Saturday, 12 November 2016

Uchambuzi wa Kitabu cha " GETTING RESULTS THE AGILE"

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!
J.D Meier ni mwandishi wa kitabu cha GETTING RESULTS THE AGILE WAY. Mwandishi katika kitabu hiki anatueleza mfumo wenye nguvu ya kukupatia matokeo katika kazi na maisha. Na mwandishi anazidi kusisitiza kuwa siri kubwa ya kupata matokeo imefichwa katika uwezo wa kuendana na mabadiliko. 





Rafiki hapa nakushirikisha mambo muhimu ambayo nimejifunza katika kitabu hiki:
1. Uwezo wetu wa kupokea mabadiliko inaamua kuhusu kiwango cha mafanikio
2. Ni muhimu kujenga uwezo wa kutawala mabadiliko na siyo mabadiliko yakutawale na kukuendesha
3. Unapokutana na changamoto ambazo zimekuzidi uwezo , ujuzi hata maarifa , njia ya pekee ya kushinda ni kujifunza mifumo ambayo wanatumia wengine katika kuleta matokeo kwao nawe unatumia njia hiyo
4. Ni vizuri kuwa na uwajibikaji kuhusiana na muda wako, weka mipaka kuhusiana na muda ambao unaweza kuuutumia kuhusiana na jambo fulani, weka vipaumbele na focus katika mambo kadhaa
5. Ni vizuri kuamua jinsi ya kudhibiti taarifa unazozipata kuna taarifa nyingine ni za kupokea na kuzitupilia mbali , si taarifa zote unahitaji kuzibeba na kuendelea nazo
6. Ni muhimu kujifunza namna ya kusimamia miradi itakuwezesha kulivunjavunja tatizo kubwa kuwa dogo dogo na kukusaidia kupata matokeo ndani ya muda husika
7. Mambo mengi tunajifunza shuleni na kazini , lakini ni mambo machache tunajifunza kwa muda mfupi ambayo yanabadilisha maisha yetu
8. Ni muhimu kujua thamani gani unaitoa katika kile unachofanya kuliko kufanya kwa lengo la kukamilisha tuu uonekane umemaliza shughuli husika
9. Ni vema kuwa na mipaka ya muda, nguvu ambayo unayoweza kuwekeza katika shughuli fulani na siyo kufanya tuu ili kuonekana umefanya maana unaweza kupoteza muda na nguvu nyingi katika shughuli bila kuwa na uangalizi. Kuwa na mipaka kunakusaidia kuwa na mlinganyo katika maisha
10. Kujua kipimio chako cha mafanikio kunakusaidia kuweka vipaumbele katika yale unayoyafanya
11. Ni muhimu njia unayotumia kufanikisha jambo lako iwe inaendana na misingi yako ila pia ni njia inayoaminika na inayoweza kutumiwa na yoyote na kutoa majibu yale yale, na pia ni njia ambayo inaweza kuboreshwa na pia ni njia ambayo inaongeza ufanisi wako na inapunguza udhaifu wako
12. Ili kuweza kujifunza zaidi unahitaji kufanya tathmini ya kila wiki kipi ambacho kinafanya kazi kwako, uimara wako, udhaifu wako, yale ambayo hayafanyi kazi kwako achana nayo tafuta namna mpya ambayo itakusaidia kupata matokeo bora zaidi
13. Ili kuweza kupata matokeo yanayohitajika ni muhimu kujua jinsi ya kudhibiti muda, nguvu na utumiaji wa mbinu bora za kuifanikisha. Nguvu huamuliwa na shauku uliyonayo katika kukamilisha jambo, na muda unaotumia katika jambo huamuliwa na nguvu uliyonayo ya kulitenda jambo husika
14. Kanuni ya 3
Hapa unaamua kuhakikisha unakamilisha mambo matatu tu katika mwaka, mwezi, wiki hata siku hii inakusaidia kuweka kipaumbele na mipaka ya vitu unavyotaka kuvipata ndani ya muda fulani
15. Kila wiki ni mwanzo mpya, hakikisha kila jumatatu unakuwa na maono ya Wiki, matokeo ya kila siku na kufanya tathmini kila ijumaa kuhusiana na matokeo matatu ambayo unayalenga kuyapata
16. Katika yale unayofanya ni muhimu kuwa na mwendelezo katika kutoa thamani sawasawa na jinsi unavyokua au unavyoongezeka kutokana na shughuli zako
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako.
Goodluck Moshi
Author
StadizaMafanikio

0 comments:

Post a Comment