Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!
Rafiki katika wiki tuna siku saba, kati ya siku hizi kuna baadhi ya watu kutegemea na ratiba ya majukumu pale anapofanya kazi anakuwa na siku moja au mbili za mapumziko. Siku hizi za mapumziko huwa zinafahamika kwa jina la wikiendi.
Lakini pia katika kalenda huwa kunakuwa na siku ambazo zipo maalum kulingana na matukio, hizi siku huwa tunaziita sikukuu. Kawaida katika siku hizi za wikiendi na sikukuu kunakuwa hamna ratiba maalum kama ambayo inakuoongoza katika siku za kawaida za majukumu yako.
Rafiki katika makala hii ninapenda kukushirikisha mambo ya msingi ambayo ukichukua hatua yatakusaidia kutumia muda vizuri katika siku hizi za wikiendi na sikukuu, pia zitachangia sana katika kukusogeza hatua moja zaidi kuelekea mafanikio yako.
Ni kawaida katika siku za kazi tunakuwa na muda maalum ambao tunatakiwa kuripoti eneo la kazi. Kuwepo kwa muda huu maalum kunasababisha kuwepo na muda maalum pia wa kulala ili uweze kuamka mapema, upate muda wa kutosha kujiandaa na upate muda wa kutosha wa kusafiri kuelekea eneo la kazi ili uweze kufika kwa wakati. Asilimia kubwa ya watu hulala kati ya saa tatu hadi saa tano usiku, na muda wa kuamka huwa kati ya saa kumi hadi saa kumi na mbili asubuhi. Ratiba hii hudumu kwa siku zote za kazi.
Katika siku za wikiendi utakuta ratiba hii inabadilika, unakuta kuna kuchelewa katika muda wa kulala kutokana na kutokuwa na ulazima ya muda maalum wa kuamka. Sababu ya pili ni watu wengi wanapenda kufidia usingizi wa zile siku za kazi ambazo amekuwa akilala masaa pungufu , hivyo atataka achelewe kuamka mpaka usingizi au uchovu utakapoisha. Kuchelewa huku huharibu siku nzima kwa sababu kama utaamka mathalani saa tano asubuhi maanake utapata kifungua kinywa muda huo wakati kawaida yako siku za kazi unapata kifungua kinywa saa tatu asubuhi.
Kiafya mwili wa binadamu huenda kwa ratiba maalum ambayo inaeleweka, kukosa ratiba inayoeleweka mwili unakuwa unachanganyikiwa na kukosa mwelekeo na hivyo kupata uchovu na kuwa dhaifu.
Rafiki hakikisha una muda maalum wa kulala na kuamka ambao unafanana kwa siku zako za kazi,sikukuu na wikiendi. Hakikisha kati ya muda wa kulala na kuamka unapata idadi ya masaa saba hadi nane. Kamwe usilale masaa pungufu au masaa ya ziada, hii itakusaidia kuwa na stamina ya kuweza kuamka na kulala muda maalum.
Ni dhahiri kama utafuata ushauri huu utaona katika siku za wikiendi na sikukuu utakuwa na muda mwingi umewahi kuamka na wakati huna vitu vya kufanya. La hasha! muda huu ndiyo muda wa pekee ambao utaleta mabadiliko makubwa katika maisha yako. Watu wote wenye mafanikio makubwa , siri kubwa ya mafanikio yao imejificha katika muda huu wa ziada kwa mambo ambayo wanayafanya.
Katika muda huu fanya mambo yafuatayo:
(a) Kuwa na muda kwa ajili yako binafsi, mara nyingi umekuwa na muda kwa ajili ya watu mbalimbali hata kwa ajili ya shughuli fulani, lakini ni watu wachache wanakuwa na muda kwa ajili yao binafsi kutafakari au kufanya meditation. Muda huu itulize akili yako inaweza kukisaidia kufikia uwezo wako wa akili katika kufikiri au kugundua na kukufanya uwe na ufanisi zaidi (mindfulness, creativity, well being).
(b) Panga ratiba ya wiki inayofuata. Hapa weka malengo makubwa matatu ambayo utayakamilisha katika wiki inayofuata. Pangilia kila siku utakuwa unafanya nini, wakati gani utafanya, rasilimali zinazohitaji. Hii itakusaidia kuwa na nidhamu ya kukataa kupoteza muda kufanya yale mambo ambayo hayachangii kufanikisha malengo yako.
(c) Fanya tathmini ya mambo uliyoyafanya wiki iliyopita. Ikiwa kuna makosa uliyoyafanya hakikisha unayarekebisha katika wiki inayofuata.
(d) Ongeza maarifa kwa kujifunza mambo mapya kupitia vitabu, semina au makala mbalimbali.
Hakikisha unafanya vitu ambavyo vitakuhamasisha na kukupa nguvu mpya ya kuweza kuanza wiki ukiwa na hamasa na uchangamfu mkubwa.
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako
0 comments:
Post a Comment