Mambo 17 niliyojifunza katika kitabu cha SPEED WEALTH
Mambo niliyojifunza kutoka katika kitabu cha SPEED WEALTH kilichoandikwa na T Harv Eker
1. Ili uweze kufanikiwa na kuchomoza katika mafanikio unahitaji kumiliki biashara, ukitumia njia ya ajira ya kuwa umesoma ,umepata kazi nzuri, na ufanye kazi kwa jitihada haisaiidii sana wewe kuwa huru kifedha kwa kuwa mfumo huu haufanyi kazi katika mazingira ya sasa
2. Unaweza kuwa unahifadhi fedha ili ziweze kupitia katika riba na ziweze kukua, kiwango cha riba katika mazingira ya sasa pia ni kidogo hivo utakuta unachukua muda mwingi pia kufikia uhuru wa kifedha
3. Ukiona mtu anafanikiwa zaidi yako unahitaji kufahamu kuwa kuna maarifa ya ziada anayo ambayo wewe bado hujaweza kuwa nayo au huyafahamu, hivyo unahitaji kufanya maamuzi ya kukusudia kuwekeza muda zaidi kujifunza
4. Siri kubwa ya wengi waliofanikiwa ni kujifunza kuwa na kipato kikubwa na matumizi madogo, biashara zote zilizochomoza wamejizatiti zaidi katika kutengeneza mapato zaidi kwa kutumia matumizi kidogo
5. Kutokana na mabadiliko yanayotokea kwa kasi katika kila nyanja kuanzia teknolojia na maeneo mengine ,pia kasi ya kupata uhuru wa kifedha nayo inaongezeka, ili kuweza kuendana na haya mabadiliko kwa kasi unahitaji pia kubadilika na kuyapokea mabadiliko kwa kasi pia ili kuichangamkia fursa kwa kasi
6. Mafanikio ni kitu ambacho unaweza kujifunza kabisa, na siri ni kuwa ukitaka kuwa mtaalamu katika kada husika ni lazima ujifunze na pia uweke katika matendo yale uliyojifunza
7. Unahitaji kuwa na nia ya kujifunza na shauku ya kufanikiwa kwa haraka ili uweze kujenga kujitoa, kuwa na msimamo na kuweka jitihada katika kile unachotaka kufanya
8. Malipo unayoyapata inategemea na kiwango cha thamani unachokipeleka katika soko , ikiwa kiwango cha thamani ni kidogo na pia hakipo katika ujazo wa kujitosheleza au kumridhisha basi malipo nayo sambamba huwa kidogo.
9. Nguzo kuu nne zinazojenga thamani inayotolewa na bidhaa au huduma:
a) Hitaji : Kiwango ch a uhitaji wa thamani inayobebwa na bidhaa yako katika soko inaamua fedha utakayokuwa unalipwa
b) Upatikanaji : Thamani ya kitu huongezeka kutokana na Upatikanaji kuwa adimu katika soko. Unahitaji kutoa thamani ambayo wengine hawatoi au hawana au kufanya vitu tofauti na wengine wanavyofanya
c) Ubora: kiwango cha ubora katika thamani iliyopo katika bidhaa huamua kiwango cha malipo unayoweza kupata. Ni vema ukawa na msimamo kuwa unafanya kwa ubora au haufanyi kabisa
d) Kiasi (Uwingi): idadi ya bidhaa ulizonazo unazoweza kuziweka katika soko inaamua kiwango cha utajiri unaoweza kuipata
10. Ni vizuri kujua muda gani wa kuingia na kutoka sokoni, muda mzuri ni ule hitaji ni kubwa kuliko Upatikanaji, na kuna njia nyingi ni kushirikiana na mtu anayetoa huduma ambayo huwezi kutoa, au kukopi huduma fulani kutoka eneo lingine na kuleta katika eneo husika
11. Unahitaji kuwa na mfumo ambao unaweka shughuli zako katika utaratibu unaokusudia, hii itakusaidia sana kuongeza rasilimali ya muda n.k. Kuwepo kwa mfumo kunasaidia biashara kufanya kwa ufanisi bila wewe mhusika kuwepo eneo la biashara. Na mambo yanayohitajika kuwekewa mfumo ni masoko, uzalishaji na uendeshaji
12. Ni muhimu kujua namna ambavyo unaweza kutengeza kipato zaidi huku ukiwa wewe umelala au ukiwa umetumia fedha, muda na rasilimali kidogo
13. Maisha ni mafupi kitu chochote unachotaka kukifanya kifanye leo na vile unataka kuwa kuwa leo usingoje wakati mwingine
14. Ukihitaji kufanikiwa unatakiwa uweke jitihada katika kujifunza kujiendeleza binafsi na kuzisoma biashara
15. Kila unayemwona leo ni bora sana aliwahi kuwa wa kawaida sana wakati anaanza
16. Biashara ni ujuzi ambao unaweza kujifunza
17. Hakikisha kama unajifunza , basi unajifunza vile vitu ambavyo vinaleta tofauti na vina tija.
0 comments:
Post a Comment