Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!
Pasipo kutegemea lugha gani unaitumia katika uandishi wa makala ambazo unaziweka katika blogu yako, bado suala la uandishi lina changamoto. Changamoto kubwa inatokea wakati unaoanisha kati ya ujumbe ambao umelenga kufikisha kwa hadhira na yale maneno uliyoyaandika katika makala yako unayokusudia hadhira yako iyasome.
Ikiwa maneno unayoyaandika yatashindwa kufikisha ujumbe kikamilifu sawasawa na vile ambavyo wazo lilipokuja kwako mwanzo, itasababisha tafsiri mbalimbali kwa msomaji. Baadhi ya tafsiri ni msomaji kukataa makala yako kutokana na makosa yanayoonesha kukosekana kwa mtiririko wa kumuwezesha msomaji kukufuatilia kupokea kusudi la makala husika, tafsiri nyingine ni kumfanya msomaji kuona mwandishi amekosa umakini wa kuzingatia mambo madogo ambayo ni ya msingi kabisa (basic).
Katika makala hii ninapenda kukukumbusha mambo ambayo ukiyafanyia kazi kwa umakini yatachangia kuboresha kazi yako kutoka hatua iliyopo sasa kwenda hatua nyingine nzuri zaidi.
(a) Jambo la kwanza ni kusoma vitabu, makala au machapisho zaidi yanayohusiana na eneo ulilochagua kuandika. Maneno unayoyaandika ni matokeo (output) yanayopatikana kutokana na kuweza kuingiza maneno mengi mapya katika kiwanda chako (akili au mind). Maneno haya unayapata baada ya kusoma kwa wingi makala, vitabu au machapisho mbalimbali. Na si kupata maneno mapya pekee bali itakusaidia kuona waandishi wengine wameandika nini , namna yao ya uandishi, na kugundua pengo lilipo ili uweze kuliziba kupitia makala yako utakayoandika.
(b) Jambo la pili ni kujenga tabia ya kuandika kila siku. Uandishi ni fani au ujuzi ambao unahitaji kujengwa. Kama ilivyo aina nyingine za ujuzi hatua ya kwanza inakuwa ni kujifunza kwa nadharia na hatua ya pili inakuwa ni kufanya kwa vitendo yale uliyojifunza. Kwa kadiri ya wingi wa mazoezi unayoyafanya inachangia sana kugundua na kusahihisha makosa ambayo unayafanya. Kuandika makala ndefu yenye maneno mfano elfu moja au zaidi kwa siku moja katika wiki hakusaidii kuboresha ujuzi wako katika uandishi ukilinganisha na mtu anayeandika maneno mia mbili kila siku mfululizo bila kuwa na pengo kati ya siku na siku. Kuna maneno ya kiingereza yanasema "Practise Makes Perfect". Maneno haya yanaashiria kadiri unavyofanya mazoezi ya kuandika ni sawasawa na kuzidi kujinoa katika uandishi na hii itapelekea kuwepo kwa thamani katika makala zako kunakosababishwa na umakini ulioujenga.
(c) Jambo la tatu rafiki yangu fanya tathmini ya makala uliyoandika kabla hujaruhusu wasomaji kuiona na baada ya wasomaji. Ninaelewa ni jinsi gani inachosha kurudia kazi ambayo umetumia kiasi cha saa moja au zaidi kuandika. Na hii inaweza kuleta hali ya kuona uvivu wa kupitia kuangalia kama kuna kosa au kupoteza maana kutokana na maboresho uliyoyafanya.
Rafiki kama unataka kuona uandishi wako unakuwa basi ni muhimu kwanza wewe binafsi ukubali kupitia kazi yako na kukosoa makosa madogo madogo, pili ukubali kumpa mtu ambaye atasoma makala yako na aweze kukusaidia kuboresha na mwisho kuwa unapitia mara kwa mara kazi zako ili kuendelea kuzihuisha kadiri ujuzi wako wa uandishi unavyokua.
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako.
0 comments:
Post a Comment