Friday, 4 November 2016

Mbinu Tano (05) Zitakazomzuia Mteja Wako Kukasirika

Habari rafiki yangu ambaye ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya Stadi za Mafanikio!

Unaposhindwa kukidhi mahitaji ya mteja sawasawa na matarajio yake, au mteja anapoona mtoa huduma anamkwepa au mteja anapokosa ushirikiano kutoka kwa mtoa huduma , au anapokuwa hana furaha na huduma aliyopatiwa,hii hali humfanya mteja apate hasira.




Kama utakosa umakini namna ya kumhudumia mteja wa namna ambaye kimsingi tayari amejeruhiwa ,itakusababisha kumpoteza mteja huyo moja kwa moja. Hivyo ni muhimu kwa kila mmliki wa biashara au mtoa huduma yoyote kuhakikisha kuna mikakati thabiti iliyowekwa ambayo inaelekeza namna ya kuhudumia mteja mwenye hasira au mteja ambaye hana furaha.
Katika makala ya leo rafiki napenda kukushirikisha mbinu ambazo unaweza kuitumia kama mwongozo pia kukusaidia unapokutana na aina hii ya wateja.
(a) Epuka kuahidi kwa mteja kumpatia huduma au bidhaa ambayo hauna uhakika na uwezo wa kumpatia. Ahidi yale mambo ambayo unauhakika yapo ndani ya uwezo wako na unaweza kuyatimiza kwa kiwango kizuri.
(b) Fahamu kwa kina matarajio ambayo mteja anayo katika huduma au bidhaa anayotarajia kupokea kutoka kwako na uhakika wa uwezo wako kukidhi matarajio ambayo amekueleza.
(c) Ikiwa kuna mazingira yametokea na imesababisha ugumu wa kuweza kutimiza ahadi uliyoweka kwa mteja, kwanza ni vizuri uwe wazi na mkweli kwa mteja wako kumuelewesha kuwa hutaweza kutimiza ahadi, pili nenda hatua ya ziada umpatie mteja huduma au bidhaa mbadala ili kuokoa muda wake na pia kupunguza usumbufu.
(d) Ni muhimu na daima hakikisha mteja anapokea mrejesho kutoka kwako kuhusiana na mwenendo au hatua ulizofikia katika kuhakikisha unamridhisha. Kuwa na taarifa ni kuwa na nguvu (information is power).
(e) Jaribu kuwa na picha mapema jinsi ambavyo mteja atapokea kutoka kwako taarifa ambayo ipo kinyume na matarajio yake ili iweze kukusaidia kufanya maandalizi mazuri kabla hujakutana na mteja.
Rafiki mbinu hizi ni muhimu sana katika kukusaidia kuepuka kuingia katika kipindi kigumu cha kukuudhi mteja.
Rafiki unaweza kuwashirikisha wengine kuhusu blogu hii kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali na pia unaweza kubofya hapa ili kuweza kupata makala kila inapowekwa kupitia barua pepe yako.

0 comments:

Post a Comment