Saturday, 15 October 2016

Uchambuzi wa Kitabu cha " SECRETS OF SELF MADE MILLIONAIRE"

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!

Mwandishi na mjasiriamali Adam Khoo kupitia kitabu hiki cha Secrets of Self Made Millionare, anatushirikisha mbinu mbalimbali ambazo matajiri wengi wametumia kutengeneza vipato visivyo vya kawaida kutoka ngazi ya chini kabisa ya kiuchumi mpaka kufikia kiwango cha uhuru wa kifedha. Kitu ambacho cha kipekee kinachohamasisha ni kuwa walianza bila ya kuwa na fedha, walianza na wazo tuu.



Mambo ambayo nimejifunza katika kitabu hiki
1. Moja ya rasilimali ya pekee na thamani uliyonayo ni akili yako, kuwekeza muda na fedha kwa ajili ya elimu ya fedha ni uwekezaji wa pekee ambao malipo yake yamethibitishwa kuwa na faida zaidi.
2. Mzazi ni vizuri katika hatua ya malezi ya mtoto amjengee njaa ya mafanikio kwa kutompatia kila kitu anachoomba bali amwambie atafute mwenyewe. Lakini pia jukumu kubwa  la mzazi ni kumpatia mtoto upendo, chakula na support ya kielimu.
3. Mambo ambayo unaweza kujifunza ikiwa umeanza kutafuta mwenyewe:
(a) Jinsi ya kupambana na hali ya kuona aibu
(b) Jinsi ya kupambana na hali ya kukataliwa
(c) Jinsi ya kuongea na kutumbuiza hadhira
4. Muundo wa elimu hausadii kukujengea ujuzi wa namna ya kudhibiti fedha na stadi za maisha ambazo zinaweza kukusaidia kukufanya ufanikiwe, badala yake unaelekezwa namna ya kufanya vizuri katika masomo upate kazi nzuri.
5. Ili uweze kuwa na maisha ya mafanikio unahitaji kuwa na mtazamo wa ushindi. Watu wengi wanapenda kuwa na mtazamo wa kulaumu. Mtazamo huu umejikita zaidi katika kutoa sababu kuliko kutafuta utatuzi wa matatizo.
6. Hatua Saba Kuelekea Uhuru wa Kifedha
(a) Kuwa na Mtazamo wa Milionea
Mtazamo huu utakusaidia sana kuyaangalia mambo mbalimbali kwa jicho la tofauti sana. Sehemu ambapo watu wanalalamika kuhusu tatizo wewe utakuwa unaona fursa ya kutengeneza kipato kupitia kutatua tatizo husika. Na mabadiliko haya yatakwenda hadi katika ngazi ya tabia yako, kujifunza kwako, kufikiri kwako.
(b) Weka Kwa Ufasaha Malengo Yako ya Kifedha
Suala la kuwa tajiri halitokei kwa bahati mbaya , ni jambo ambalo linatokea kwa maksudi kabisa kutokana na uamuzi wako wa kuwa tajiri. Ufasaha wa malengo unaonekana katika kiwango sahihi unachokitaka kukipata, kiwango hiki ni lazima kiwe kinaweza kupimika. Malengo yanayowezekana kupimika yanasaidia sana katika upangaji wa mkakati, kuonesha kiwango cha jitihada kinachohitajika kuwekwa.
(c) Tengeneza mpango wa kifedha
Baada ya kukamilisha uwekaji wa malengo, ni muhimu kuwa na mpango wa kukuwezesha kufikia malengo yako. Mpango wako ni lazima uwe na ufasaha kwamba kiasi gani utakitunza, kiasi gani utawekeza, idadi ya mifereji ya kipato utakayoitengeneza, kiwango cha faida unachokitaka kutoka katika uwekezaji unaofanya. Ingawa kuna wataalamu ambao wanaweza kukusaidia kutengeneza mpango huu ila ni muhimu suala hili ukalifanya wewe mwenyewe binafsi.
(d) Ongeza kiasi chako cha kipato
Kikawaida baada ya kuwa na mpango utaona kama itakuchukua muda mrefu mpaka uweze kufikia uhuru wa kifedha. Ukweli ni kuwa unahitaji kuongeza kipato chako sio kwa kiwango cha asilimia bali ni kiwango cha maradufu, mara tatu au zaidi kadiri inavyowezekana. Na hili unaweza kulifanya bila kuacha ajira unayofanya au kuhatarisha kwa kuwekeza fedha zote unazopata kwenda katika biashara.
(e) Dhibiti mapato na matumizi yako
Ni muhimu kuangalia mlinganyo kati ya fedha unazoingiza na fedha unazozitoa. Kuingiza fedha nyingi na kuwa na matumizi ya fedha kidogo ndiyo siri kuu. Unapokuwa na matumizi kidogo inasaidia kubakia na kiasi cha fedha ambacho unaweza kuwekeza na kuhifadhi. Tofauti katika maisha ya tajiri na maskini imejengwa hapa  unafanya nini ni hiki kiasi kinachobaki.
(f) Kuza fedha ziweze kukurudia katika kiwango cha milioni
Baada ya kudhibiti matumizi yako ni vizuri kiasi kile ambacho unabakiza ukiwekeze katika maeneo ambayo faida yake utaipata katika kiwango cha milioni au zaidi. Na siyo unawekeza tuu bila kuzingatia kiwango cha faida unayopata. Hii ni muhimu sababu itafika wakati huwezi kutumia nguvu zako kutengeneza fedha bali fedha uliyonayo iwe inafanya kazi ya kukutengenezea fedha.
(g) Weka ulinzi katika utajiri wako
Utengenezaji utajiri ni suala ambalo utatumia muda na jitihada. Ni muhimu kuhakikisha haupati hasara katika uwekezaji ambao umefanya. Ulinzi unautengeneza kwa kuweka bima , kumpata mtaalamu wa kisheria ambaye anaweza kukushauri mambo ya kisheria kuhusu uwekezaji unaoufanya, na hata wataalamu wa mahesabu ya fedha ili wakuongoze katika eneo hilo bila ya kupata hasara.
7. Tabia za Watu wenye mtazamo wa kuwa milionea
Utajiri wowote huanza kwenye akili kwanza kabla ya kutokea katika uhalisia. Utajiri unapokuwa katika akili unakusaidia kuyatazama mambo mbalimbali katika hali ya fursa ya kuwa milionea zaidi. Na pia inakusaidia hata makosa yakitokea hautakufa kifedha kabisa bali utaweza kuendelea. Hamna utajiri ambao unatengenezwa kwa fedha bali unatengenezwa kutoka katika akili.
(a) Unatakiwa kwa kile unachozalisha uzidi matarajio ya wateja wako. Angalia washindani ambao wapo katika soko moja na wewe wanafanya nini, kisha ongeza thamani kwa kufanya zaidi ya kile kinachotarajiwa na mpokea huduma. Usizalishe sawasawa na matarajio ya mteja au chini ya matarajio ya mteja.
(b) Unatakiwa kuwa na uthubutu wa kuchukua hatua. Usisubiri mpaka mambo yawe yameshakwenda katika hatua nyingine ngumu ndo uchukue hatua au kusubiria hali ya mazingira ifike kiwango fulani ndiyo uchukue hatua. Usiwe mtu wa kulaumu.
(c) Kubali kubeba wajibu wa matokeo yako unayoyapata ili uweze kuwa katika control. Usilaumu wala kulalamika kwa nini jambo fulani halijawa vile umetarajia , kwa sababu itakufanya kutokuwa katika control ya kukufanya wewe ufanikiwe bali vitu vingine tofauti na wewe ndiyo vinakuwa katika control.
(d) Unahitaji kuwa na hali ya uvumilivu na kukubali kuchelewa kukumbuka kutumia fedha zako kwa ajili ya anasa au vitu ambavyo sio vya kuwekeza kukuongezea ujuzi na maarifa. Unahitaji kuwa na kusita kutumia fedha kwa ajili ya starehe au vitu ambavyo vinashuka thamani.
(e) Hakuna eneo fulani maalum ambalo ukifanya biashara ndiyo litakupa faida tuu katika vipindi vyote. Eneo ambalo ni sahihi kwa ajili ya mtu yoyote kufanya biashara ni lile ambalo analipenda sana. Sababu hili ni eneo ambalo wakati unajenga biashara yako hutaona kama unafanya kazi bali itakuwa ni sehemu ya kufurahia, lakini pia itakusaidia kukupa hamasa na msukumo wa kuendelea bila kuchoka.
(f) Unahitaji kuwa mwaminifu katika eneo la biashara unayofanya. Uaminifu uanze katika ngazi ya wateja, wafanyakazi wenzako na hata jamii. Uaminifu ni sawa na uwekezaji ambao unaendelea kujilimbikiza. Na hii ni nguzo muhimu ambayo itakusaidia wateja na kila mtu unayeshirikiana nae katika biashara kukuamini.
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako.

0 comments:

Post a Comment