Tuesday, 15 November 2016

Mambo Matano (05) Yanayosababisha Kushindwa

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!

Rafiki si wote wanajifunza kutokana na makosa wanayoyafanya au kutambua mapema makosa waliyoyafanya ili wasiyarudie. Kuwa na mwongozo kutasaidia sana kujua namna ya kuenenda katika mambo haya.

Katika maisha ya kila siku kuna mambo matano yanayosababisha kushindwa. Ukiyafahamu na kujua jinsi ya kuyakabili utakuwa umesaidia kuondoa vizuizi katika njia yako ya kuelekea mafanikio.

Jambo la kwanza ni kulaumu wengine kuwa ndiyo wamesababisha kutokea kushindwa. Hii hali hujitokeza kipindi ambapo kosa limetokea badala ya kubeba wajibu wa kuuliza mambo gani yamechangia kuwafikisha katika kushindwa badala yake unamtafuta mtu wa kumlaumu kama yeye ndiye chanzo kikuu cha kushindwa.

Jambo la pili lipo kinyume na hilo la kwanza , hapa unakuta unajilaumu binafsi kuwa wewe ni chanzo cha kusababisha kushindwa. Hapa badala ya kupambana na tatizo lililosababisha kushindwa, kupambana ili kulitatua na kuzuia lisijirudie , badala yake unajilaumu. Suala kubwa si kushindwa je umeridhika na kushindwa huko, ukiridhika na kushindwa maana yake umekubaliana na hali na hujipatii nafasi ya kukua kupitia kujiendeleza binafsi.

Soma Makala Hii Inayohusiana : Namna ya Kutambua Dalili Za Kushindwa

Jambo la tatu ni kutokuwa na malengo. Kukosa malengo ni sawa na kutokuwa na uelekeo wa safari yako yaani unasafiri lakini hufahamu kituo cha mwisho cha safari yako. Kutokuwa na malengo kunasababisha kutokuwa na umakini wa kuzingatia wapi uweze kuelekeza nguvu na vipaji ambavyo umepewa na muumba wako.

Jambo la nne ni kutokuwa na malengo sahihi. Watu wengi wanafanya kosa la kutokupanga malengo yao wao wenyewe badala yake wanawaachia watu wengine kama wanafamilia au marafiki au mazingira kuwasaidia kupanga. Wanapofika mwisho wa safari ya kutimiza lengo husika wanakosa furaha kutokana na kukosa uhusiano wa lengo kutokuwa yeye ndiye mwanzilishi au umiliki wa lengo.

Jambo la tano ni kupenda kutumia short cut. Matumizi ya shortcut huonekana ni njia ya haraka ya kupata matokeo. Changamoto ya njia hii ni kuwa matokeo unayoyapata hayadumu yanakuwa ya muda mfupi , kwa sababu ili kupata matokeo ya kudumu ni lazima kazi ifanyike ambayo huhesabika kuwa ni gharama ya kufikia matokeo husika.

Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako.

Goodluck Moshi
Author
StadizaMafanikio

0 comments:

Post a Comment