Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!
Rafiki kuna kipindi unaweka malengo na unakuta kadiri muda unavyokwenda unaanza kupata mashaka kama unaweza kuyatimiza au kuyaleta katika uhalisia. Ikiwa utajishawishi na kuikubali hii hali kuendelea itakufanya ushindwe kutimiza malengo yako kutokana na kupoteza morali. Morali huwa inasaidia sana kusukuma mambo yaweze kutokea. Bila kujali umefikaje katika hali hiyo ya kupata mashaka ninapenda utambue kuwa unao uwezo wa kuyafikia malengo yako makuu katika maisha.
Kuna njia mbalimbali za kukusaidia kujitambua una uwezo kiasi gani wa kufanya vitu vinavyoweza kuacha alama katika dunia. Katika makala hii ninapenda kukushirikisha njia mbili.
(a) Njia ya kwanza ni kufanya tathmini binafsi kufahamu mambo gani unaweza kuyafanya vizuri sana (strength) na mambo gani uko dhaifu yaani huwezi kuyafanya vizuri (weakness). Tathmini hii unaweza kuifanya kwa namna ya kujiuliza maswali. Hapa unaandaa orodha ya maswali pamoja na majibu ambayo itakuwa inakugusa wewe binafsi.
(b) Njia ya pili ni kuwashirikisha watu wako wa karibu kama marafiki , ndugu na kadhalika ambao wanaweza kukueleza ukweli bila kukuficha au kuona aibu kuhusu mambo yale unayoweza kufanya vizuri (strength) na mambo yale ambayo huwezi kuyafanya vizuri (weakness).
Baada ya kukamilisha hatua hiyo ya kwanza itakusaidia katika kuweza kuyafikia malengo yako makuu katika maisha. Tathmini hii itachangia sana kuoanisha uhusiano wa ukubwa wa malengo yako uliyoyaweka na kiwango halisia cha rasilimali uwezo wako unaohitajika kukuwezesha utimize malengo yako. Jambo la kulizingatia rafiki usiweke malengo ambayo yanaendana sawasawa na kiwango cha uwezo ulionao wakati au pindi unaweka malengo. Hii ni muhimu kwa sababu unahitaji fursa ya kukua (growth) unapokuwa katika safari ya kutimiza malengo yako.
Siri kubwa ambayo rafiki napenda kukuambia ni kuwa kila palipo na fursa ya kukua (growth) kuna faida kadhaa ambazo huambatana nazo, baadhi ya hizo faida ni:
(a) Kupata nafasi ya kujifunza mambo mapya na kupelekea kutengeza maarifa ambayo yanaweza kutumika kama mwongozo wa kuwasaidia wengine katika eneo husika.
(b) Kufanya mambo mapya tofauti na yale ambayo umekuwa ukiyafanya mara kwa mara na kukusaidia kupata matokeo tofauti.
(c) Kukujengea stamina itakayokusaidia kuhimili kuendelea kuweka jitihada kuelekea kuyatimiza malengo yako.
(d) Kutokukata tamaa kunakosababishwa na na dalili za awali za kushindwa kunakotokea kiasili kwa jambo lolote unalofanya linapokuwa katika hatua ya uchanga.
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako.
0 comments:
Post a Comment