Monday, 31 October 2016

Kanuni Kumi (10) za Huduma Bora Kwa Mteja

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!
Tafiti zinaonesha asilimia sabini ya sababu zinazosababisha kampuni kupoteza wateja zinahusiana kwa kiwango kidogo sana na bidhaa. Ila sababu kubwa ni kila kitu kinachohusiana na huduma kwa mteja. Katika makala ya leo napenda kukushirikisha kanuni kumi zitakazokuongoza katika kutoa huduma bora kwa wateja:



(a) Wateja utawapata ikiwa utazalisha bidhaa au utatoa huduma zenye ubora wa hali ya juu, na wateja ambao umewapata wataendelea kutumia bidhaa au huduma yako ikiwa utakuwa na kiwango cha juu cha huduma kwa mteja (superior customer service).
(b) Unalo jukumu la kuhakikisha unajibu mahitaji na matarajio ya wateja wako kadiri inavyowezekana. Wateja wanahitaji kuridhishwa kwa kuondolewa hofu walizonazo na kutatua malalamiko yao kuhusu bidhaa au huduma yako.
(c) Wateja ndiyo kiungo muhimu cha uhai wa kampuni yako. Uwepo wa wateja ndiyo unaosababisha kampuni yako iweze kuendelea kuwepo.
(d) Wateja ni binadamu kama wewe, wana hisia, wanafurahi, wanachukia kama ambavyo kwa upande wako ingekuwa, hivyo ni muhimu mara zote kuhakikisha unawahudumia vizuri zaidi kuliko ambavyo ungependa kuhudumiwa.
(e) Wateja wana haki ya kupokea huduma bora na kupewa umakini wakati unawapatia huduma.
(f) Wateja wanakupendelea kwa kutembelea kampuni yako na haina maana kuwa wewe ndiye unawapendelea kwa kuwahudumia bali wanafanya biashara yako iendelee kukua.
(g) Lengo kuu la bidhaa unayozalisha au huduma unayotoa ni wateja unaowahudumia na siyo vinginevyo.
(h) Wateja hawakutegemei wewe bali wewe ndiye unawategemea ili biashara yako iendelee kuwepo. Hakuna kitu ambacho mteja anapoteza kama hatatumia bidhaa au huduma yako.
(i) Mwajiri au bosi wako mkuu ni mteja unayemhudumia.
(j) Ubora  wa huduma ndiyo silaha pekee ambayo itakusaidia kutangaza bidhaa au huduma yako na inasaidia kuendesha biashara yako.
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako

Saturday, 29 October 2016

Namna Bora ya Kuandika Kichwa cha Habari (Title) Katika Makala

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!
Rafiki katika moja ya makala zilizopita nilikushirikisha kuhusu jinsi ya kukabili changamoto za uandishi katika blogu .Katika hiyo makala nilieleza kwa undani mambo makuu matatu; jambo la kwanza ni kusoma vitabu, jambo la pili ni kuandika kila siku na jambo la tatu ni kufanya tathmini ya makala unazoandika. Kama hujasoma makala hiyo unaweza kubonyeza maandishi hapa chini kufungua usome kabla hujaendelea.



Katika makala hii ninapenda kukushirikisha changamoto nyingine inayohusiana na kichwa cha habari (title) cha makala husika katika blogu yako.
Kichwa cha habari cha makala ndicho kinachobeba ujumbe mkuu katika makala yako. Kichwa hiki ni muhimu kiwe na sifa zifuatazo:
(a) Kiwe na maneno machache (kifupi) kadiri inavyowezekana.
(b) Kiwe kinavutia au kumhamasisha msomaji kuweza kufungua na kuangalia maarifa yaliyobebwa na kichwa husika.
(c) Kiwe na muundo wa herufi ya kwanza ya kila neno kuwa herufi kubwa.
Faida kubwa unazozipata kwa kichwa cha habari kuwa na sifa hizo ni:
(a) Kupata wasomaji wengi ambao watakuwa wanakufuatilia.
(b) Kuonesha kiwango cha umakini katika uandishi wako.
Kuna njia mbili unazoweza kutumia kuandika kichwa cha habari bora, kifupi na kinachovutia au kuhamasisha wasomaji wako.
(a) Njia ya kwanza ni kuanza kuandika ujumbe na kumaliza na kichwa cha habari.
Katika njia hii unaandika makala yako yote ukiwa umeipangilia kuwa na sehemu kuu tatu; utangulizi (introduction), mada kuu (body) na hitimisho (conclusion).
Baada ya kukamilisha kuandika sehemu zote hizo tatu, unaipitia na kuanza kutafakari maneno machache ambayo yanaweza kubeba ujumbe wote ulioandika.
Faida ya njia hii ni kuwa haikubani wakati wa uandishi kuwa ni mambo gani uyaandike kutokana na kuwa haujaanza na kichwa cha habari ambacho kingekupa mipaka ya vitu gani vya kuandika. Kwa hiyo unakuwa huru zaidi kuweka mawazo na maarifa yako yote kuhusu mada unayoandika.
(b) Njia ya pili ni kuanza kuandika kichwa cha habari na kumaliza na ujumbe.
Njia hii ipo kinyume cha njia (a) niliyoeleza hapo juu. Hapa unaanza na kichwa cha habari ambacho kinakupa mipaka ya vitu vya kuandika maana unakuwa tayari umeshaweka mwongozo. Ni njia ambayo unahitaji kuweka jitihada sana ili kichwa cha habari kiweze kuendana na ujumbe uliomo ndani.
Pamoja na hiyo changamoto rafiki napenda nikushirikishe kifaa cha mtandaoni ambacho kinaweza kukusaidia kupata kichwa cha habari  kizuri na kinachovutia. Nenda katika Google tafuta Portent Content Idea Generator . Ukishafungua tovuti yao unaweza kuweka mada na ukawa unabofya kupata vichwa mbalimbali.
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako.

Friday, 28 October 2016

Jinsi ya Kupata na Kuongeza Wasomaji Katika Blogu Yako

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!
Rafiki katika moja ya makala zilizopita nilikushirikisha kuhusu hatua nne ambazo zinafuatwa katika uandishi wa makala katika blogu. Moja ya hatua ambayo niliandika ni kuhusu kuhamasisha. Kama hujasoma makala hiyo unaweza kubonyeza maandishi hapa chini kufungua usome kabla hujaendelea.


Katika makala ya leo napenda kukushirikisha namna ya kuangalia chanzo (source) wanapotokea wasomaji wanaotembelea blogu yako. Hapa nitaeleza namna ya kusoma hizi takwimu kisha nitaeleza namna ya kupata maana au tafsiri kutoka katika takwimu.



(a) Ingia katika Dashboard yako ya blogger, kisha bofya jina la blogu yako
(b) Nenda upande wa kushoto na bofya sehemu iliyoandikwa maneno Stats. Mara baada ya kubofya chini yake yatatokea maneno yafuatayo; Overview, Posts, Traffic Sources na Audiences.
(c) Bofya sehemu iliyoandikwa maneno Traffic Sources. Sehemu hii imegawanyika katika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza ni referring URLs, sehemu ya pili ni referring sites na sehemu ya tatu ni search keywords.
Katika sehemu ya URLs na sites wataorodhesha tovuti ambazo wasomaji wako walipata link ya makala kutoka katika blogu. Mfano m.facebook.com hii ina maana msomaji alitokea katika mtandao wa facebook kabla ya kufika katika tovuti yako.
Katika sehemu ya search keywords hii inaonesha msomaji wako alitafuta neno gani katika Google kabla ya kubofya link ya makala yako na kuisoma ikiwa ni mojawapo ya majibu ya maneno aliyoyatafuta.
Hizi sehemu zote tatu zitaorodheshwa na kupangiliwa kuanzia ambayo wasomaji wengi wameitumia yaani yenye click nyingi na kuendelea mpaka yenye click chache.
Mathalani kama Facebook ndiyo imeonekana ina namba kubwa kuliko mtandao mwingine kati ya ile iliyoorodheshwa. Hii ina maana Facebook ni sehemu ambayo unahitaji kuipa kipaumbele katika kuwafikia wasomaji wako kupitia vile unavyovihitaji katika blogu. Lakini pia kwa mitandao mingine unahitaji kuweka jitihada uweze kupata pia wasomaji au kuamua kuacha mitandao mingine ili kuwekeza nguvu zote katika mtandao wa facebook ambao umekuonyesha una wasomaji wengi.
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako

Thursday, 27 October 2016

Jinsi ya Kutatua Ukosefu wa Intaneti Katika Smartphone

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!
Rafiki kuna wakati unakuta katika smartphone yako umeweka kifurushi cha kutosha cha intaneti lakini huwezi kutumia kutokana na kuikosa. Changamoto hii husababishwa na settings za Access Point Name (APN) kuwa tofauti na zile ambazo zimetolewa na mtoa huduma.
APN ni jina ambalo mtoa huduma wa mtandao wa simu analitumia kuunganisha kati yake na mtandao mwingine wa intaneti. Hii ni kwa ajili ya kuwapatia watumiaji wa mtandao wa simu huduma ya intaneti katika simu zake.



Katika makala hii napenda kukushirikisha hatua unazohitaji kuzifuata ili kufanya settings za APN katika smartphone yako.
(a) Bofya sehemu ya settings katika smartphone yako
(b) Tafuta sehemu iliyoandikwa network au wireless & network, kisha bofya sehemu iliyoandikwa more
(c) Mara baada ya kufunguka, bofya sehemu iliyoandikwa Mobile Networks
(d) Tafuta na bofya sehemu iliyoandikwa Access Point Names
(e) Ikiwa kuna APN yoyote ambayo ilishafanyiwa settings itaonekana na jina lake. Ili kufanya settings sahihi, bofya hilo jina la APN.
(f) Utahitajika kubofya kwa kuanza sehemu iliyoandikwa Name na andika maneno yafuatayo:
i . Kama unatumia mtandao wa Vodacom andika Vodacom
ii . Kama unatumia mtandao wa Tigo andika Tigo
iii . Kama unatumia mtandao wa Halotel andika halotel
iv . Kama unatumia mtandao wa Airtel andika Tz-airtelweb
v . Kama unatumia mtandao wa Zantel andika zantel
(g) Baada ya hatua (f) bofya sehemu iliyoandikwa APN na andika maneno yafuatayo:
i . Kama unatumia mtandao wa Vodacom andika internet
ii . Kama unatumia mtandao wa Tigo andika tigoweb
iii . Kama unatumia mtandao wa Halotel andika b-internet
iv . Kama unatumia mtandao wa Airtel andika internet
v . Kama unatumia mtandao wa Zantel andika znet
(h) Baada ya hatua (g) bofya katika vidoti vitatu kulia juu , kisha chagua na kubofya neno save ili kukamilisha settings. Hakikisha pia umeweka on Mobile Data.
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako

Wednesday, 26 October 2016

Jinsi ya Kubadili Settings za Kusave Katika Microsoft Word

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!
Microsoft Word ni moja ya programu muhimu ambayo inatumika kwa kazi mbalimbali katika kompyuta. Programu hii hutumika kwa ajili ya kutengeneza/kuandika document mpya au kuboresha document ambayo ilishatengenezwa. Unaweza kutumia Microsoft Word kuandaa barua, wasifu (CV), ripoti na kadhalika.




Programu ya Microsoft Word inapokuwa imemalizika kuwa installed katika kompyuta yako, inachagua sehemu maalum katika kompyuta yako ambapo itakuwa inahifadhi document zako zote unazoandika. Ili kuweza kuhifadhi document zako unahitaji kubofya sehemu iliyoandikwa Save au Save As. Baada ya kubofya Save au Save As utapelekwa katika sehemu iliyoandikwa Documents. Hapa ndiyo sehemu ambayo programu ya Microsoft Word hupendelea kuhifadhi document unazotengeneza.
Rafiki sehemu hii ya Documents unaweza kubadilisha na kuchagua sehemu nyingine ambayo utaipendelea tofauti na hiyo ambayo programu ya Microsoft Word imekuchagulia baada ya installation.
Katika makala hii ninatumia Microsoft Word 2007 kukushirikisha hatua muhimu unazohitaji kuzifuata.
(a) Fungua programu yako ya Microsoft  Word.
(b) Kwa kutumia mouse nenda upande wa juu kushoto na bofya sehemu ambayo itaonesha maneno Office Button.
(c) Kwa kutumia mouse tena nenda upande wa chini kulia katika kiboksi kilichojitokeza baada ya hatua (b) hapo juu, bofya sehemu iliyoandikwa maneno Word Options.


(d) Katika kiboksi kipya kilichotokea bofya sehemu imeandikwa Save.
(e) Nenda sehemu iliyoandikwa default file location, bofya upande wa kulia wa kiboksi palipoandikwa Browse ili uweze kubadilisha sehemu ya kuhifadhi document zako na kuhamisha kwenda sehemu unayoipendelea.
(f) Baada ya hatua (e) hapo juu utabofya OK na utakuwa umefanikiwa kubadili.
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako

Tuesday, 25 October 2016

Jinsi ya Kutengeneza Bootable USB Drive

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!
Flash ni kifaa ambacho hutumika kwa ajili ya kuhifadhi data kutoka katika kompyuta. Flash inaweza kuchomekwa na kutolewa katika kompyuta. Kwa kiingereza kifaa hiki huitwa Flash Disk au USB Flash Drive.



Uwezo wa kifaa hiki hupimwa kwa kipimo cha MB au GB. MB ni kifupi cha neno Megabyte wakati GB ni kifupi cha neno Gigabyte. GB ni kubwa kuliko MB.
Operating System ambazo huwa zinakuwa installed katika kompyuta hupatikana katika CD au DVD. CD ni kifupi cha neno Compact Disk na DVD ni kifupi cha neno Digital Versatile Disk. CD au DVD ambayo itatumika kuinstall operating system  huwa zimetengenezwa kuwa na uwezo wa kuboot moja kwa moja.
Changamoto kubwa iliyopo sasa ni utunzaji wa CD au DVD. CD au DVD huwa zinakwaruzika au kupata scratch na hii husababisha kushindwa kuendelea kutumika. Kwa kutengeneza bootable flash inasaidia kuepuka hii changamoto. Ili kutengeneza bootable flash unahitaji kufuata hatua zifuatazo:
(a) Hakikisha umeinstall programu inaitwa PowerISO katika kompyuta yako, umehifadhi operating system yako katika kompyuta na unayo flash disk.
(b) Fungua programu ya PowerISO. Bofya katika sehemu ya Tools na uende kuchagua "create bootable USB drive".
(c) Katika sehemu iliyoandikwa  image file litafute faili ambalo lina operating system. Faili lina kuwa linaishia na .iso
(d) Katika sehemu iliyoandikwa destination USB drive , chagua flash unayoitaka kuitengeneza iwe bootable.
(e) Baada ya kumaliza hatua hizo hapo juu utakuwa tayari umetengeneza bootable flash.
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako

Monday, 24 October 2016

Uchambuzi wa Kitabu " TOUGH TIMES NEVER LAST BUT TOUGH PEOPLE DO"

Robert H Schuller ni mwandishi wa kitabu cha "TOUGH TIMES NEVER LAST BUT TOUGH PEOPLE DO" . Katika kitabu hiki mwandishi anatupa mbinu za kutumia tunapokuwa tunapitia vipindi vigumu katika maisha yetu ya kila siku. Hapa ninakushirikisha mbinu mia moja ambazo ukizitumia kipindi unapopitia magumu zitakusaidia kuvuka kipindi kigumu salama bila athari. Karibu tujifunze rafiki.



1. Watu wengi huwa wanapenda kushughulika na lawama badala ya kushughulika na tatizo
2. Tatizo huwa kubwa kama mtakosa mtazamo sahihi kuhusu tatizo husika
3. Ukiwa unatakiwa kuongea au kutoa tamko ili kushauri kitu na hauna cha kuongea , washirikishe historia yoyote inayokuhusu wewe
4. Hakuna mafanikio bila kutumia kanuni ya kuzidisha
5. Watu walio wakubwa kimafanikio ni watu wa kawaida ambao wana kiwango kikubwa cha maamuzi ambayo yamezidi maamuzi ya kawaida
6. Hakuna mtu anashindwa jumla kama atathubutu kujaribu kufanya    kitu cha thamani
7. Vipindi vigumu havidumu kamwe bali watu wagumu hudumu
8. Kitu ambacho tunatakiwa kukihofia ni hofu yenyewe
9. Kwa binadamu inaonekana haiwezekani lakini kwa Mungu mambo yote yanawezekana
10. Haiwezekani ukashindwa jumla kama utathubutu kujaribu
11. Ni muhimu kujifunza namna ya kutatua na kusimamia matatizo
12. Sio lazima kila tatizo liwe na ufumbuzi ingawa kila tatizo linaweza kusimamiwa vyema
13. Watu wanaofanikiwa ni wale ambao kamwe hawaachi kuamini
14. Ukifikiri kwa ukubwa na ukifanya kazi kwa juhudi, unaweza kufanya chochote unachotaka, unaweza kuwa vyovyote unavyotaka na unaweza kwenda popote unapotaka
15. Yaweke matatizo katika mtazamo sahihi usiruhusu tatizo likupatie udhuru
16. Mafanikio hayaondoi matatizo bali hutengeneza matatizo mapya
17. Mtu anayechagua kuyakwepa matatizo kiuhalisia anatengeneza matatizo mapya
18. Kila mwanadamu anayeishi anayo matatizo
19. Kila tatizo lina muda wake wa kuishi ambao ni ndogo
20. Matatizo huwa yanaisha
21. Hakuna tatizo litakalodumu kila tatizo litapita
22. Kila tatizo linabeba fursa ya kipekee
23. Kila tatizo litakubadilisha
24. Unao uwezo wa kuchagua tatizo likufanyie nini
25. Usipuuzie tatizo
26. Unao uwezo wa kukabiliana na tatizo
27. Mtazamo chanya hubadili tatizo lililokutoa machozi kukufanya uwe nyota kwa kukupatia uzoefu
28. Usilikuze tatizo kwa kuwa tatizo litapita
29. Hakuna mtu ambaye yuko kubadilishana matatizo na mwingine
30. Pambano kubwa ambalo wengi wanashindwa ni hofu ya kushindwa
31. Kadiri unavosubiri kutatua tatizo ndivyo unavopoteza wakati na fursa
32. Wewe binafsi ndio mwenye wajibu wa kutatua tatizo usimsubiri mtu mwingine
33. Hakuna mtu ambaye anashindwa mpaka anapoanza kulaumu wengine
34. Kila mwisho ni mwanzo mpya
35. Uongozi ni kitu ambacho kinachagua ndoto zako na kinaweka malengo yako
36. Maamuzi ya leo ndo uhakika wa kesho
37. Ni bora kujaribu kitu kikubwa na kushindwa kuliko kutokujaribu chochote na kuona umefanikiwa
38. Kushindwa hakuamaanishi wewe ndiye uliyeshindwa bali kunamaanisha hujafanikiwa bado
39. Kushindwa hakumaanishi hautimiza/haujafanikisha kitu bali kunamaanisha umejifunza kitu
40. Kushindwa hakumaanishi wewe ni mjinga bali kunamaanisha unayo imani ya kutosha
41. Kushindwa hakumaanishi umeabika bali kunamaanisha una nia ya kujaribu
42. Kushindwa hakumaanishi hauna mbinu za kufanya kitu bali kunamaanisha unahitaji kufanya kwa mbinu tofauti
43. Kushindwa hakumaanishi umepoteza maisha bali kunamaanisha unayo sababu ya kuanza tena
44. Kushindwa hakumaanishi ukate tamaa bali kunamaanisha kujaribu tena kwa jitihada zaidi
45. Kushindwa hakumaanishi hautakamilisha bali kunamaanisha jambo unalofanya litachikua muda mrefu
46. Kushindwa hakumaanishi Mungu amekuacha bali kunamaanisha Mungu ana mawazo mazuri zaidi kwa ajili yako
47. Hauhitaji kuhofia kushindwa unaweza kuwa mtu unayetaka kuwa
48. Usiruhusu tatizo likupe udhuru
49. Mtazamo ni muhimu zaidi kuliko ukweli
50. Kitu chochote cha kutisha kinapotokea usifanye chochote kwanza ila fikiri
51. Ni bora kufanya kitu kisicho kamili kuliko kutokufanya chochote kisicho na dosari
52. Tengeneza njia sehemu ambako hapatakuwa na njia
53. Usilitupilie mbali wazo kwa sababu haliwezekani lipe nafasi
54. Kamwe Usidharau thamani ya wazo
55. Unapoweza kubadili kisichowezekana kuwa kinachowezekana hayo ndio maendeleo (progress)
56. Hakuna Kushinda Kama hautaanza kufanya kitu
57. Hatua ya kwanza ya imani ni kujiamini wewe mwenyewe
58. Kama tatizo ulilonalo halijaisha je jiulize umelipatia kila ulichonacho kuhakikisha linaisha?
59. Ukiwa na imani Kama ya kuhamisha mlima hauwezi kushindwa ila ukiwa hauko tayari kulipa gharama ukashindwa
60. Hata ukiwa umezungukwa na kutokuwezekana kwingi inatakiwa usikate tamaa uendelee kuwa na imani
61. Unao uchaguzi wa kuendelea kuamini au kuacha katika kukifanikisha kile unachofanya
62. Unaweza kupumzika kwa kile unachokifanya kama unakutana na vikwazo vingi lakini sio kuacha moja kwa moja
63. Usikate tamaa hata kama mwendo unaonekana ni polepole
64. Pale mambo yanapokuwa mabaya zaidi ndipo hautakiwi kukata tamaa au kuacha kile unachofanya
65. Amini imani yako na kuwa na shaka na mashaka yako
66. Kufanya maamuzi ni rahisi kama hamna mkanganyiko katika mfumo wako wa uthaminishaji
67. Maombi ni nguvu muhimu inayovuta kila kitu ili kukufanikisha
68. Usikatishwe tamaa au kukosa ujasiri unapoambiwa hapana
69. Kuna rundo la kukataliwa kabla hujakubaliwa
70. Namna ya kutengeneza upya uimara (strength) wako
a) Tazama ulikopitia kipindi cha nyuma
b) Chunguza mambo yote yanayowezekana sasa
c) Andika gharama ambayo upo tayari kuilipa
d) Chagua jambo moja linalowezekana bila kujali gharama yake ni kubwa kiasi gani
e) Fanya kazi na uwe na subira
71. Tumaini na msaada huja katika muda ambao ameupanga Mungu
72. Mambo mema unayofanya leo yatasahaulika kesho ila we endelea kufanya mema
73. Ukifanikiwa utapata marafiki wa uongo na maadui wa kweli lakini we endelea kufanikiwa bila kujali
74. Tafuta furaha katika kufanya yale yaliyo mapenzi ya Mungu bila kujali yanatafsiriwa vipi au yanapokelewa vipi
75. Wakati watu wanapopitia magumu hutazama matatizo wanayopitia kuliko fursa zilizopo mbeleni wanakokwenda
76. Maisha ya leo ni mkusanyiko wa matokeo ya machaguo uliyoyafanya
77. Kufanikiwa katika maisha unahitaji mambo 2:
a) Kuanza kufanya kitu
b) Kuokuacha kukifanya hicho kitu ulichochagua
78. Kubali uhalisia kuwa utafanikiwa sehemu fulani kwa Namna yoyote tuu
79. Kwa maneno yoyote utakayochagua kiyatumia chagua maneno chanya na sio maneno hasi
80. Maneno hasi huleta matokeo hasi
81. Unastahili kufanikiwa Kama mtu mwingine yoyote anavyoweza kufanikiwa
82. Amini kwa namna yoyote mahali fulani kuna mtu atakusaidia kufanikiwa kufikia malengo yako
83. Amua kung'ang'ania kutimiza ndoto yako
84. Thubutu kujaribu kufanya kitu
85. Jipatie maarifa kila siku kwa kuwa na maarifa utakuwa na majibu sahihi kwa ajili ya watu wenye nguvu
86. Kuwa na mtazamo wa kutoa (giving) ndo siri ya mafanikio
87. Kadiri unavyopanda ndivyo utakavyovuna
88. Wanaofanikiwa ni wale wanaotoa jitihada/juhudi za ziada na wanaenda kupitiliza mipaka yao
89. Tumaini ni kuendelea kung'ang'ania , kuomba kwa matarajio ya kupata na kutokukata tamaa kamwe
90. Piga teke kukata tamaa au kukandamizwa
91. Yacheke matatizo yako
92. Kuwa tayari kuanza kidogo na kuongeza mipango kadiri unavyoendelea
93. Unahitaji kuwa na timu ya kufanya nayo mambo ili kufanikiwa
94. Acha kulalamika kwa sababu maisha hayawezi kuwa Kama unavyotaka
95. Funga mlango wa mambo yaliyopita yanakusononesha na utupe funguo wake usonge mbele
96. Kama bado hujafanikiwa unahitaji tu kujipanga tena upya
97. Kamwe usipoteze maono yako
98. Kabiliana na kila kilicho mbele yako ukiwa na Mungu Kama rafiki yako utafanikiwa
99. Elekeza maisha yako na matatizo yako kwa Mungu
100. Hakuna mbadala wa kufanikiwa bila kufanya kazi kwa juhudi
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako

Saturday, 22 October 2016

Matumizi Bora ya Siku za Wikiendi na Sikukuu

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!
Rafiki katika wiki tuna siku saba, kati ya siku hizi kuna baadhi ya watu kutegemea na ratiba ya majukumu pale anapofanya kazi anakuwa na siku moja au mbili za mapumziko. Siku hizi za mapumziko huwa zinafahamika kwa jina la wikiendi.
Lakini pia katika kalenda huwa kunakuwa na siku ambazo zipo maalum kulingana na matukio, hizi siku huwa tunaziita sikukuu. Kawaida katika siku hizi za wikiendi na sikukuu kunakuwa hamna ratiba maalum kama ambayo inakuoongoza katika siku za kawaida za majukumu yako.
Rafiki katika makala hii ninapenda kukushirikisha mambo ya msingi ambayo ukichukua hatua yatakusaidia kutumia muda vizuri katika siku hizi za wikiendi na sikukuu, pia zitachangia sana katika kukusogeza hatua moja zaidi kuelekea mafanikio yako.
Ni kawaida katika siku za kazi tunakuwa na muda maalum ambao tunatakiwa kuripoti eneo la kazi. Kuwepo kwa muda huu maalum kunasababisha kuwepo na muda maalum pia wa kulala ili uweze kuamka mapema, upate muda wa kutosha kujiandaa na upate muda wa kutosha wa kusafiri kuelekea eneo la kazi ili uweze kufika kwa wakati. Asilimia kubwa ya watu hulala kati ya saa tatu hadi saa tano usiku, na muda wa kuamka huwa kati ya saa kumi hadi saa kumi na mbili asubuhi. Ratiba hii hudumu kwa siku zote za kazi.
Katika siku za wikiendi utakuta ratiba hii inabadilika, unakuta kuna kuchelewa katika muda wa kulala kutokana na kutokuwa na ulazima ya muda maalum wa kuamka. Sababu ya pili ni watu wengi wanapenda kufidia usingizi wa zile siku za kazi ambazo amekuwa akilala masaa pungufu , hivyo atataka achelewe kuamka mpaka usingizi au uchovu utakapoisha. Kuchelewa huku huharibu siku nzima kwa sababu kama utaamka mathalani saa tano asubuhi maanake utapata kifungua kinywa muda huo wakati kawaida yako siku za kazi unapata kifungua kinywa saa tatu asubuhi.
Kiafya mwili wa binadamu huenda kwa ratiba maalum ambayo inaeleweka, kukosa ratiba inayoeleweka mwili unakuwa unachanganyikiwa na kukosa mwelekeo na hivyo kupata uchovu na kuwa dhaifu.
Rafiki hakikisha una muda maalum wa kulala na kuamka ambao unafanana kwa siku zako za kazi,sikukuu na wikiendi. Hakikisha kati ya muda wa kulala na kuamka unapata idadi ya masaa saba hadi nane. Kamwe usilale masaa pungufu au masaa ya ziada, hii itakusaidia kuwa na stamina ya kuweza kuamka na kulala muda maalum.
Ni dhahiri kama utafuata ushauri huu utaona katika siku za wikiendi na sikukuu utakuwa na muda mwingi umewahi kuamka na wakati huna vitu vya kufanya. La hasha! muda huu ndiyo muda wa pekee ambao utaleta mabadiliko makubwa katika maisha yako. Watu wote wenye mafanikio makubwa , siri kubwa ya mafanikio yao imejificha katika muda huu wa ziada kwa mambo ambayo wanayafanya.
Katika muda huu fanya mambo yafuatayo:
(a) Kuwa na muda kwa ajili yako binafsi, mara nyingi umekuwa na muda kwa ajili ya watu mbalimbali hata kwa ajili ya shughuli fulani, lakini ni watu wachache wanakuwa na muda kwa ajili yao binafsi kutafakari au kufanya meditation. Muda huu itulize akili yako inaweza kukisaidia kufikia uwezo wako wa akili katika kufikiri au kugundua na kukufanya uwe na ufanisi zaidi (mindfulness, creativity, well being).
(b) Panga ratiba ya wiki inayofuata. Hapa weka malengo makubwa matatu ambayo utayakamilisha katika wiki inayofuata. Pangilia kila siku utakuwa unafanya nini, wakati gani utafanya, rasilimali zinazohitaji. Hii itakusaidia kuwa na nidhamu ya kukataa kupoteza muda kufanya yale mambo ambayo hayachangii kufanikisha malengo yako.
(c) Fanya tathmini ya mambo uliyoyafanya wiki iliyopita. Ikiwa kuna makosa uliyoyafanya hakikisha unayarekebisha katika wiki inayofuata.
(d) Ongeza maarifa kwa kujifunza mambo mapya kupitia vitabu, semina au makala mbalimbali.
Hakikisha unafanya vitu ambavyo vitakuhamasisha na kukupa nguvu mpya ya kuweza kuanza wiki ukiwa na hamasa na uchangamfu mkubwa.
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako

Friday, 21 October 2016

Hatua Nne (04) Katika Uandishi wa Blogu

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!
Rafiki unapoanza kuandika makala katika blogu kuna changamoto mbalimbali ambazo utakutana nazo. Changamoto hizi zinatokana na kuwa mgeni katika eneo la uandishi wa makala. Mchakato mzima wa makala kumfikia msomaji una hatua mbalimbali ambazo zinatakiwa kuzingatiwa.
Waandishi wengi wachanga hawazifahamu hizi hatua ingawa huwa ni lazima uzipitie ili makala yako iweze kupewa umakini unaostahili. Kutokana na ugeni katika eneo hili la uandishi, waandishi wachanga wanakosa kuwa na mlinganyo katika kila hatua. 



Hatua ya kwanza ni uandishi wa makala, hii ni hatua ambayo kila mwandishi anaipitia, hakuna ambaye anairuka au kuikwepa. Ili uweze kuwa na ufanisi katika hatua hii unahitaji kuandaa mazingira sahihi yanakuwezesha kutoa matokeo bora zaidi. Mazingira sahihi yanajumuisha kuandaa vifaa vya kuandika makala, mfano wa vifaa ni programu mbalimbali kama vile Microsoft Word 2013 ambayo inaweza kukusaidia pia kufanya "proofreading" na "grammar" katika lugha.
Mazingira pia hujumuisha eneo ambalo kwako ni sahihi linaloweza kukupa umakini wa kuweza kuzalisha matokeo bora kupitia unachoandika. Mfano mwandishi mwingine anapenda akaenda sehemu iliyo kimya ili aweze kuandika vizuri zaidi. Mazingira sahihi pia yanajumuisha kuwa na maandalizi ya mada unayoenda kuandika na siyo unapofika wakati wa kuandika ndipo unaanza kutafuta mada.
Hatua ya pili ni kufanya promosheni au uhamasishaji wa makala yako kwa kuwashirikisha makundi mbalimbali. Hapa rafiki ni lazima ufahamu hata kama makala yako ina ubora mkubwa sana , kipindi cha mwanzo lazima uchukue hatua ya kuwafuata wasomaji kwa kuwapa link ambayo itawasaidia kufika katika blogu yako ili waweze kusoma, hii hali na itafika kipindi ambapo wao wasomaji watakuwa wanakufuata wenyewe kusoma makala katika blogu yako kabla ya wewe kuwafuata.
Rafiki kwa kadiri unavyoweka jitihada kuandika makala bora zinazoongeza thamani kwa wasomaji, basi vile vile unahitaji kuweka jitihada ya kuhamasisha kupitia makundi mbalimbali watu wasome makala katika blogu yako. Kama una akaunti katika mitandao ya kijamii hakikisha watu ulionao katika orodha yako wanapata makala kila unavyoweka. Programu ya hootsuite inaweza kukusaidia sana katika hatua hii.
Hatua ya tatu ni kuwasiliana (networking), hapa unahitaji kujitahidi kujibu maoni, maswali na ushauri mbalimbali ambao wasomaji wako wanatuma aidha kupitia katika blogu yako katika sehemu iliyotengwa ama kupitia barua pepe yako. Hii ni muhimu sana katika kuwafanya wasomaji wajisikie vizuri hasa kwa kuwa unapitia yale mambo wanayokushirikisha.
Mawasiliano ni ya pande mbili, upande wa kwako uliukamilisha kupitia uandishi wa makala , na wasomaji nao wanapoandika maoni, maswali au ushauri ndiyo njia yao ya kuwasiliana na wewe. Hivyo unahitaji kuwajibu kwa kila wanachoandika.
Hatua ya nne ni kujiboresha kwa kuongeza ufanisi kwa kile unachokifanya. Kama mfano unaandika makala za  basi siku hadi siku thamani ionekane inapanda kwa msomaji.
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako

Thursday, 20 October 2016

Vigezo vya Kuzingatia Katika Ununuzi wa Smartphone

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!

Kutokana na kuwepo watengenezaji mbalimbali wa smartphone, kumekuwa na changamoto ya kuzichagua. Mara nyingi nimekuwa nikiulizwa na marafiki maswali haya;je, ninunue smartphone gani? au smartphone ipi ni nzuri?

Uzuri au ubaya wa smartphone unaamuliwa na viwango vya sifa ilizonazo. Hapa nakushirikisha vitu ambavyo unapaswa kuviangalia katika smartphone kabla hujanunua. Lakini pia hii itakusaidia kupima kama unapata thamani ya fedha (value for money) unayolipa kwa kununua aina husika ya smartphone.

(a) Processor
Processor inapokuwa nzuri inasaidia katika wepesi wa ufunguzi wa programu mbalimbali zilizopo katika smartphone yako. Wepesi huu wa ufunguaji programu huchangia kurefusha muda ambao betri itadumu kabla ya kuchaji tena. Processor katika smartphone huandikwa CPU. Kadiri processor inavyokuwa na uwezo mkubwa ndivyo kasi ya ufunguaji programu inaongezeka.

(b) RAM
RAM ni memory ambapo programu yoyote inapofunguliwa katika smartphone huendeshwa kupitia sehemu hii. Kadiri RAM inavyokuwa kubwa ndivyo unaweza kufungua programu nyingi zikiwa zinatumika kwa pamoja (simultaneously) bila kusababisha smartphone yako kuganda (kustack).

(c) Battery
Betri huhifadhi umeme ambao unasaidia smartphone kutumika bila kuunganishwa katika umeme. Kiwango cha umeme unaohifadhiwa katika betri za smartphone hupimwa kwa mAh. Betri inapokuwa na kiwango kikubwa cha mAh inaashiria kuwa inaweza kukaa kwa muda mrefu zaidi baada ya kuchaji ukilinganisha na betri yenye kiwango kidogo cha mAh.

(d) Camera
Smartphone nyingi huwa zina camera ya kawaida au nyuma au primary na camera ya mbele au secondary. Uwezo wa camera nyingi huamuliwa kwa kipimo cha megapixel (MP). Kiwango cha MP kinapokuwa kikubwa kinaashiria kuwa uwezo wa camera ya smartphone ni mkubwa na mzuri, hii ina maana MP zikiwa kubwa picha au video itakayochukuliwa itakuwa inaonekana vizuri zaidi bila kuwa na ukungu.

(e) Screen au Display
Huu ni ukubwa kioo cha smartphone. Ukubwa huu hupimwa kwa inchi. Smartphone zilizo ndogo kabisa huwa na ukubwa chini ya inchi 4.5, smartphone za saizi ya kati huwa na ukubwa kati ya inchi 4.5 hadi 5.4 na smartphone kubwa huwa na ukubwa kuanzia inchi 5.4 na zaidi.

(f) Network
Hapa huonesha aina ya teknologia za network zinazokubalika katika aina ya smartphone. Kuna network zifuatazo; GSM, HSPA, LTE, 2G,3G,4G. Na hii husaidia kuamua kasi ya data kama utakuwa unatumia intaneti na hata katika upande wa sauti pia.

(g) Operating System (OS)
Hii ndio programu kuu inayoendesha smartphone. Kutegemeana na mtengenezaji huamua OS gani aitumie. Zipo nyingi lakini ambayo ni maarufu kwa sasa ni Android.

SOMA: Unawezaje Kutofautisha TABLET na iPAD?

NB:
Bei ya smartphone isiwe ndiyo kigezo kikuu utakachotumia kuamua kununua. Au uzoefu wa mtu kutokana na matumizi ya smartphone aina fulani usiwe ndiyo kigezo pekee cha kuamua kununua. Lakini tumia pamoja na vigezo nilivyotaja hapo juu kupata chaguo zuri la smartphone.

Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako

Wednesday, 19 October 2016

Jinsi ya Kuzuia Kupoteza Makala Katika Blogu Yako (Backup)

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!

Rafiki makala unazoziandika kila siku ni muhimu zikahifadhiwa katika sehemu salama. Si vema sana kuacha zikawepo pale zilipo tuu kwa sasa na kujiamini kuwa inatosha bila kuwa na sehemu mbadala ambapo unaweza kuzipata tena. Mimi natumia mtandao wa blogger kuhifadhi makala za blogu yangu. Hivi karibuni nilifanya maboresho katika blogu yangu katika muonekano wake , lakini kabla sijafanya maboresho nilihakikisha nimechukua tahadhari kwa kuhifadhi nakala ya makala zangu zote. Hii ilinisaidia pale ambapo sikuridhishwa na muonekano kuweza kurejesha katika hali iliyokuwa mwanzo kabla ya maboresho. Zoezi hili huitwa "backup". Unaweza kulifanya kila siku, wiki au mwezi kutegemeana na kiwango cha maboresho  unayoyaweka katika blogu yako.

SOMA : Jinsi ya Kukabili Changamoto za Uandishi Katika Blogu

Hapa nakushirikisha hatua ambazo unapaswa kuzifuata ili kuweza kufanya backup.

(a) Fungua "browser" katika kompyuta yako na uingie katika akaunti yako uliyoitumia kufungulia blogu. Bila shaka akaunti itakuwa ni ya Gmail.

SOMA : Faida Nne (04) Unazopata Ukiwa na Akaunti ya Gmail.

(b) Katika "browser"  yako fungua tab nyingine mbele ya hiyo ya hapo juu kipengele (a) kwa kubofya sehemu palipoandikwa "new tab". Baada ya kufunguka "new tab", nenda sehemu ya address na uandike www.blogger.com

(c) Bofya sehemu iliyoandikwa jina unalotumia kwa ajili ya blogu yako. Mfano, kwa upande wangu inasomeka hivi "Stadi za Mafanikio", hii ni kwa sababu jina la blogu yangu ni www.stadizamafanikio.blogspot.com

(d) Katika upande wa kushoto utaona kuna sehemu imeandikwa maneno "Template". Bofya katika maneno hayo. Mara baada ya kubofya utaona aina mbalimbali za template.

(e) Ukiwa bado katika ukurasa huo huo, angalia upande wa kulia juu utaona maneno "Backup/Restore". Bofya katika hayo maneno. Mara baada ya kubofya kutatokea kisanduku kingine kwa juu, bofya sehemu iliyoandikwa maneno "Download full template".

(f) Utaona faili limepakuliwa linaloanzia na neno template ikifuatiwa na namba na itaishia na neno xml. Faili hili linakuwa makala zote ambazo umeziweka katika blogu yako.

SOMA : Jinsi ya Kutumia Kompyuta Yako Kuwa Chanzo cha Intaneti

Baada ya kulipata faili hili linaloishia na xml unaweza kulihifadhi mtandao kwa kutumia barua pepe, au Dropbox. Au unaweza kuhifadhi sehemu ambako unahifadhi data zako za kieletroniki mfano katika flash.

NB:
Hatua hizi huwezi kuzitumia katika mtandao wa WordPress kwa sababu ya tofauti ya kimuundo.

Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako

Tuesday, 18 October 2016

Jinsi ya Kuandaa Tangazo la Semina au Mafunzo

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!

Waandaji mbalimbali wa kozi fupi au semina au mikutano huwa na kawaida ya kutuma taarifa zinazoeleza masuala yatakayofundishwa katika mafunzo husika.

Kupitia kiwango cha taarifa anazozituma aliyeandaa mafunzo , unaweza kutambua ni kwa kiasi gani mafunzo husika yatakuwa ya msaada katika kuongeza maarifa yako. Lakini pia itakusaidia kujua umakini na kiwango cha utaalamu wa aliyeandaa mafunzo katika mada atakayoifundisha.

Hapa ninapenda kukushirikisha vipengele ambavyo unahitaji kuvitazama katika taarifa unazotumiwa na aliyeandaa mafunzo. Lakini pia vipengele hivi vinaweza kukusaidia kufahamu mambo ambayo unahitaji kuyaweka ili uweze kueleweka kwa wale wenye uhitaji na mafunzo kipindi ambacho utahitaji kuandaa semina au kozi fupi au mafunzo.

SOMA : Mambo 3 ya Msingi Kuhusu Malengo

(a) Kichwa cha Mafunzo
Hapa unahitaji kuandika mada kuu inayobeba mafunzo yako utakayoyaendesha. Kichwa hiki ni lazima kiwe kifupi, kinachoeleweka, kinachomvutia msomaji ili aweze kufuatilia mafunzo yaliyobebwa na mada husika. Lakini pia kiwe kinaweza kumhamasisha msomaji kuchukua hatua ya kujiunga na mafunzo.

(b) Muda na Mahali
Hapa utaandika idadi ya siku mafunzo yatachukua , muda ambao utakuwa unaanza mafunzo katika siku husika. Ukumbi au eneo ambapo mafunzo yataendeshwa utaueleza hapa ili anayehudhuria aweze kujua namna ya kujipanga. Ikiwa mafunzo yanaendeshwa kwa njia ya mtandao basi unahitaji kusema muda ambao mafunzo yatakuwa katika mtandao unaoutumia. Na kuhusu mahali utataja kama ni kupitia akaunti zao za barua pepe ndipo watapokea mafunzo au kupitia sehemu maalum katika mtandao ambayo utakuwa umeiandaa watakapopatumia kuyapata mafunzo.

(c) Gharama ya Mafunzo
Hapa utaandika ada ambayo mshiriki mmoja mmoja atalipa au kikundi kitalipa kwa ajili ya kugharamia uendeshaji wa mafunzo. Ni vizuri pia umweleze mwanasemina atarajie atapata nini kutokana na ada aliyolipa.


(d) Njia ya Malipo
Hapa utaandika njia mbalimbali ambazo zinaweza kutumika kwa ajili ya kupokea malipo ya ada ya semina. Kwa njia utakayotumia kupokea ada hakikisha inaonesha uthibitisho wa mpokeaji fedha
kuwa ni wewe muandaaji wa semina. Kufanana kwa majina utakayomwelekeza mlengwa wa semina itamjengea ujasiri, kukuamini ,kuona kiwango chako cha umakini na kuweza kuzuia kutapeliwa na watu wasio waaminifu. Lakini pia anayehudhuria mafunzo aweze kutambulika kuwa amelipa ada na itumike kuwa ni njia ya kumpa ruhusa ya kuhudhuria mafunzo

Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako.

Monday, 17 October 2016

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Kipindi cha Mazoezi ya Vitendo


Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!

Kwa wanafunzi ambao wanasomea fani maalum katika elimu ya juu huwa mtaala wao unagawanywa katika vipindi viwili. Kipindi cha kwanza katika muhula huwa ni kujifunza kwa nadharia. Hapa wanafunzi hujifunza nadharia mbalimbali kuhusiana na mambo yanayohusu fani waliyoichagua. Kipindi cha pili katika muhula huwa ni kujifunza kwa vitendo. Hapa wanafunzi huwekwa katika mazingira halisi ya kazi na kuanza kuelekezwa hatua kwa hatua jinsi ya kutumia maarifa aliyoyapata darasani katika kuzalisha matokeo.

Ni mara chache utakuta chuo ulipotoka wamekupa mwongozo wa mambo gani hasa unatakiwa kuyafanya kwa kipindi unaenda mazoezi ya vitendo. Kitendea kazi ambacho chuo watakupa ni logbook, hapa utajaza mambo ambayo umeyafanya kwa kipindi chote cha mazoezi ya vitendo.

Vilevile kwa upande wa kampuni ambayo unaenda kufanya mazoezi ya vitendo wanategemea utakuwa upo katika ngazi fulani nzuri ya kuweza kuzalisha matokeo chanya. Hapa wanakutazama kama mwajiriwa mwenzao. Kwa hiyo kuna wakati utakuta unaaagizwa kazi nyingine ambazo hufahamu namna ya kuzifanya, au ni mpya kabisa hujawahi kukutana nazo kabisa.

Rafiki ni muhimu utambue na kujiuliza maswali haya nani hasa ni mhusika mkuu katika kufanikisha mazoezi haya? Je, ni chuo ambako umetoka? Je, ni kampuni ambayo umeenda kufanya mazoezi? Katika maswali haya yote mhusika mkuu ni wewe ambaye ni mwanafunzi, chuo na kampuni ni wahusika washiriki tu ambao wanakusaidia kukamilisha jukumu lako.

Rafiki nimekutana na wanafunzi mbalimbali ambao nimekuwa nawasimamia katika mazoezi yao ya vitendo. Hapa ninapenda kukushirikisha mambo ambayo ukiyazingatia yatakusaidia kufaidika kipindi cha mazoezi na hata baada ya mazoezi.

(a) Weka Malengo
Ni vizuri ukaandika malengo ambayo unakusudia kuyafikia baada ya mazoezi ya vitendo. Kila siku asubuhi kabla hujaenda katika mazoezi andika mambo angalau kwa uchache matatu utakayoyafanya yatakayochangia kukufikisha katika malengo uliyojiwekea katika kipindi hiki. Inapofika jioni fanya tathmini ni kwa kiasi gani hatua ulizozichukua tangu siku ilipoanza zinachangia au zinaathiri kufikia malengo uliyojiwekea. Kama kuna mapungufu yaliyojitokeza hakikisha unaanza nayo kuyafanyia kazi katika siku inayofuata.

SOMA : Zingatia Haya Ili Uifanye Siku Yako Bora

(b) Tembea na Notibuku
Msimamizi wako wa mazoezi ya vitendo atakuelekeza mambo mengi mapya ambayo huenda hujakutana nayo katika mazingira ya chuo. Mmoja wa wanamafanikio maarufu Jim Rohn alisema katika moja ya semina alizokuwa anafanya kuwa usiamini uwezo wa akili yako katika kukumbuka unayofundishwa ila uwe mwanafunzi mzuri kwa kuyaandika yale unayofundishwa ili uweze kutumia wakati ujao. Kufanya hivi kunachangia kupeleka ujumbe kwa wanaokuzunguka ni jinsi gani uko makini na kiwango chako cha kuzingatia mafunzo unayoyapata katika kampuni husika.

(c) Tumia Intaneti Kuongeza Ufanisi
Matumizi ya mitandao ya kijamii yameteka sehemu kubwa ya jamii. Kamwe usijisahau muda wa kazi ukautumia kutembelea mitandao ya kijamii. Badala yake tumia intaneti hasa google kujifunza namna ya kuboresha jinsi ya kufanya kazi zinazoendana na mazingira uliyopo. Hakikisha unafanya kitu bora kupita matarajio yao lakini pia kiwe kinaacha alama kuwa ulifanya kitu kikawasaidia kuboresha ufanisi katika kazi zao za kila siku. Hakikisha kipindi unamaliza mazoezi ya vitendo unawaacha katika hali bora kuliko kipindi umejiunga kufanya mazoezi.

SOMA : Umakini Unaouhitaji Kabla Hujaanza Kufanya Lolote

Rafiki mambo mengine ya kuzingatia ni kuhakikisha unakuwa nadhifu katika mavazi na kazi unazofanya, kufika kwa wakati katika eneo la mazoezi ya vitendo, kutoa taarifa kwa msimamizi endapo hautaweza kuhudhuria kutokana na dharula yoyote, kuuliza maswali mengi kadiri unavyoweza, kuwa tayari kufanya kazi za ziada ili kujifunza zaidi, na kadhalika.

Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako.

Saturday, 15 October 2016

Uchambuzi wa Kitabu cha " SECRETS OF SELF MADE MILLIONAIRE"

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!

Mwandishi na mjasiriamali Adam Khoo kupitia kitabu hiki cha Secrets of Self Made Millionare, anatushirikisha mbinu mbalimbali ambazo matajiri wengi wametumia kutengeneza vipato visivyo vya kawaida kutoka ngazi ya chini kabisa ya kiuchumi mpaka kufikia kiwango cha uhuru wa kifedha. Kitu ambacho cha kipekee kinachohamasisha ni kuwa walianza bila ya kuwa na fedha, walianza na wazo tuu.



Mambo ambayo nimejifunza katika kitabu hiki
1. Moja ya rasilimali ya pekee na thamani uliyonayo ni akili yako, kuwekeza muda na fedha kwa ajili ya elimu ya fedha ni uwekezaji wa pekee ambao malipo yake yamethibitishwa kuwa na faida zaidi.
2. Mzazi ni vizuri katika hatua ya malezi ya mtoto amjengee njaa ya mafanikio kwa kutompatia kila kitu anachoomba bali amwambie atafute mwenyewe. Lakini pia jukumu kubwa  la mzazi ni kumpatia mtoto upendo, chakula na support ya kielimu.
3. Mambo ambayo unaweza kujifunza ikiwa umeanza kutafuta mwenyewe:
(a) Jinsi ya kupambana na hali ya kuona aibu
(b) Jinsi ya kupambana na hali ya kukataliwa
(c) Jinsi ya kuongea na kutumbuiza hadhira
4. Muundo wa elimu hausadii kukujengea ujuzi wa namna ya kudhibiti fedha na stadi za maisha ambazo zinaweza kukusaidia kukufanya ufanikiwe, badala yake unaelekezwa namna ya kufanya vizuri katika masomo upate kazi nzuri.
5. Ili uweze kuwa na maisha ya mafanikio unahitaji kuwa na mtazamo wa ushindi. Watu wengi wanapenda kuwa na mtazamo wa kulaumu. Mtazamo huu umejikita zaidi katika kutoa sababu kuliko kutafuta utatuzi wa matatizo.
6. Hatua Saba Kuelekea Uhuru wa Kifedha
(a) Kuwa na Mtazamo wa Milionea
Mtazamo huu utakusaidia sana kuyaangalia mambo mbalimbali kwa jicho la tofauti sana. Sehemu ambapo watu wanalalamika kuhusu tatizo wewe utakuwa unaona fursa ya kutengeneza kipato kupitia kutatua tatizo husika. Na mabadiliko haya yatakwenda hadi katika ngazi ya tabia yako, kujifunza kwako, kufikiri kwako.
(b) Weka Kwa Ufasaha Malengo Yako ya Kifedha
Suala la kuwa tajiri halitokei kwa bahati mbaya , ni jambo ambalo linatokea kwa maksudi kabisa kutokana na uamuzi wako wa kuwa tajiri. Ufasaha wa malengo unaonekana katika kiwango sahihi unachokitaka kukipata, kiwango hiki ni lazima kiwe kinaweza kupimika. Malengo yanayowezekana kupimika yanasaidia sana katika upangaji wa mkakati, kuonesha kiwango cha jitihada kinachohitajika kuwekwa.
(c) Tengeneza mpango wa kifedha
Baada ya kukamilisha uwekaji wa malengo, ni muhimu kuwa na mpango wa kukuwezesha kufikia malengo yako. Mpango wako ni lazima uwe na ufasaha kwamba kiasi gani utakitunza, kiasi gani utawekeza, idadi ya mifereji ya kipato utakayoitengeneza, kiwango cha faida unachokitaka kutoka katika uwekezaji unaofanya. Ingawa kuna wataalamu ambao wanaweza kukusaidia kutengeneza mpango huu ila ni muhimu suala hili ukalifanya wewe mwenyewe binafsi.
(d) Ongeza kiasi chako cha kipato
Kikawaida baada ya kuwa na mpango utaona kama itakuchukua muda mrefu mpaka uweze kufikia uhuru wa kifedha. Ukweli ni kuwa unahitaji kuongeza kipato chako sio kwa kiwango cha asilimia bali ni kiwango cha maradufu, mara tatu au zaidi kadiri inavyowezekana. Na hili unaweza kulifanya bila kuacha ajira unayofanya au kuhatarisha kwa kuwekeza fedha zote unazopata kwenda katika biashara.
(e) Dhibiti mapato na matumizi yako
Ni muhimu kuangalia mlinganyo kati ya fedha unazoingiza na fedha unazozitoa. Kuingiza fedha nyingi na kuwa na matumizi ya fedha kidogo ndiyo siri kuu. Unapokuwa na matumizi kidogo inasaidia kubakia na kiasi cha fedha ambacho unaweza kuwekeza na kuhifadhi. Tofauti katika maisha ya tajiri na maskini imejengwa hapa  unafanya nini ni hiki kiasi kinachobaki.
(f) Kuza fedha ziweze kukurudia katika kiwango cha milioni
Baada ya kudhibiti matumizi yako ni vizuri kiasi kile ambacho unabakiza ukiwekeze katika maeneo ambayo faida yake utaipata katika kiwango cha milioni au zaidi. Na siyo unawekeza tuu bila kuzingatia kiwango cha faida unayopata. Hii ni muhimu sababu itafika wakati huwezi kutumia nguvu zako kutengeneza fedha bali fedha uliyonayo iwe inafanya kazi ya kukutengenezea fedha.
(g) Weka ulinzi katika utajiri wako
Utengenezaji utajiri ni suala ambalo utatumia muda na jitihada. Ni muhimu kuhakikisha haupati hasara katika uwekezaji ambao umefanya. Ulinzi unautengeneza kwa kuweka bima , kumpata mtaalamu wa kisheria ambaye anaweza kukushauri mambo ya kisheria kuhusu uwekezaji unaoufanya, na hata wataalamu wa mahesabu ya fedha ili wakuongoze katika eneo hilo bila ya kupata hasara.
7. Tabia za Watu wenye mtazamo wa kuwa milionea
Utajiri wowote huanza kwenye akili kwanza kabla ya kutokea katika uhalisia. Utajiri unapokuwa katika akili unakusaidia kuyatazama mambo mbalimbali katika hali ya fursa ya kuwa milionea zaidi. Na pia inakusaidia hata makosa yakitokea hautakufa kifedha kabisa bali utaweza kuendelea. Hamna utajiri ambao unatengenezwa kwa fedha bali unatengenezwa kutoka katika akili.
(a) Unatakiwa kwa kile unachozalisha uzidi matarajio ya wateja wako. Angalia washindani ambao wapo katika soko moja na wewe wanafanya nini, kisha ongeza thamani kwa kufanya zaidi ya kile kinachotarajiwa na mpokea huduma. Usizalishe sawasawa na matarajio ya mteja au chini ya matarajio ya mteja.
(b) Unatakiwa kuwa na uthubutu wa kuchukua hatua. Usisubiri mpaka mambo yawe yameshakwenda katika hatua nyingine ngumu ndo uchukue hatua au kusubiria hali ya mazingira ifike kiwango fulani ndiyo uchukue hatua. Usiwe mtu wa kulaumu.
(c) Kubali kubeba wajibu wa matokeo yako unayoyapata ili uweze kuwa katika control. Usilaumu wala kulalamika kwa nini jambo fulani halijawa vile umetarajia , kwa sababu itakufanya kutokuwa katika control ya kukufanya wewe ufanikiwe bali vitu vingine tofauti na wewe ndiyo vinakuwa katika control.
(d) Unahitaji kuwa na hali ya uvumilivu na kukubali kuchelewa kukumbuka kutumia fedha zako kwa ajili ya anasa au vitu ambavyo sio vya kuwekeza kukuongezea ujuzi na maarifa. Unahitaji kuwa na kusita kutumia fedha kwa ajili ya starehe au vitu ambavyo vinashuka thamani.
(e) Hakuna eneo fulani maalum ambalo ukifanya biashara ndiyo litakupa faida tuu katika vipindi vyote. Eneo ambalo ni sahihi kwa ajili ya mtu yoyote kufanya biashara ni lile ambalo analipenda sana. Sababu hili ni eneo ambalo wakati unajenga biashara yako hutaona kama unafanya kazi bali itakuwa ni sehemu ya kufurahia, lakini pia itakusaidia kukupa hamasa na msukumo wa kuendelea bila kuchoka.
(f) Unahitaji kuwa mwaminifu katika eneo la biashara unayofanya. Uaminifu uanze katika ngazi ya wateja, wafanyakazi wenzako na hata jamii. Uaminifu ni sawa na uwekezaji ambao unaendelea kujilimbikiza. Na hii ni nguzo muhimu ambayo itakusaidia wateja na kila mtu unayeshirikiana nae katika biashara kukuamini.
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako.

Friday, 14 October 2016

Hatua Saba (07) za Kukusaidia Kuelekea Uhuru wa Kifedha

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!

Rafiki kila mtu anapenda kuishi katika hali ya kuwa na kiwango cha fedha kinachoweza kuhudumia mahitaji yale ya muhimu na kufanya mambo mengine ya ziada. Asilimia kubwa ya watu wanatumia muda na nguvu ili kupata kipato kinachowasaidia kujikimu. Hivyo utakubaliana na mimi hawana uhuru katika maisha yao maana kuna muda fulani maalum lazima awepo kwa mwajiri wake,wanabadilishana muda na ujuzi wake kwa fedha (mshahara). Hapa chini nakushirikisha hatua chache ambazo ukizifanyia kazi zitakusaidia kufikia uhuru wa kifedha.




(a) Kuwa na mtazamo wa kimilionea
Mtazamo huu utakusaidia sana kuyaangalia mambo mbalimbali kwa jicho la tofauti sana. Sehemu ambapo watu wanalalamika kuhusu tatizo wewe utakuwa unaona fursa ya kutengeneza kipato kupitia kutatua tatizo husika. Na mabadiliko haya yatakwenda hadi katika ngazi ya tabia yako, kujifunza kwako, kufikiri kwako. Utakuwa ni mtu ambaye anatatua matatizo na kulipwa kutokana na kuleta suluhisho la tatizo.
(b) Weka kwa ufasaha malengo yako ya kifedha
Suala la kuwa tajiri halitokei kwa bahati mbaya , ni jambo ambalo linatokea kwa maksudi kabisa kutokana na uamuzi wako wa kuwa tajiri. Ufasaha wa malengo unaonekana katika kiwango sahihi unachokitaka kukipata, kiwango hiki ni lazima kiwe kinaweza kupimika. Malengo yanayowezekana kupimika yanasaidia sana katika upangaji wa mkakati, kuonesha kiwango cha jitihada kinachohitajika kuwekwa na pia kukupatia hamasa inayoweza kukupa stamina ya kuweza kupambana hata mambo yanapokuwa magumu.
(c) Tengeneza mpango wa kifedha
Baada ya kukamilisha uwekaji wa malengo, ni muhimu kuwa na mpango wa kukuwezesha kufikia malengo yako. Mpango wako ni lazima uwe na ufasaha ukiwa na maelezo yanayogusa masuala kama vile; kiasi gani utakitunza, kiasi gani utawekeza, idadi ya mifereji ya kipato utakayoitengeneza, kiwango cha faida unachokitaka kutoka katika uwekezaji unaofanya. Ingawa kuna wataalamu ambao wanaweza kukusaidia kutengeneza mpango huu ila ni muhimu suala hili ukalifanya wewe mwenyewe binafsi, hii ni kwa sababu wewe ndiye unayefahamu kwa ufasaha unachokitaka.
(d) Ongeza kiasi chako cha kipato
Kikawaida baada ya kuwa na mpango utaona kama itakuchukua muda mrefu mpaka uweze kufikia uhuru wa kifedha hasa ukifanya ulinganisho na hali yako ya kifedha ya sasa. Ukweli ni kuwa unahitaji kuongeza kipato chako sio kwa kiwango cha asilimia bali ni kiwango cha maradufu, mara tatu au mara nyingi zaidi kadiri inavyowezekana. Ukomo wa kiasi gani ni mara ngapi unaweza kuongeza kipato chako unaamuliwa na uwezo wako hakuna mtu anayeweza kujizuia. Na hili unaweza kulifanya bila kuacha ajira unayofanya au kuhatarisha kwa kuwekeza fedha zote unazopata kwenda katika biashara.
(e) Dhibiti mapato na matumizi yako
Ni muhimu kuangalia mlinganyo kati ya fedha unazoingiza na fedha unazozitoa. Kuingiza fedha nyingi na kuwa na matumizi ya fedha kidogo ndiyo siri kuu. Unapokuwa na matumizi kidogo inasaidia kubakia na kiasi cha fedha ambacho unaweza kuwekeza na kuhifadhi. Tofauti katika maisha ya tajiri na maskini imejengwa hapa  unafanya nini na hiki kiasi kinachobaki.
(f) Kuza fedha ziweze kukurudia katika kiwango cha milioni au zaidi
Baada ya kudhibiti matumizi yako ni vizuri kiasi kile ambacho unabakiza ukiwekeze katika maeneo ambayo faida yake utaipata katika kiwango cha milioni au zaidi. Na siyo unawekeza tuu bila kuzingatia kiwango cha faida unayopata. Hii ni muhimu sababu itafika wakati huwezi kutumia nguvu zako kutengeneza fedha bali fedha uliyonayo iwe inafanya kazi ya kukutengenezea fedha.
(g) Weka ulinzi katika utajiri wako
Utengenezaji utajiri ni suala ambalo utatumia muda na jitihada. Ni muhimu kuhakikisha haupati hasara katika uwekezaji ambao umefanya. Ulinzi unautengeneza kwa kuweka bima , kumpata mtaalamu wa kisheria ambaye anaweza kukushauri mambo ya kisheria kuhusu uwekezaji unaoufanya, na hata wataalamu wa mahesabu ya fedha ili wakuongoze katika eneo hilo bila ya kupata hasara.
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako.

Thursday, 13 October 2016

Jinsi ya Kukabili Changamoto za Uandishi Katika Blogu

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!
Pasipo kutegemea lugha gani unaitumia katika uandishi wa makala ambazo unaziweka katika blogu yako, bado suala la uandishi lina changamoto. Changamoto kubwa inatokea wakati unaoanisha kati ya ujumbe ambao umelenga kufikisha kwa hadhira na yale maneno uliyoyaandika katika makala yako unayokusudia hadhira yako iyasome.
Ikiwa maneno unayoyaandika yatashindwa kufikisha ujumbe kikamilifu sawasawa na vile ambavyo wazo lilipokuja kwako mwanzo, itasababisha tafsiri mbalimbali kwa msomaji. Baadhi ya tafsiri ni msomaji kukataa makala yako kutokana na makosa yanayoonesha kukosekana kwa mtiririko wa kumuwezesha msomaji kukufuatilia kupokea kusudi la makala husika, tafsiri nyingine ni kumfanya msomaji kuona mwandishi amekosa umakini wa kuzingatia mambo madogo ambayo ni ya msingi kabisa (basic).



Katika makala hii ninapenda kukukumbusha mambo ambayo ukiyafanyia kazi kwa umakini yatachangia kuboresha kazi yako kutoka hatua iliyopo sasa kwenda hatua nyingine nzuri zaidi.
(a) Jambo la kwanza ni kusoma vitabu, makala au machapisho zaidi yanayohusiana na eneo ulilochagua kuandika. Maneno unayoyaandika ni matokeo (output) yanayopatikana kutokana na kuweza kuingiza maneno mengi mapya katika kiwanda chako (akili au mind). Maneno haya unayapata baada ya kusoma kwa wingi makala, vitabu au machapisho mbalimbali. Na si kupata maneno mapya pekee bali itakusaidia kuona waandishi wengine wameandika nini , namna yao ya uandishi, na kugundua pengo lilipo  ili uweze kuliziba kupitia makala yako utakayoandika.
(b) Jambo la pili ni kujenga tabia ya kuandika kila siku.  Uandishi ni fani au ujuzi ambao unahitaji kujengwa. Kama ilivyo aina nyingine za ujuzi hatua ya kwanza inakuwa ni kujifunza kwa nadharia na hatua ya pili inakuwa ni kufanya kwa vitendo yale uliyojifunza. Kwa kadiri ya wingi wa mazoezi unayoyafanya inachangia sana kugundua na kusahihisha makosa ambayo unayafanya. Kuandika makala ndefu yenye maneno mfano elfu moja au zaidi kwa siku moja katika wiki hakusaidii kuboresha ujuzi wako katika uandishi ukilinganisha na mtu anayeandika maneno mia mbili kila siku mfululizo bila kuwa na pengo kati ya siku na siku. Kuna maneno ya kiingereza yanasema "Practise Makes Perfect". Maneno haya yanaashiria kadiri unavyofanya mazoezi ya kuandika ni sawasawa na kuzidi kujinoa katika uandishi na hii itapelekea kuwepo kwa thamani katika makala zako kunakosababishwa na umakini ulioujenga.
(c) Jambo la tatu rafiki yangu fanya tathmini ya makala uliyoandika kabla hujaruhusu wasomaji kuiona na baada ya wasomaji. Ninaelewa ni jinsi gani inachosha kurudia kazi ambayo umetumia kiasi cha saa moja au zaidi kuandika. Na hii inaweza kuleta hali ya kuona uvivu wa kupitia kuangalia kama kuna kosa au kupoteza maana kutokana na maboresho uliyoyafanya.
Rafiki kama unataka kuona uandishi wako unakuwa basi ni muhimu kwanza wewe binafsi ukubali kupitia kazi yako na kukosoa makosa madogo madogo, pili ukubali kumpa mtu ambaye atasoma makala yako na aweze kukusaidia kuboresha na mwisho kuwa unapitia mara kwa mara kazi zako ili kuendelea kuzihuisha kadiri ujuzi wako wa uandishi unavyokua.
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako.

Wednesday, 12 October 2016

Uhusiano Uliopo Kati ya Malengo, Uwezo na Ukuaji Wako

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!

Rafiki kuna kipindi unaweka malengo na unakuta kadiri muda unavyokwenda unaanza kupata mashaka kama unaweza kuyatimiza au kuyaleta katika uhalisia. Ikiwa utajishawishi na kuikubali hii hali kuendelea itakufanya ushindwe kutimiza malengo yako kutokana na kupoteza morali. Morali huwa inasaidia sana kusukuma mambo yaweze kutokea. Bila kujali umefikaje katika hali hiyo ya kupata mashaka ninapenda utambue kuwa unao uwezo wa kuyafikia malengo yako makuu katika maisha.

Kuna njia mbalimbali za kukusaidia kujitambua una uwezo kiasi gani wa kufanya vitu vinavyoweza kuacha alama katika dunia. Katika makala hii ninapenda kukushirikisha njia mbili.

(a) Njia ya kwanza ni kufanya tathmini binafsi kufahamu mambo gani unaweza kuyafanya vizuri sana (strength) na mambo gani uko dhaifu yaani huwezi kuyafanya vizuri (weakness). Tathmini hii unaweza kuifanya kwa namna ya kujiuliza maswali. Hapa unaandaa orodha ya maswali pamoja na majibu ambayo itakuwa inakugusa wewe binafsi.

(b) Njia ya pili ni kuwashirikisha watu wako wa karibu kama marafiki , ndugu na kadhalika ambao wanaweza kukueleza ukweli bila kukuficha au kuona aibu kuhusu mambo yale unayoweza kufanya vizuri (strength) na mambo yale ambayo huwezi kuyafanya vizuri (weakness).

Baada ya kukamilisha hatua hiyo ya kwanza itakusaidia katika kuweza kuyafikia malengo yako makuu katika maisha. Tathmini hii itachangia sana kuoanisha uhusiano wa ukubwa wa malengo yako uliyoyaweka na kiwango halisia cha rasilimali uwezo wako unaohitajika kukuwezesha utimize malengo yako. Jambo la kulizingatia  rafiki usiweke malengo ambayo yanaendana sawasawa na kiwango cha uwezo ulionao wakati au pindi unaweka malengo. Hii ni muhimu kwa sababu unahitaji fursa ya kukua (growth) unapokuwa katika safari ya kutimiza malengo yako.

Siri kubwa ambayo rafiki napenda kukuambia ni kuwa kila palipo na fursa ya kukua (growth) kuna faida kadhaa ambazo huambatana nazo, baadhi ya hizo faida ni:
(a) Kupata nafasi ya kujifunza mambo mapya na kupelekea kutengeza maarifa ambayo yanaweza kutumika kama mwongozo wa kuwasaidia wengine katika eneo husika.
(b) Kufanya mambo mapya tofauti na yale ambayo umekuwa ukiyafanya mara kwa mara na kukusaidia kupata matokeo tofauti.
(c) Kukujengea stamina itakayokusaidia kuhimili kuendelea kuweka jitihada kuelekea kuyatimiza malengo yako.
(d) Kutokukata tamaa kunakosababishwa na na dalili za awali za kushindwa kunakotokea kiasili kwa jambo lolote unalofanya linapokuwa katika hatua ya uchanga.

Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako.

Tuesday, 11 October 2016

Maana za Vibao Vya Namba Za Magari (Plate Number)

Habari rafiki!
Katika kila gari kuna sehemu mbili ambapo huwekwa vibao vyenye namba kwa ajili ya kulitambulisha gari husika. Vibao hivi huwekwa mbele na nyuma ya gari. Katika lugha ya kiingereza huitwa "plate number". Katika makala ya leo ninakushirikisha namna ya kupata ujumbe unaowasilishwa na pindi unaposoma kibao husika cha namba ya gari.


Aina za Vibao vya Namba za Magari
1. Kibao chenye rangi ya njano na namba inayoanza na herufi T
Kibao hiki kinabeba maana kuwa gari husika limesajiliwa kutumika kwa ajili ya shughuli binafsi. Kwa kiingereza inasemwa "private use". Magari yenye vibao hivi hayaruhusiwi kutumika kwa ajili ya biashara.
2. Kibao chenye rangi nyeupe na namba inayoanza na herufi T
Kibao hiki kinabeba maana kuwa gari husika limesajiliwa kwa ajili ya matumizi ya biashara. Kwa kiingereza inasemwa "commercial use". Mfano mzuri daladala au basi za kubeba abiria na taxi.
3. Kibao chenye rangi ya njano na namba haianzi na herufi T
Kibao hiki kinabeba maana kuwa gari husika linamilikiwa na taasisi ya umma au serikali. Hapa kuna makundi yafuatayo:
(a) SU - shirika la umma , mfano vyuo vikuu vya serikali
(b) SM - Serikali za Mitaa , mfano ni halmashauri
(c) STK,STL,STJ - serikali, mfano ni wizara
4. Kibao chenye rangi nyekundu na namba inayoanza na herufi DFP au DFPA
Kibao hiki kinabeba maana kuwa gari husika limetolewa kwa ajili ya matumizi ya miradi inayofadhiliwa na wafadhili kutoka nje ya nchi.
5. Kibao chenye rangi ya bluu na namba inayoanza na herufi T kufuatiwa na namba na kisha herufi CD
Kibao hiki kinabeba maana kuwa gari husika linamilikiwa na moja ya shirika la umoja wa mataifa. Mfano shirika la Afya Duniani (WHO).
6. Kibao chenye rangi ya kijani na namba inayoanza na herufi T kufuatiwa na namba na kisha herufi CD
Kibao hiki kinabeba maana kuwa gari husika linamilikiwa na ofisi za ubalozi wa nchi fulani. Mfano ubalozi wa Ufaransa.
7. Kibao chenye rangi nyeusi na namba zimeandiwa kwa rangi ya njano
Kibao hiki kinabeba maana kuwa gari husika linamilikiwa na Jeshi la  Polisi. Namba hizi huwa na herufi PT
8. Kibao chenye rangi nyeusi na namba zimeandiwa kwa rangi ya njano
Kibao hiki kinabeba maana kuwa gari husika linamilikiwa na Jeshi la Wananchi (JW). Namba hizi huwa na herufi JW.
9. Kibao chenye rangi ya kijani na namba zenye herufi MT
Kibao hiki kinabeba maana kuwa gari husika linamilikiwa na Jeshi la Magereza.
Unaweza kubofya hapa ili kuweka barua pepe yako au rafiki yako ambaye unapenda makala hizi azipate moja kwa moja katika barua pepe.

Monday, 10 October 2016

Uandishi Sahihi wa Siku na Mwezi Katika Mwaka

Habari rafiki mfuatiliaji wa makala mbalimbali katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!


Muda unaweza kuoneshwa kwa vipimo mbalimbali. Kipimo kidogo  cha muda ni sekunde. Sekunde zikikusanyika na kufika idadi ya sitini  (60) tunapata dakika moja (01). Dakika zikikusanyika na kufikia idadi ya sitini (60) tunapata saa moja(01). Saa zikikusanyika na kufika idadi ya ishirini na nne (24) tunapata siku moja (01). Siku zikikusanyika na kufikia idadi ya saba (07) tunapata wiki moja (01). Wiki zikikusanyika na kufika idadi ya nne (04) tunapata mwezi mmoja  (01). Miezi nayo ikikusanyika na kufika idadi ya kumi na mbili (12) tunapata mwaka mmoja (01).
Katika makala hii nimeigawa katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza nitaeleza namna sahihi ya kuandika siku wakati sehemu ya pili nitaeleza namna sahihi ya kuandika mwezi. Katika sehemu zote mbili nitaonesha namna ya kuandika kwa maneno kamili na namna ya kuandika kwa ufupisho.


Uandishi wa Siku
Kama nilivyoeleza hapo juu kuna idadi ya siku saba. Katika siku hizi saba ,kuna siku tano ambazo ni kwa ajili ya kufanya kazi na kuna siku mbili kwa ajili ya kupumzika. Siku hizi mbili hufahamika kwa jina la wikiendi. Kuna uwezekano pia kutegemeana na majira katika wiki kuwa na siku zenye shughuli maalum, shughuli hizi zinaweza kuwa za kidini, kitaifa na kadhalika. Siku hizi zenye shughuli maalum zinaitwa sikukuu ambapo zinategemea sana tarehe katika kalenda. Siku za wikiendi na sikukuu zinatumika zaidi kwa ajili ya mapumziko.




(a) Uandishi wa siku kwa maneno kamili
Siku za Wikiendi
Majina ya siku hizi katika lugha ya kiswahili ni  Jumamosi na Jumapili. Majina ya siku hizi katika lugha ya kiingereza ni Saturday na Sunday.

Siku za Kazi
Majina ya siku hizi ni Jumatatu, Jumanne, Jumatano, Alhamisi na Ijumaa. Majina ya siku hizi katika lugha ya kiingereza ni Monday, Tuesday, Wednesday, Thursday, Friday.


(b) Uandishi wa siku kwa ufupisho
Siku za Wikiendi
Katika lugha ya kiingereza hutumika herufi tatu za kwanza yaani Sat na Sun. Katika lugha ya kiswahili yamekuwa yakitumika maneno Jmosi na Jpili au J1 na J2 lakini namna sahihi ya kuandika hizi siku kwa ufupisho ni Jumamosi na Jumapili.

Siku za Kazi
Katika lugha ya kiingereza hutumika herufi tatu za kwanza yaani Mon, Tue, Wed, Thu na Fri. Katika lugha ya kiswahili yamekuwa yakitumika maneno Jtatu, Jnne,Jtano, Al, Iju au J3,J4,J5 lakini namna sahihi ya kuandika hizi siku kwa ufupisho ni Jumatatu, Jumanne, Jumatano, Alhamisi na Ijumaa.


Uandishi wa Mwezi
Idadi ya miezi ikifika kumi na mbili huitwa mwaka. Mwezi unaweza kuwa na idadi ya siku thelathini au thelathini na moja isipokuwa mwezi februari ambao unaweza kuwa na siku ishirini na nane au ishirini na tisa. Idadi ya miezi ikiwa ni mitatu huitwa robo mwaka. Kwa kuwa kuna miezi kumi na mbili hivyo katika mwaka ukiugawa katika miezi mitatu utapata robo nne. Idadi ya miezi ikiwa ni sita huitwa mwaka. Kwa kuwa kuna miezi kumi na mbili hivyo ukigawa katika miezi sita utapata nusu mbili.



(a) Uandishi wa mwezi kwa maneno kamili
Majina ya miezi katika lugha ya kiswahili ni Januari, Februari, Machi, Aprili, Mei, Juni, Julai, Agosti, Septemba, Oktoba,Novemba na Disemba.
Majina ya miezi katika lugha ya kiingereza ni January, February, March, April, May,June, July, August, September, October,November na December.


(b) Uandishi wa Mwezi kwa ufupisho
Katika lugha ya kiingereza hutumia herufi tatu za kwanza yaani Jan, Feb, Mar, Apr, May, Jun, Jul, Aug, Sep, Oct, Nov na Dec. Katika lugha ya kiswahili kwa ufupisho inafanana na hapo juu kipengele (a).


Unaweza kubofya hapa ili kuweka barua pepe yako au rafiki yako ambaye unapenda makala hizi azipate moja kwa moja katika barua pepe.

Sunday, 9 October 2016

Faida Nne (04) Unazopata Ukiwa na Akaunti ya Gmail.

Habari rafiki yangu unayefuatilia makala zinazowekwa katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!
Leo napenda kukuletea mambo manne (04) ambayo unaweza kuyafanya kwa kuwa na akaunti ya barua pepe kutoka kampuni ya Google. Akaunti hii hufahamika kwa jina la Gmail.

1. Nafasi ya ukubwa wa kiasi cha Gigabyte 15 kwa ajili ya kuhifadhi taarifa zako mtandaoni
Kila mtu ambaye ana akaunti ya Gmail anapata sehemu ya kuhifadhi "data" yenye ukubwa wa kiasi cha Gigabyte 15. Hii nafasi inapatikana bure bila malipo yoyote. Na unaweza kuzitumia taarifa zako sehemu yoyote duniani ambapo umeunganishwa na mtandao.

2. Kuhifadhi orodha ya majina kutoka katika kumbukumbu ya simu yako
Kila mtu ambaye ana akaunti ya Gmail anapata nafasi ya kuhifadhi majina, namba za simu kutoka katika kumbukumbu ya mawasiliano ya simu husika. Hii huduma pia inapatikana bila ya malipo yoyote. Ni huduma ambayo huwa inasaidia sana wakati aidha unapotaka kubadili simu yako ama simu inapokuwa imeharibika ama simu imepotea. Ikiwa umehifadhi orodha yako katika Gmail utaweza kurejesha orodha ya majina na namba za simu kwa haraka na urahisi.

3. Kuwa na blogu katika mtandao wa blogspot.com
Kila mtu ambaye ana akaunti ya Gmail anaweza kufungua blogu ambapo ataweza kuweka taarifa au maarifa mbalimbali kwenda kwa jamii husika. Blogu hii ataifungua bila ya malipo yoyote. Jina lake la blogu atalipendekeza kutegemeana na anavyoona inafaa na baada ya jina hilo ambalo amependekeza litafuata neno .blogspot.com

4. Kuweka programu mbalimbali katika simu zinazotumia Google Android OS
Programu mbalimbali ambazo zinatumika katika smartphone unaweza kuzipata kutoka katika Play Store. Ili uweze kuziona na kuchagua programu hizi kutoka play store unahitaji kuwa na akaunti ya Gmail. Mfano tunapowapelekea mafundi wa simu watuwekee programu kama vile WhatsApp, You tube, Facebook na kadhalika, wanachofanya hasa ni kutumia akaunti ya Gmail kuingia playstore, kutafuta programu ulizomwambia na kuziweka, ambapo ni kitendo ungeweza pia kukifanya ikiwa unayo akaunti ya Gmail.
Endelea kutembelea mtandao huu kujifunza zaidi.

Saturday, 8 October 2016

Uchambuzi wa Kitabu cha " THE 21 IRREFUTABLE LAWS OF LEADERSHIP"

Habari rafiki,
John C. Maxwell ni mmoja wa waandishi maarufu ambao amedumu akitushirikisha mambo mbalimbali ambayo amejifunza katika maisha yake. John ni mwanafalsafa mzuri sana katika eneo la Uongozi. Wiki hii nimepata nafasi ya kusoma kitabu chake kinachoitwa " THE 21 IRREFUTABLE LAWS OF LEADERSHIP". Hapa chini ninakushirikisha maarifa machache kwa muhtasari ambayo nimejifunza kutoka katika kitabu hiki.


1. Mafanikio yoyote ambayo mtu anayapata yanaamuliwa na uwezo wake wa uongozi, ili kuweza kufanikiwa zaidi ni lazima uingie gharama ya kuweka jitihada kujiimarisha katika eneo la uongozi , na hii huwezekana kwa kupitia kujifunza. Uwezo wako wa uongozi unapoongezeka husababisha ufanisi pia kuongezeka.
2. Mambo makuu mawili ambayo yanahitajika kufanyika ikiwa kampuni haifanyi vizuri kibiashara:
(a) Kuwafundisha wafanyakazi wake kuboresha uwezo wao wa kutoa huduma bora ya viwango vya pekee kwa wateja.
(b) Kumfukuza kiongozi ambaye yupo sasa kwa sababu ameshindwa kufanya kazi yake ya uongozi kusaidia kampuni kuweza kufanya vizuri katika biashara.
3. Hakuna mafanikio yoyote ambayo yanaweza kutokea katika kipindi kifupi mfano ndani ya siku moja. Mafanikio yanahitaji nidhamu ya kujifunza kwa uendelevu kidogo kidogo. Muendelezo huu wa kujifunza usio na ukomo au nafasi kwa kuruka kati ya siku moja na nyingine ni sawa na uwekezaji ambao ukiupima kwa kutazama muda tangu umeanza kufanya uwekezaji kwa kujifunza ni gharama uliyolipia ili kuwa sawasawa na uliyojifunza.
4. Kabla hujaanza kufanya mradi au project yoyote ni vizuri kuhakikisha umefanya tathmini kwa upande chanya na upande hasi pia kutokana na uzoefu ulionao ili kama kuna mazuri ambayo uliyafanya kupitia miradi iliyopita uyachukue yakusaidie kupata urahisi wa kufanya mradi wa sasa na kama kuna mabaya ambayo yalikukwamisha yakusaidie kuyaepuka usiyarudie. Washirikishe wataalamu mbalimbali ambao wanaweza kukusaidia kufanya homework kujua vitu vinavyohusiana na mradi unaofanya ili wakusaidie taarifa muhimu zinazohitajika kufanikisha mradi.
5. Kiongozi yoyote hutunza mahusiano na wale anaowaongoza kwa kuhakikisha thamani inapewa kipaumbele. Thamani katika mahusiano ya kiongozi na anawaongoza inaweza kuwa kwa njia zifuatazo:
(a) Kuwathamini unaowaongoza kupitia njia ya kuwajali kwa kufanya mambo madogo kama kuwasalimu, kuwajulia hali na kadhalika.
(b) Kuongeza thamani kupitia yale mambo ambayo umejifunza au unayafahamu lakini wao hawayafahamu. Hapa unawasaidia kwa kuwapa maarifa na hivyo wanakuwa wamepata thamani kupitia kuwa na wewe.
(c) Kuheshimu vile vitu ambavyo wao wanavithamini, kwa kufanya hivi kunajenga mahusiano mazuri na kuona unawaheshimu.
6. Kiongozi anatakiwa kujenga uaminifu kwa watu anaowaongoza, uaminifu hujengwa kupitia matendo ya kiongozi na sio maneno anayoyazungumza kwa watu anaowaongoza. Kiwango cha watu kumwamini kiongozi hudhihirika kupitia heshima wanayompa kiongozi, kiongozi atapata heshima kutoka kwa watu wake ikiwa:
(a) Atafanya maamuzi ambayo yanaleta tija au manufaa kwa ajili ya wale anaowaongoza.
(b) Atakubali kukosolewa pale anapoenda tofauti au kukubali makosa ambayo ameyafanya aidha yawe katika maamuzi ama katika utekelezaji au utendaji.
(c) Atayapa kipaumbele maslahi ya wale anaowaongoza na kuyaweka pembeni na kuuacha maslahi yake binafsi.
7. Kiongozi mzuri ni yule ambaye anaweza kusoma hali au kuelewa nyakati husika wale anaowaongoza wanapitia. Kabla hajatatua tatizo lolote ni vizuri kujitahidi kukusanya taarifa za kutosha ili ziweze kusaidia katika kutumia uwezo wako wa kuongoza kutatua tatizo linalowakabili wale unaowaongoza. Ni muhimu kiongozi kuwa na kitu cha ziada ambacho wale anaowaongoza hawana ili waweze kumheshimu , kumsikiliza na hata kutekeleza maagizo anayoyatoa kwa kuwa wale anaowaongoza wanaamini katika uwezo wake mkubwa alionao wa uongozi katika kuwavusha kutoka hatua waliopo kwenda hatua iliyobora zaidi.
8. Ubora au sifa au uwezo alionao kiongozi unaweza kufahamika kutegemeana na watu wake wa karibu. Kikawaida watu wanavutiwa na kiongozi mwenye sifa zinazolingana na wao au uwezo au ubora kama walionao . Mara baada ya kujitathmini ukiona watu walio karibu na wewe sio wenye vile viwango vinavyofanana na wewe unaweza kuamua kuanza kuwekeza katika kujifunza ili ukuze uwezo wako au ubora wako na hivyo itapelekea kuwavutia na kuwaleta karibu watu ambao mnaendana uwezo au ubora.
Endelea kutembelea blogu hii kujifunza zaidi.

Friday, 7 October 2016

Unawezaje Kutofautisha TABLET na iPAD?

Habari rafiki,
Kutokana na maendeleo makubwa yanayotokea katika teknologia kumekuwa na vifaa vya aina mbalimbali vinatengenezwa ili kusaidia kwanza  kuendana na kasi ya ukuaji katika teknologia lakini pili kurahisha utaratibu wa kawaida wa utendaji kazi kwa kutumia vifaa hivi.
Ni hakika katika jamii yetu utakuwa umekutana na aina za simu ambazo zinakuwa na kioo kikubwa chenye saizi kuanzia inchi saba, nane au zaidi.Aidha kutegemeana na namna mtu husika anavyofahamu ama urahisi wa kutamka kutoka kwa mhusika inachangia sana katika kifaa husika kitakavyoitwa. Aina hizi za simu kitaalamu zinaitwa "Tablet".


Kuna makampuni ya aina mbalimbali ambayo wanatengeneza hizi "tablet". Kwa kuyaorodhesha ni Apple, Nokia,HP, Dell, Lenovo, Toshiba, Asus, Samsung, Google Nexus na kadhalika.
Katika hizi "tablet" kuna programu maalum ambayo inawekwa na mtengenezaji ili kumsaidia mtumiaji kutumia kifaa hiki. Programu hii
inatambulika kwa lugha ya kiingereza "Operating System". Kuna aina tatu maarufu za "Operating System" ambazo zinatumika katika "tablet";
1. Apple iOS
Hii ni "Operating System" ambayo imetengenezwa na kampuni ya Apple. Mara nyingi huwekwa katika bidhaa za kampuni hii tuu.
2. Google Android OS
Hii ni "Operating System" ambayo imetengenezwa na kampuni ya Google. Hizi hutumiwa na kampuni zingine pia sio Google peke yake lakini hazitumiwi na kampuni ya Apple.
3. Microsoft Windows Phone OS
Hii ni "Operating System" ambayo imetengenezwa na kampuni ya Microsoft. Hizi hutumiwa mara nyingi na bidhaa za kampuni ya Nokia.
"Tablet" ambazo zimetengenezwa na kampuni ya Apple zinatumia "operating system" ya iOS. Hizi zinafahamika kwa jina maarufu la "iPad". Ni jina ambalo kampuni ya Apple wanatumia kuzitambulisha "tablet" zao kwa wateja.
"Tablet" zingine ambazo zimetengenezwa na kampuni nyingine kama nilivyoorodhesha hapo juu hutumia "operating system" aidha ya Android au Windows. Hizi ndiyo ambazo hutumia jina la "tablet".
Kwa mfano kama unatumia "tablet" iliyotengenezwa na kampuni ya Samsung si sahihi kuiita iPad bali unapaswa kuiita "tablet" au "Samsung Tablet".
N.B:
Aina nyingine za "operating system" zinazotumika katika simu ni Symbian OS, web OS, Blackberry OS na kadhalika.
Endelea kutembelea blogu hii kujifunza zaidi.