali utaweza kuendelea. Hamna utajiri ambao unatengenezwa kwa fedha bali unatengenezwa kutoka katika akili.
(a) Unatakiwa kwa kile unachozalisha uzidi matarajio ya wateja wako. Angalia washindani ambao wapo katika soko moja na wewe wanafanya nini, kisha ongeza thamani kwa kufanya zaidi ya kile kinachotarajiwa na mpokea huduma. Usizalishe sawasawa na matarajio ya mteja au chini ya matarajio ya mteja.
(b) Unatakiwa kuwa na uthubutu wa kuchukua hatua. Usisubiri mpaka mambo yawe yameshakwenda katika hatua nyingine ngumu ndo uchukue hatua au kusubiria hali ya mazingira ifike kiwango fulani ndiyo uchukue hatua. Usiwe mtu wa kulaumu.
(c) Kubali kubeba wajibu wa matokeo yako unayoyapata ili uweze kuwa katika control. Usilaumu wala kulalamika kwa nini jambo fulani halijawa vile umetarajia , kwa sababu itakufanya kutokuwa katika control ya kukufanya wewe ufanikiwe bali vitu vingine tofauti na wewe ndiyo vinakuwa katika control.
(d) Unahitaji kuwa na hali ya uvumilivu na kukubali kuchelewa kukumbuka kutumia fedha zako kwa ajili ya anasa au vitu ambavyo sio vya kuwekeza kukuongezea ujuzi na maarifa. Unahitaji kuwa na kusita kutumia fedha kwa ajili ya starehe au vitu ambavyo vinashuka thamani.
(e) Hakuna eneo fulani maalum ambalo ukifanya biashara ndiyo litakupa faida tuu katika vipindi vyote. Eneo ambalo ni sahihi kwa ajili ya mtu yoyote kufanya biashara ni lile ambalo analipenda sana. Sababu hili ni eneo ambalo wakati unajenga biashara yako hutaona kama unafanya kazi bali itakuwa ni sehemu ya kufurahia, lakini pia itakusaidia kukupa hamasa na msukumo wa kuendelea bila kuchoka.
(f) Unahitaji kuwa mwaminifu katika eneo la biashara unayofanya. Uaminifu uanze katika ngazi ya wateja, wafanyakazi wenzako na hata jamii. Uaminifu ni sawa na uwekezaji ambao unaendelea kujilimbikiza. Na hii ni nguzo muhimu ambayo itakusaidia wateja na kila mtu unayeshirikiana nae katika biashara kukuamini.
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako.

Friday, 14 October 2016

Hatua Saba (07) za Kukusaidia Kuelekea Uhuru wa Kifedha

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!

Rafiki kila mtu anapenda kuishi katika hali ya kuwa na kiwango cha fedha kinachoweza kuhudumia mahitaji yale ya muhimu na kufanya mambo mengine ya ziada. Asilimia kubwa ya watu wanatumia muda na nguvu ili kupata kipato kinachowasaidia kujikimu. Hivyo utakubaliana na mimi hawana uhuru katika maisha yao maana kuna muda fulani maalum lazima awepo kwa mwajiri wake,wanabadilishana muda na ujuzi wake kwa fedha (mshahara). Hapa chini nakushirikisha hatua chache ambazo ukizifanyia kazi zitakusaidia kufikia uhuru wa kifedha.




(a) Kuwa na mtazamo wa kimilionea
Mtazamo huu utakusaidia sana kuyaangalia mambo mbalimbali kwa jicho la tofauti sana. Sehemu ambapo watu wanalalamika kuhusu tatizo wewe utakuwa unaona fursa ya kutengeneza kipato kupitia kutatua tatizo husika. Na mabadiliko haya yatakwenda hadi katika ngazi ya tabia yako, kujifunza kwako, kufikiri kwako. Utakuwa ni mtu ambaye anatatua matatizo na kulipwa kutokana na kuleta suluhisho la tatizo.
(b) Weka kwa ufasaha malengo yako ya kifedha
Suala la kuwa tajiri halitokei kwa bahati mbaya , ni jambo ambalo linatokea kwa maksudi kabisa kutokana na uamuzi wako wa kuwa tajiri. Ufasaha wa malengo unaonekana katika kiwango sahihi unachokitaka kukipata, kiwango hiki ni lazima kiwe kinaweza kupimika. Malengo yanayowezekana kupimika yanasaidia sana katika upangaji wa mkakati, kuonesha kiwango cha jitihada kinachohitajika kuwekwa na pia kukupatia hamasa inayoweza kukupa stamina ya kuweza kupambana hata mambo yanapokuwa magumu.
(c) Tengeneza mpango wa kifedha
Baada ya kukamilisha uwekaji wa malengo, ni muhimu kuwa na mpango wa kukuwezesha kufikia malengo yako. Mpango wako ni lazima uwe na ufasaha ukiwa na maelezo yanayogusa masuala kama vile; kiasi gani utakitunza, kiasi gani utawekeza, idadi ya mifereji ya kipato utakayoitengeneza, kiwango cha faida unachokitaka kutoka katika uwekezaji unaofanya. Ingawa kuna wataalamu ambao wanaweza kukusaidia kutengeneza mpango huu ila ni muhimu suala hili ukalifanya wewe mwenyewe binafsi, hii ni kwa sababu wewe ndiye unayefahamu kwa ufasaha unachokitaka.
(d) Ongeza kiasi chako cha kipato
Kikawaida baada ya kuwa na mpango utaona kama itakuchukua muda mrefu mpaka uweze kufikia uhuru wa kifedha hasa ukifanya ulinganisho na hali yako ya kifedha ya sasa. Ukweli ni kuwa unahitaji kuongeza kipato chako sio kwa kiwango cha asilimia bali ni kiwango cha maradufu, mara tatu au mara nyingi zaidi kadiri inavyowezekana. Ukomo wa kiasi gani ni mara ngapi unaweza kuongeza kipato chako unaamuliwa na uwezo wako hakuna mtu anayeweza kujizuia. Na hili unaweza kulifanya bila kuacha ajira unayofanya au kuhatarisha kwa kuwekeza fedha zote unazopata kwenda katika biashara.
(e) Dhibiti mapato na matumizi yako
Ni muhimu kuangalia mlinganyo kati ya fedha unazoingiza na fedha unazozitoa. Kuingiza fedha nyingi na kuwa na matumizi ya fedha kidogo ndiyo siri kuu. Unapokuwa na matumizi kidogo inasaidia kubakia na kiasi cha fedha ambacho unaweza kuwekeza na kuhifadhi. Tofauti katika maisha ya tajiri na maskini imejengwa hapa  unafanya nini na hiki kiasi kinachobaki.
(f) Kuza fedha ziweze kukurudia katika kiwango cha milioni au zaidi
Baada ya kudhibiti matumizi yako ni vizuri kiasi kile ambacho unabakiza ukiwekeze katika maeneo ambayo faida yake utaipata katika kiwango cha milioni au zaidi. Na siyo unawekeza tuu bila kuzingatia kiwango cha faida unayopata. Hii ni muhimu sababu itafika wakati huwezi kutumia nguvu zako kutengeneza fedha bali fedha uliyonayo iwe inafanya kazi ya kukutengenezea fedha.
(g) Weka ulinzi katika utajiri wako
Utengenezaji utajiri ni suala ambalo utatumia muda na jitihada. Ni muhimu kuhakikisha haupati hasara katika uwekezaji ambao umefanya. Ulinzi unautengeneza kwa kuweka bima , kumpata mtaalamu wa kisheria ambaye anaweza kukushauri mambo ya kisheria kuhusu uwekezaji unaoufanya, na hata wataalamu wa mahesabu ya fedha ili wakuongoze katika eneo hilo bila ya kupata hasara.
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako.

Thursday, 13 October 2016

Jinsi ya Kukabili Changamoto za Uandishi Katika Blogu

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!
Pasipo kutegemea lugha gani unaitumia katika uandishi wa makala ambazo unaziweka katika blogu yako, bado suala la uandishi lina changamoto. Changamoto kubwa inatokea wakati unaoanisha kati ya ujumbe ambao umelenga kufikisha kwa hadhira na yale maneno uliyoyaandika katika makala yako unayokusudia hadhira yako iyasome.
Ikiwa maneno unayoyaandika yatashindwa kufikisha ujumbe kikamilifu sawasawa na vile ambavyo wazo lilipokuja kwako mwanzo, itasababisha tafsiri mbalimbali kwa msomaji. Baadhi ya tafsiri ni msomaji kukataa makala yako kutokana na makosa yanayoonesha kukosekana kwa mtiririko wa kumuwezesha msomaji kukufuatilia kupokea kusudi la makala husika, tafsiri nyingine ni kumfanya msomaji kuona mwandishi amekosa umakini wa kuzingatia mambo madogo ambayo ni ya msingi kabisa (basic).



Katika makala hii ninapenda kukukumbusha mambo ambayo ukiyafanyia kazi kwa umakini yatachangia kuboresha kazi yako kutoka hatua iliyopo sasa kwenda hatua nyingine nzuri zaidi.
(a) Jambo la kwanza ni kusoma vitabu, makala au machapisho zaidi yanayohusiana na eneo ulilochagua kuandika. Maneno unayoyaandika ni matokeo (output) yanayopatikana kutokana na kuweza kuingiza maneno mengi mapya katika kiwanda chako (akili au mind). Maneno haya unayapata baada ya kusoma kwa wingi makala, vitabu au machapisho mbalimbali. Na si kupata maneno mapya pekee bali itakusaidia kuona waandishi wengine wameandika nini , namna yao ya uandishi, na kugundua pengo lilipo  ili uweze kuliziba kupitia makala yako utakayoandika.
(b) Jambo la pili ni kujenga tabia ya kuandika kila siku.  Uandishi ni fani au ujuzi ambao unahitaji kujengwa. Kama ilivyo aina nyingine za ujuzi hatua ya kwanza inakuwa ni kujifunza kwa nadharia na hatua ya pili inakuwa ni kufanya kwa vitendo yale uliyojifunza. Kwa kadiri ya wingi wa mazoezi unayoyafanya inachangia sana kugundua na kusahihisha makosa ambayo unayafanya. Kuandika makala ndefu yenye maneno mfano elfu moja au zaidi kwa siku moja katika wiki hakusaidii kuboresha ujuzi wako katika uandishi ukilinganisha na mtu anayeandika maneno mia mbili kila siku mfululizo bila kuwa na pengo kati ya siku na siku. Kuna maneno ya kiingereza yanasema "Practise Makes Perfect". Maneno haya yanaashiria kadiri unavyofanya mazoezi ya kuandika ni sawasawa na kuzidi kujinoa katika uandishi na hii itapelekea kuwepo kwa thamani katika makala zako kunakosababishwa na umakini ulioujenga.
(c) Jambo la tatu rafiki yangu fanya tathmini ya makala uliyoandika kabla hujaruhusu wasomaji kuiona na baada ya wasomaji. Ninaelewa ni jinsi gani inachosha kurudia kazi ambayo umetumia kiasi cha saa moja au zaidi kuandika. Na hii inaweza kuleta hali ya kuona uvivu wa kupitia kuangalia kama kuna kosa au kupoteza maana kutokana na maboresho uliyoyafanya.
Rafiki kama unataka kuona uandishi wako unakuwa basi ni muhimu kwanza wewe binafsi ukubali kupitia kazi yako na kukosoa makosa madogo madogo, pili ukubali kumpa mtu ambaye atasoma makala yako na aweze kukusaidia kuboresha na mwisho kuwa unapitia mara kwa mara kazi zako ili kuendelea kuzihuisha kadiri ujuzi wako wa uandishi unavyokua.
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako.

Wednesday, 12 October 2016

Uhusiano Uliopo Kati ya Malengo, Uwezo na Ukuaji Wako

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!

Rafiki kuna kipindi unaweka malengo na unakuta kadiri muda unavyokwenda unaanza kupata mashaka kama unaweza kuyatimiza au kuyaleta katika uhalisia. Ikiwa utajishawishi na kuikubali hii hali kuendelea itakufanya ushindwe kutimiza malengo yako kutokana na kupoteza morali. Morali huwa inasaidia sana kusukuma mambo yaweze kutokea. Bila kujali umefikaje katika hali hiyo ya kupata mashaka ninapenda utambue kuwa unao uwezo wa kuyafikia malengo yako makuu katika maisha.

Kuna njia mbalimbali za kukusaidia kujitambua una uwezo kiasi gani wa kufanya vitu vinavyoweza kuacha alama katika dunia. Katika makala hii ninapenda kukushirikisha njia mbili.

(a) Njia ya kwanza ni kufanya tathmini binafsi kufahamu mambo gani unaweza kuyafanya vizuri sana (strength) na mambo gani uko dhaifu yaani huwezi kuyafanya vizuri (weakness). Tathmini hii unaweza kuifanya kwa namna ya kujiuliza maswali. Hapa unaandaa orodha ya maswali pamoja na majibu ambayo itakuwa inakugusa wewe binafsi.

(b) Njia ya pili ni kuwashirikisha watu wako wa karibu kama marafiki , ndugu na kadhalika ambao wanaweza kukueleza ukweli bila kukuficha au kuona aibu kuhusu mambo yale unayoweza kufanya vizuri (strength) na mambo yale ambayo huwezi kuyafanya vizuri (weakness).

Baada ya kukamilisha hatua hiyo ya kwanza itakusaidia katika kuweza kuyafikia malengo yako makuu katika maisha. Tathmini hii itachangia sana kuoanisha uhusiano wa ukubwa wa malengo yako uliyoyaweka na kiwango halisia cha rasilimali uwezo wako unaohitajika kukuwezesha utimize malengo yako. Jambo la kulizingatia  rafiki usiweke malengo ambayo yanaendana sawasawa na kiwango cha uwezo ulionao wakati au pindi unaweka malengo. Hii ni muhimu kwa sababu unahitaji fursa ya kukua (growth) unapokuwa katika safari ya kutimiza malengo yako.

Siri kubwa ambayo rafiki napenda kukuambia ni kuwa kila palipo na fursa ya kukua (growth) kuna faida kadhaa ambazo huambatana nazo, baadhi ya hizo faida ni:
(a) Kupata nafasi ya kujifunza mambo mapya na kupelekea kutengeza maarifa ambayo yanaweza kutumika kama mwongozo wa kuwasaidia wengine katika eneo husika.
(b) Kufanya mambo mapya tofauti na yale ambayo umekuwa ukiyafanya mara kwa mara na kukusaidia kupata matokeo tofauti.
(c) Kukujengea stamina itakayokusaidia kuhimili kuendelea kuweka jitihada kuelekea kuyatimiza malengo yako.
(d) Kutokukata tamaa kunakosababishwa na na dalili za awali za kushindwa kunakotokea kiasili kwa jambo lolote unalofanya linapokuwa katika hatua ya uchanga.

Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako.

Tuesday, 11 October 2016

Maana za Vibao Vya Namba Za Magari (Plate Number)

Habari rafiki!
Katika kila gari kuna sehemu mbili ambapo huwekwa vibao vyenye namba kwa ajili ya kulitambulisha gari husika. Vibao hivi huwekwa mbele na nyuma ya gari. Katika lugha ya kiingereza huitwa "plate number". Katika makala ya leo ninakushirikisha namna ya kupata ujumbe unaowasilishwa na pindi unaposoma kibao husika cha namba ya gari.


Aina za Vibao vya Namba za Magari
1. Kibao chenye rangi ya njano na namba inayoanza na herufi T
Kibao hiki kinabeba maana kuwa gari husika limesajiliwa kutumika kwa ajili ya shughuli binafsi. Kwa kiingereza inasemwa "private use". Magari yenye vibao hivi hayaruhusiwi kutumika kwa ajili ya biashara.
2. Kibao chenye rangi nyeupe na namba inayoanza na herufi T
Kibao hiki kinabeba maana kuwa gari husika limesajiliwa kwa ajili ya matumizi ya biashara. Kwa kiingereza inasemwa "commercial use". Mfano mzuri daladala au basi za kubeba abiria na taxi.
3. Kibao chenye rangi ya njano na namba haianzi na herufi T
Kibao hiki kinabeba maana kuwa gari husika linamilikiwa na taasisi ya umma au serikali. Hapa kuna makundi yafuatayo:
(a) SU - shirika la umma , mfano vyuo vikuu vya serikali
(b) SM - Serikali za Mitaa , mfano ni halmashauri
(c) STK,STL,STJ - serikali, mfano ni wizara
4. Kibao chenye rangi nyekundu na namba inayoanza na herufi DFP au DFPA
Kibao hiki kinabeba maana kuwa gari husika limetolewa kwa ajili ya matumizi ya miradi inayofadhiliwa na wafadhili kutoka nje ya nchi.
5. Kibao chenye rangi ya bluu na namba inayoanza na herufi T kufuatiwa na namba na kisha herufi CD
Kibao hiki kinabeba maana kuwa gari husika linamilikiwa na moja ya shirika la umoja wa mataifa. Mfano shirika la Afya Duniani (WHO).
6. Kibao chenye rangi ya kijani na namba inayoanza na herufi T kufuatiwa na namba na kisha herufi CD
Kibao hiki kinabeba maana kuwa gari husika linamilikiwa na ofisi za ubalozi wa nchi fulani. Mfano ubalozi wa Ufaransa.
7. Kibao chenye rangi nyeusi na namba zimeandiwa kwa rangi ya njano
Kibao hiki kinabeba maana kuwa gari husika linamilikiwa na Jeshi la  Polisi. Namba hizi huwa na herufi PT
8. Kibao chenye rangi nyeusi na namba zimeandiwa kwa rangi ya njano
Kibao hiki kinabeba maana kuwa gari husika linamilikiwa na Jeshi la Wananchi (JW). Namba hizi huwa na herufi JW.
9. Kibao chenye rangi ya kijani na namba zenye herufi MT
Kibao hiki kinabeba maana kuwa gari husika linamilikiwa na Jeshi la Magereza.
Unaweza kubofya hapa ili kuweka barua pepe yako au rafiki yako ambaye unapenda makala hizi azipate moja kwa moja katika barua pepe.

Monday, 10 October 2016

Uandishi Sahihi wa Siku na Mwezi Katika Mwaka

Habari rafiki mfuatiliaji wa makala mbalimbali katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!


Muda unaweza kuoneshwa kwa vipimo mbalimbali. Kipimo kidogo  cha muda ni sekunde. Sekunde zikikusanyika na kufika idadi ya sitini  (60) tunapata dakika moja (01). Dakika zikikusanyika na kufikia idadi ya sitini (60) tunapata saa moja(01). Saa zikikusanyika na kufika idadi ya ishirini na nne (24) tunapata siku moja (01). Siku zikikusanyika na kufikia idadi ya saba (07) tunapata wiki moja (01). Wiki zikikusanyika na kufika idadi ya nne (04) tunapata mwezi mmoja  (01). Miezi nayo ikikusanyika na kufika idadi ya kumi na mbili (12) tunapata mwaka mmoja (01).
Katika makala hii nimeigawa katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza nitaeleza namna sahihi ya kuandika siku wakati sehemu ya pili nitaeleza namna sahihi ya kuandika mwezi. Katika sehemu zote mbili nitaonesha namna ya kuandika kwa maneno kamili na namna ya kuandika kwa ufupisho.


Uandishi wa Siku
Kama nilivyoeleza hapo juu kuna idadi ya siku saba. Katika siku hizi saba ,kuna siku tano ambazo ni kwa ajili ya kufanya kazi na kuna siku mbili kwa ajili ya kupumzika. Siku hizi mbili hufahamika kwa jina la wikiendi. Kuna uwezekano pia kutegemeana na majira katika wiki kuwa na siku zenye shughuli maalum, shughuli hizi zinaweza kuwa za kidini, kitaifa na kadhalika. Siku hizi zenye shughuli maalum zinaitwa sikukuu ambapo zinategemea sana tarehe katika kalenda. Siku za wikiendi na sikukuu zinatumika zaidi kwa ajili ya mapumziko.




(a) Uandishi wa siku kwa maneno kamili
Siku za Wikiendi
Majina ya siku hizi katika lugha ya kiswahili ni  Jumamosi na Jumapili. Majina ya siku hizi katika lugha ya kiingereza ni Saturday na Sunday.

Siku za Kazi
Majina ya siku hizi ni Jumatatu, Jumanne, Jumatano, Alhamisi na Ijumaa. Majina ya siku hizi katika lugha ya kiingereza ni Monday, Tuesday, Wednesday, Thursday, Friday.


(b) Uandishi wa siku kwa ufupisho
Siku za Wikiendi
Katika lugha ya kiingereza hutumika herufi tatu za kwanza yaani Sat na Sun. Katika lugha ya kiswahili yamekuwa yakitumika maneno Jmosi na Jpili au J1 na J2 lakini namna sahihi ya kuandika hizi siku kwa ufupisho ni Jumamosi na Jumapili.

Siku za Kazi
Katika lugha ya kiingereza hutumika herufi tatu za kwanza yaani Mon, Tue, Wed, Thu na Fri. Katika lugha ya kiswahili yamekuwa yakitumika maneno Jtatu, Jnne,Jtano, Al, Iju au J3,J4,J5 lakini namna sahihi ya kuandika hizi siku kwa ufupisho ni Jumatatu, Jumanne, Jumatano, Alhamisi na Ijumaa.


Uandishi wa Mwezi
Idadi ya miezi ikifika kumi na mbili huitwa mwaka. Mwezi unaweza kuwa na idadi ya siku thelathini au thelathini na moja isipokuwa mwezi februari ambao unaweza kuwa na siku ishirini na nane au ishirini na tisa. Idadi ya miezi ikiwa ni mitatu huitwa robo mwaka. Kwa kuwa kuna miezi kumi na mbili hivyo katika mwaka ukiugawa katika miezi mitatu utapata robo nne. Idadi ya miezi ikiwa ni sita huitwa mwaka. Kwa kuwa kuna miezi kumi na mbili hivyo ukigawa katika miezi sita utapata nusu mbili.



(a) Uandishi wa mwezi kwa maneno kamili
Majina ya miezi katika lugha ya kiswahili ni Januari, Februari, Machi, Aprili, Mei, Juni, Julai, Agosti, Septemba, Oktoba,Novemba na Disemba.
Majina ya miezi katika lugha ya kiingereza ni January, February, March, April, May,June, July, August, September, October,November na December.


(b) Uandishi wa Mwezi kwa ufupisho
Katika lugha ya kiingereza hutumia herufi tatu za kwanza yaani Jan, Feb, Mar, Apr, May, Jun, Jul, Aug, Sep, Oct, Nov na Dec. Katika lugha ya kiswahili kwa ufupisho inafanana na hapo juu kipengele (a).


Unaweza kubofya hapa ili kuweka barua pepe yako au rafiki yako ambaye unapenda makala hizi azipate moja kwa moja katika barua pepe.

Sunday, 9 October 2016

Faida Nne (04) Unazopata Ukiwa na Akaunti ya Gmail.

Habari rafiki yangu unayefuatilia makala zinazowekwa katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!
Leo napenda kukuletea mambo manne (04) ambayo unaweza kuyafanya kwa kuwa na akaunti ya barua pepe kutoka kampuni ya Google. Akaunti hii hufahamika kwa jina la Gmail.

1. Nafasi ya ukubwa wa kiasi cha Gigabyte 15 kwa ajili ya kuhifadhi taarifa zako mtandaoni
Kila mtu ambaye ana akaunti ya Gmail anapata sehemu ya kuhifadhi "data" yenye ukubwa wa kiasi cha Gigabyte 15. Hii nafasi inapatikana bure bila malipo yoyote. Na unaweza kuzitumia taarifa zako sehemu yoyote duniani ambapo umeunganishwa na mtandao.

2. Kuhifadhi orodha ya majina kutoka katika kumbukumbu ya simu yako
Kila mtu ambaye ana akaunti ya Gmail anapata nafasi ya kuhifadhi majina, namba za simu kutoka katika kumbukumbu ya mawasiliano ya simu husika. Hii huduma pia inapatikana bila ya malipo yoyote. Ni huduma ambayo huwa inasaidia sana wakati aidha unapotaka kubadili simu yako ama simu inapokuwa imeharibika ama simu imepotea. Ikiwa umehifadhi orodha yako katika Gmail utaweza kurejesha orodha ya majina na namba za simu kwa haraka na urahisi.

3. Kuwa na blogu katika mtandao wa blogspot.com
Kila mtu ambaye ana akaunti ya Gmail anaweza kufungua blogu ambapo ataweza kuweka taarifa au maarifa mbalimbali kwenda kwa jamii husika. Blogu hii ataifungua bila ya malipo yoyote. Jina lake la blogu atalipendekeza kutegemeana na anavyoona inafaa na baada ya jina hilo ambalo amependekeza litafuata neno .blogspot.com

4. Kuweka programu mbalimbali katika simu zinazotumia Google Android OS
Programu mbalimbali ambazo zinatumika katika smartphone unaweza kuzipata kutoka katika Play Store. Ili uweze kuziona na kuchagua programu hizi kutoka play store unahitaji kuwa na akaunti ya Gmail. Mfano tunapowapelekea mafundi wa simu watuwekee programu kama vile WhatsApp, You tube, Facebook na kadhalika, wanachofanya hasa ni kutumia akaunti ya Gmail kuingia playstore, kutafuta programu ulizomwambia na kuziweka, ambapo ni kitendo ungeweza pia kukifanya ikiwa unayo akaunti ya Gmail.
Endelea kutembelea mtandao huu kujifunza zaidi.