Habari na karibu ndugu
mpenzi msomaji wa blogu hii. Ni matumaini yetu umekuwa na wiki ya mafanikio
sana. Ni dhahiri umekuwa ukipata mlo kamili wa akili siku hadi siku kupitia
blogu hii. Ninachopenda kukuhamasisha jitahidi katika kila makala inayowekwa
hapa tafuta vitu vichache ambavyo vitafanya tofauti kubwa inayoweza kuonekana waziwazi
au inayoweza kupimika katika maisha yako na vitu hivo viwe ni rahisi kuanza na
kuendelea navyo kadiri unavyosafiri katika safari yako ya kuelekea mafanikio.
Kwanza, ili kuwa na
viongozi wazuri unahitaji kuwapa muda; ukiwa kama kiongozi ambaye unaandaa
viongozi watarajiwa unahitaji kuwaamini wale unaowaandaa kwa kuwatamkia wazi
wazi na kuwatia moyo namna ambavyo unaamini katika uwezo wao wa kutenda mambo
wanayoyafanya na hii itaanza kuwahamasisha na kuwafanya pia wajiamini binafsi.
Unahitaji kujitolea ukiwa unamaanisha na kuwepo kwa muda watakaohitaji
uwashauri.
Pili, kuwa na msimamo
thabiti, bila kujali hali inayojitokeza unahitajika kuwaonyesha msimamo
wako ambao hauyumbishwi na unakuwa katika
kiwango kile kile kila mara katika utoaji ushauri, kujitolea muda wako na
kuwahamisha. Hii itawasaidia kujenga uaminifu au kukuamini wewe.
Tatu, tambua
kufanikisha kwao, waonyeshe kile wanachofanya kina umuhimu na thamani kwako
wewe kama kiongozi wao na pia kwa taasisi.Namna rahisi ambayo unaweza kuongeza
umuhimu katika kazi wanayofanya hawa unaowaandaa kuwa viongozi ni kuwahusisha
kuwa sehemu ya kitu cha thamani kwa kuwapa picha kubwa ambayo taasisi husika
imekusudia kuifikia na namna gani wao ni sehemu muhimu ya kufanikisha hilo
kufanikiwa.
Nne, wapatie usalama, watu
wakifahamu kuwa wapo sehemu salama ni rahisi kuwa na utayari wa kukua,
kujiendeleza kwa kujifunza, na hata kuchukua hatari kwa ajili ya kujiboresha
wao wenyewe.
Tano, toa tuzo kwa ufanikishaji wa jambo lolote,
unahitaji kuwafanya wajue nini matarajio yako na ni tuzo gani watapata au
zinawasubiri kwa wao kufanikiwa kufikia au kuzidi matarajiao yako hii
itawafanya wajitume kufikia hayo matarajio uliyoyaweka. Na ni vizuri
kuhakikisha wanapewa tuzo stahiki ambazo zifanyike kwa njia ya wazi kutegemeana
na taratibu mlizoziweka na si lazima ziwe ni za kifedha tuu bali zinaweza kuwa
za kutambua mchango wa watu husika katika kufanikisha jambo katika taasisi. Kwa
kuwapatia tuzo kwa kazi nzuri iliyofanywa itawasadia kujisukuma kufanya vizuri
zaidi.
Sita, wapatie msaada au
waunge mkono, hakuna kitu ambacho kinaumiza kama kuwapa watu kazi waifanye na
huwapatii msaada wanaostahili na rasilimali wanazozihitaji ili kufanikisha kazi
uliyowapa. Tengeneza mfumo mzuri wa wao kupata msaada kutoka kwako na msaada
unaweza kuwa ni wa kuwahamasisha, kuwajali, kifedha, kiujuzi, mafunzo au hata
kifaa sahihi cha kuwarahishia kazi au mtu wa kuwaongezea nguvu.
0 comments:
Post a Comment